Teknolojia saidizi ni muarobaini kwa watoto wenye ulemavu- UNICEF

7 Machi 2019

Asilimia 75 ya watoto wenye ulemavu huko Ulaya ya Mashariki na Kati pamoja na Asia ya Kati hawapati elimu bora na jumuishi, limesema shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF hii leo.

Kupitia taarifa yake iliyotolewa leo mjini Geneva, Uswisi, UNICEF imesema idadi hiyo ni sawa na watoto milioni 5.1 ambao imesema wengi wao katu hawajawahi kwenda shuleni.

UNICEF inasema kwa wale ambao wamebahatika kwenda shule, hawanufaiki vya kutosha na elimu bora au hawamailizi elimu ya msingi au sekondari na zaidi ya yote maelfu yao wamesalia kwenye shule maalum wakitengwa na wenzao walio katika shule za kawaida.

Mkurugenzi wa UNICEF kanda ya Ulaya na Asia ya Kati, Afshan Khan amesema hio ni janga na kupoteza uwezo wa watoto hao na familia zao kuchangia katika uchumi wa jamii na taifa.

Amesema ni kwa kuzingatia hilo ndio maana UNICEF inatoa wito kwa uwekezaji wa teknolojia  bunifu, rahisi na saidizi za kuwezesha watoto wenye ulemavu kupata elimu bora.

Teknolojia hizo ni pamoja na kompyuta ndogo mpakato za kuweza hata kusoma kile anachofikiria mtoto kwenye ubongo wake na vitimwendo vyepesi vya kuwawezesha kutembea kwa urahisi ili wawe huru shuleni.

Tayari teknolojia hizo zimewekwa kwenye maonyesho ya siku mbili huko Geneva, Uswisi ambapo Bi.Khan amesema, “kwa kila mtoto anayeishi na ulemavu, teknolojia saidizi zinaweza kuleta mabadiliko makubwa kati ya kutengwa na kujumuishwa kikamilifu shuleni.”

UNICEF inasema katika nchi maskini ni asilimia kati ya 5 hadi 15 tu ya watoto wenye ulemavu ndio wanapata vifaa vyenye teknolojia saidizi.

Shirika hilo limetaja sababu za watoto kukosa vifaa hivyo kuwa ni pamoja na jamii kutofahamu kuwa zipo, teknolojia hizo kutotengenezwa au kutokarabatiwa pale zinapoharibika, idadi kubwa kutofahamu jinsi ya kuzitumia, ukosefu wa utawala bora katika kuamua kuzinunua na pia gharama yake ni ya  juu.

UNICEF imekumbusha kuwa mkataba wa kimataifa wa haki za mtoto, CRC unataka serikali kuwapatia watoto wenye ulemavu teknolojia saidizi ili waweze kunufaika na maisha yao.

Kwa mantiki hiyo shirika hilo linapendekeza mambo makuu matano ili kuhakikisha watoto wenye ulemavu wanapata vifaa hivyo.

Mapendekezo hayo ni mosi, kupitisha sheria na sera za kusaidia watoto kupata teknolojia hizo, pili kutenga fedha na ruzuku ili gharama isiwe ya juu, tatu, kuweka mifumo ya kuhakikisha zinapatikana na zinaweza kukarabatiwa, nne kupatia mafunzo watendaji wa kuhakikisha matumizi ya teknolojia hizo ni endelevu na tano kushirikisha watoto na familia zao kwenye kutunga sera na kubuni teknolojia hizo saidizi.

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter