Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mgogoro wa Israel na Palestina: Ni wakati wa kunyamazisha mtutu wa bunduki: UN

Familia nyingi zimehamia kwenye makambi ya wakimbizi ya Khan Younis Kusini mwa Gaza
© WHO
Familia nyingi zimehamia kwenye makambi ya wakimbizi ya Khan Younis Kusini mwa Gaza

Mgogoro wa Israel na Palestina: Ni wakati wa kunyamazisha mtutu wa bunduki: UN

Msaada wa Kibinadamu

Mratibu mkuu wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya kibinadamu na misaada ya dharura Martin Griffiths anauwakilisha Umoja wa Mataifa kwenye mkutano wa kimataifa wa misaada ya kibinadamu kwa ajili ya  Gaza unaofanyika leo  mjini Paris Ufaransa ili kutoa wito wa kusitishwa kwa mapigano huko Gaza, ukitaka ulinzi zaidi kwa raia waliokimbia makazi yao.

Akiunga mkono kauli hiyo huku Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron akitazama, mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la msaada kwa wakimbizi wa Kipalestina UNRWA, Philippe Lazzarini, amesisitiza kuhusu hali ya "kuvunja moyo inayowakabili watoto katika eneo hilo, ambao aliwaona wiki iliyopita wakiomba kipande cha mkate na maji ya kunywa”.

Kutawanywa kwa idadi kubwa ya watu kumesababisha msongamano mkubwa katika makazi yanayowahifadhi na vitongoji vyote vimegeuzwa kuwa vifusi, amesema Lazzarini, huku kukiwa na mashambulizi makubwa ya anga na ardhini ya Israel kulipiza kisasi kwa mashambulizi mabaya yaliyofanywa na Hamas Oktoba 7.

Kuwalinda raia popote walipo

Bwana Griffiths, ambaye anawakilisha Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika mkutano huo wa ngazi ya juu ameelezea kukutana na familia za baadhi ya watu 240 wanaoshikiliwa mateka na Hamas huko Gaza tangu kundi hilo la wanamgambo kufanya mashambulizi yake ya kigaidi kusini mwa Israel zaidi ya mwezi mmoja uliopita.

Baada ya kuzungumza pia na familia huko Gaza, Bwana. Griffiths amesema kwamba hali hiyo "haiwezi kuungwa mkono na kwamba kuiruhusu iendelee itakuwa ni kosa kubwa.”

Mkuu huyo wa misaada wa Umoja wa Mataifa amesisitiza haja ya dharura ya kusitishwa kwa mapigano kwa ajili ya masuala ya kibinadamu, akisema "kunyamazisha mtutu wa bunduki ni muhimu ili kuwapa afueni raia wa Gaza na kuruhusu huduma muhimu kuanza tena katika eneo hilo”.

Pia ametoa wito wa kulindwa kwa raia popote walipo na akasisitiza kuhusu wasiwasi wake juu ya kuhamishwa na operesheni za jeshi la Israeli kwa mamia ya maelfu ya watu kutoka kaskazini hadi kusini mwa eneo la Gaza kwa kile kinachojulikana kama maeneo salama, ambapo kwa kweli. usalama wao haukuhakikishwa.”

Umoja wa Mataifa hauwezi kuunga mkono pendekezo hili bila dhamana hizo za usalama, amesema.

Kwa mujibu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya kibinadamu OCHA inayoongozwa na Bwana Griffiths, watu wengine 50,000 wameripotiwa kuhama kaskazini mwa Gaza kuelekea kusini jana Jumatano kupitia upenyo uliofunguliwa na jeshi la Israel.

Kutokana na mashambulizi yanayoendelea Ukanda wa Gaza kwenye eneo la Palestina linalokaliwa na Israeli, familia zimeamua kusaka hifadhi kwenye shule zinazoendeshwa na UNRWA.Familia zikiwa zimesaka hifadhi katika shul
© UNICEF/Eyad El Baba
Kutokana na mashambulizi yanayoendelea Ukanda wa Gaza kwenye eneo la Palestina linalokaliwa na Israeli, familia zimeamua kusaka hifadhi kwenye shule zinazoendeshwa na UNRWA.Familia zikiwa zimesaka hifadhi katika shul

Ufikishaji wa misaada zaidi ni muhimu

Katika mkutano huo wa Paris, Bwana Griffiths na Bwana Lazzarini wametoa wito kwa pande zote kuheshimu sheria za kimataifa za kibinadamu katika mzozo huo, ambao tayari umesababisha idadi isiyo ya kawaida ya raia walioathirika, na kupoteza utu wa msingi wa binadamu.

Wametoa wito wa upatikanaji usiozuiliwa wa fursa ya mamia zaidi ya mlori ya misaada kuleta chakula, maji, vifaa vya matibabu na mafuta kwa wakazi wa Gaza waliokata tamaa.

"Kuweka vikwazo vikali vya chakula, maji na dawa ni adhabu ya pamoja, ambayo ni ukiukaji wa sheria za kimataifa, ameonya Bwana Lazzarini wa UNRWA.

Viongozi hao wawili wa Umoja wa Mataifa pia wamependekeza kufunguliwa kwa vivuko vya ziada vya mpaka kusaidia, ikiwa ni pamoja na Kerem Shalom kwenye mpaka na Israel, kwani kiasi cha msaada unaokuja kupitia kivuko cha Rafah kutoka Misri bado hautoshi.

Ili kutoa huduma za kibinadamu katika kukabiliana na mahitaji yanayoongezeka, mapema wiki hii, Umoja wa Mataifa na washirika wake walitoa ombi la ufadhili wa dola bilioni 1.2 kwa lengo la kuongeza shughuli za kibinadamu kusaidia watu milioni 2.2 katika Ukanda wa Gaza na wengine 500,000 katika Ukingo wa Magharibi. .

Na kusaidia kuhamasisha ufadhili huu ni miongoni mwa malengo ya mkutano huo wa Paris.

Mgonjwa akipatiwa huduma katika chumba cha upasuaji kwenye hospitali ya Al-Quds Gaza
© WHO
Mgonjwa akipatiwa huduma katika chumba cha upasuaji kwenye hospitali ya Al-Quds Gaza

UNRWA ndio mwanga wa mwisho wa matumaini

Bwana Lazzarini ametoa wito kwa wafadhili kuongeza msaada kwa raia wa Gaza akisisitiza kwamba UNRWA ni mwanga wa mwisho wa matumaini kwa raia katika eneo hilo, wakati wafanyakazi wanaendelea kusambaza chakula na maji na kuwahudumia watu katika makazi na hospitali, licha ya hatari inayowakabili.

UNRWA ni shirika la Umoja wa Mataifa, ambalo limelipa gharama kubwa zaidi katika mzozo huu kwani wafanyikazi wake 99 wameuawa huko Gaza,na ameonya kwamba shirika hilo halitaweza kulipa mishahara ya wafanyikazi wake ifikapo mwisho wa mwaka.

Hofu ya kusambaa mzozo kikanda

Akigeukia eneo pana zaidi, Bwana Griffiths amesema kwamba hatuwezi kupuuza maonyo ya kuongezeka zaidi kwa mzozo, akitoa mfano wa matukio ya hivi karibuni ya ghasia nchini Lebanon na Yemen. Pia ameelezea wasiwasi wake juu ya kuongezeka kwa kauli za chuki dhidi ya Wayahudi na Uislamu.

Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa wa misaada ya kibinadamu amesisitiza jukumu muhimu la juhudi za kidiplomasia za kimataifa kulinda raia, kuhakikisha upatikanaji wa misaada na kuwezesha kuachiliwa kwa mateka.