Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mafuriko makubwa mashariki mwa Afrika tishio kwa uhakika wa chakula – WFP

Watoto wakisafirishwa kwenye maji ya mafuriko kwenye pipa la plastiki katika Jimbo la Hirshabelle, Somalia.
© WFP/Arete/Abdirahman Yussuf Mohamud
Watoto wakisafirishwa kwenye maji ya mafuriko kwenye pipa la plastiki katika Jimbo la Hirshabelle, Somalia.

Mafuriko makubwa mashariki mwa Afrika tishio kwa uhakika wa chakula – WFP

Tabianchi na mazingira

Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) linaonya kuwa mafuriko makubwa yanatishia kuongeza zaidi tatizo la kukosekana kwa uhakika wa chakula katika eneo la Mashariki mwa Afrika ingawa shirika hilo linajitahidi kusambaza misaada. 

Mabadiliko ya tabianchi yanaendelea kuleta maafa katika eneo la Mashariki mwa Afrika, eneo ambalo lina uchangiaji mdogo katika uzalishaji wa hewa chafuzi lakini likiwa eneo ambalo linabeba mzigo mkubwa wa dharura ya tabanchi duniani. Baada ya ukame mkali kati ya mwaka 2020 na 2022, sasa ni mvua asilimia 140 juu ya viwango vya kawaida.

Kwa mujibu wa WFP, takriban watu milioni 3 wameathiriwa, huku zaidi ya watu milioni 1.2 wakilazimika kuyahama makazi yao. Somalia, Ethiopia, na Kenya ndizo zinazobeba mzigo mkubwa wa janga hili, zikifuatiwa kwa karibu na Sudan, Sudan Kusini, Burundi, na Uganda na sasa Tanzania ambayo tukio la hivi karibuni ni maporomoko ya udongo katika Mlima Hanang, huko kaskazini mwa nchi. Kwa bahati mbaya, mvua zinatarajiwa kuendelea kote mashariki mwa Afrika hadi mapema mwaka 2024.

Petroc Wilton wa WFP Somalia anasema, "El Niño na janga la tabianchi vimepeleka athari mbaya katika maeneo mengi ya Afrika Mashariki. Tumeona mfululizo wa majanga ya tabianchi. WFP hapa Somalia tunatumia boti, tunatumia helikopta kufikisha msaada wa kuokoa maisha kwa watu wenye uhitaji zaidi.”