Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Njaa kuongezeka mara mbili Afrika Mashariki na Pembe ya Afrika sababu ya COVID-19:WFP

Chakula kutoka mpango wa chakula duniani FAO kikipakiwa katika meli kutoika Djibout hadi Yemen.
OCHA/Charlotte Cans
Chakula kutoka mpango wa chakula duniani FAO kikipakiwa katika meli kutoika Djibout hadi Yemen.

Njaa kuongezeka mara mbili Afrika Mashariki na Pembe ya Afrika sababu ya COVID-19:WFP

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Ripoti mpya iliyotolewa na shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani WFP, kuhusu athari za kijamii na kiuchumi za janga la corona au COVID-19,  imeonyesha kuwa tatizo la njaa linaweza kuongezeka zaidi ya mara mbili katika enchi za Afrika Mashariki na Pembe ya Afrika katika miezi mitatu ijayo. 

Kwa mujibu wa ripoti hiyo iliyotolewa leo mjini Nairobi Kenya watu walio katika hatari zaidi  ni masikini wanaoishi katika jamii za mijini ambao wanategemea kipato cha siku kwa ajili ya mlo kutoka kwenye sekta zisizo rasmi na mamilioni ya wakimbizi wanaoishi katika makambi yaliyofurika kwenye ukanda huo.


WFP inasema takribani watu milioni 20 tayari walikuwa wanakabiliwa na kutokuwa na uhakika wa chakula hata kabla ya COVID-19 kuwasili Afrika Mashariki na Pembe ya Afrika, kutokana na mgogoro mkubwa wa chakula, mlipuko wa nzige wa jangwani na mafuriko makubwa yanayotishia maisha ya mamilioni ya watu hasa katika nchi za Ethiopia, Sudan Kusini, Kenya, Somalia, Uganda, Rwanda, Burundi, Djibout na Eritrea.


Ripoti hiyo inakadiria kwamba idadi ya watu wasio na uhakika wa chakula katika ukanda huo inatarajiwa kuongezeka kati ya milioni 34 na milioni 43 kuanzia mwezi huu wa Mei hadi Julai kutokana na athari za kiuchumi na kijamii za COVID-19.


Na endapo idadi hiyo itafikia milioni 43 basi itakuwa imeongezeka zaidi ya mara mbili na miongoni mwa walio na tatizo la njaa ni wakimbizi milioni 3.3 wanaoishi katika nchi 9 za ukandaka huo.


Kwa mujibu wa Clementine Nkweta Salami Mkurugenzi wa kikanda wa UNHCR, “ukata wa fedha za ufadhili tayari unamaanisha kwamba wakimbizi wengi katika eneo hilo hawapokei mahitaji yao yote ya chakula na watakabiliwa na kupunguziwa zaidi mgao huo kwa sababu ya kukosekana kwa rasilimali fedha.”


Ameongeza kuwa kiwango kikubwa cha utapiamlo katika makambi na makazi ya wakimbizi kinawaweka wakimbizi hao katika hatari ya maambukizi ya COVID-19, lakini pia baadhi ya wakimbizi wanaoishi maeneo ya mijini ambapo mara nyingi ni katika mitaa ya mabanda au makazi duni ni sehemu kubwa ya watu masikini katika nchi hizo tisa.


Naye naibu mkurugenzi wa kikanda wa WFP Brenda Behan amesema, “watu zaidi wanatarajiwa kufa kutokana na athari za kiuchumi na kijamii za COVID-19 kuliko virusi vyenyewe, na wakimbizi na watu masikini wanaoishi mijini katika ukanda huu wako katika hatari kubwa zaidi”. 


Ripoti imesema watu milioni 25 Afrika Mashariki na Pembe ya Afrika wanaishi kwa kutegemea kipato cha siku wakiishi kwenye mitaa ya mabanda au makazi duni. Na mamilioni wameshapoteza ajira  kutokana na hatua za kutotembea au kusalia majumbani kupambana na COVID-19. 

Tayari WFP ina ukurasa wake wa wavuti ambao unaonesha mubashara hali ya njaa katika maeneo mbalimbali duniani. 


Hivi sasa WFP inasema ina pengo la dola milioni 103 ili kuweza kutoa mgao wa chakula au fedha taslim kwa wakimbizi zaidi ya milioni 3 katika nchi tisa za ukanda huo mgao utakaoweza kuwafikisha mwezi Septemba.