Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mamilioni ya watu kulala njaa Afrika Mashariki: WFP

Sabirin, mwenye umri wa miaka miwili ni binti ya Khadijo Mohamed Aden. Hapa  yuko nje ya makazi yao ya muda kwenye kambi ya wakimizi nje kidogo ya mji mkuu wa Somalia, Mogadishu.
© UNICEF/UN0719419/Yusuf
Sabirin, mwenye umri wa miaka miwili ni binti ya Khadijo Mohamed Aden. Hapa yuko nje ya makazi yao ya muda kwenye kambi ya wakimizi nje kidogo ya mji mkuu wa Somalia, Mogadishu.

Mamilioni ya watu kulala njaa Afrika Mashariki: WFP

Tabianchi na mazingira

Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani  WFP leo lilionya kwamba katika eneo la Afrika Mashariki, migogoro, bei ya juu ya chakula na majanga ya tabianchi vinaendelea kuwaacha mamilioni ya watu bila kujua mlo wao unaofuata utatoka wapi.

Shirika hilo lilisema hadi mwisho wa mwezi Septemba watu milioni 62.6 katika eneo hilo walikuwa na uhaba wa chakula, huku Ethiopia, Somalia, Sudan Kusini na Sudan zikiwa miongoni mwa nchi zenye majanga mbaya zaidi ya chakula duniani.

Kwa mujibu wa WFP nchi zote nne zimekuwa zikikumbwa na migogoro au kuongezeka kwa ghasia, na kuwafanya watu kuyakimbia makazi yao. 

Zaidi ya watu milioni 18 katika eneo hilo wamekimbia makazi yao ikiwa ni pamoja na watu milioni 12 ambao ni wakimbizi wa ndani ya nchi zao na wengine milioni tano ambao wamevuka mipaka ya kimataifa na kuwa wakimbizi kwingineko.

Mfumuko wa bei ni zaidi ya asilimia 13

Gharama kubwa za chakula na maisha zinaendelea Afrika Mashariki huku mfumuko wa bei ukiwa wastani wa asilimia 13.2.

WFP inasema wakati viwango rasmi vya mfumuko wa bei kwa Sudan iliyokumbwa na vita havijatolewa tangu Februari, "vinatarajiwa kuzidi asilimia 300 ifikapo mwisho wa mwaka huu".

Shirika hilo la Umoja wa Mataifa linasisitiza kuwa hali hiyo mbaya huenda ikaendelea hadi mwanzoni mwa mwaka 2024.

Mfumo wa hali ya hewa wa El Niño unatarajiwa kuleta mvua zaidi ya kawaida hadi mwezi Januari, ambayo inaweza kuwa neema kwa kilimo, hata hivyo WFP imeonya kwamba mafuriko makubwa katika maeneo ya tambarare ya Somalia, Ethiopia na Uganda yanaweza kutishia mazao na mifugo, kusababisha watu kuhama zaidi na kusababisha milipuko ya magonjwa ya kuambukiza.