Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mashirika ya kibinadamu yanahaha kuwasaidia waathirika wa tetemeko la ardhi Afghanistan:UN

Msaada wapelekwa kwenye maeneo yaliyiathirika na tetemeko Magharibi mwa Afghanistan
© UNICEF/Sharifa Khan
Msaada wapelekwa kwenye maeneo yaliyiathirika na tetemeko Magharibi mwa Afghanistan

Mashirika ya kibinadamu yanahaha kuwasaidia waathirika wa tetemeko la ardhi Afghanistan:UN

Msaada wa Kibinadamu

Mashirika ya Umoja wa Mataifa na washirika wa misaada ya kibinadamu wanaongeza juhudi za kukabiliana na athari za tetemeko la ardhi lenye ukubwa wa 6.3 katika kipimo cha Richter lililotokea jimbo la Herat, magharibi mwa Afghanistan mwishoni mwa wiki.

Juhudi za utafutaji na uokozi zinaendelea, huku timu za tathmini za haraka za sekta mbalimbali zikipelekwa katika maeneo yaliyoathirika kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa kuratibu misaada ya kibinadamu na masuala ya dharura OCHA.

Takwimu za shirika hilo zinasema “hadi kufikia sasa, watu 1,023 wanaripotiwa kupoteza Maisha na watu 1,663 kujeruhiwa katika vijiji kumi na moja vya wilaya ya Zindajan, Mkoa wa Herat, ambapo asilimia 100 ya nyumba zinakadiriwa kusambaratishwa kabisa. Watu wengine 516 wakiwemo wanaume 203 na wanawake 213 wanaripotiwa kutoweka katika wilaya hiyo.”

Pia shirika hilo limesema kwa jumla, watu 11,585 ambao ni sawa na familia 1,655 wametathminiwa kuwa wameathirika hadi sasa katika wilaya ya Zindajan ambapo familia 1,320, na Injil familia 150, Gulran familia 95, Kohsan familia 60 na wilaya ya Kushk Robat-e-Sagani familia 30. 

OCHA imesema idadi ya majeruhi na kaya zilizoathirika inatarajiwa kuongezeka kadri maeneo ya mbali yanavyofikiwa na tathmini kukamilika.

Wafanyakazi wa UNICEF wakitathmini uharibifu wa tetemeko la ardhi katika kijiji cha Karinal, mkoani Herat nchini Afghanistan.
© UNICEF/Rebecca Phwitiko
Wafanyakazi wa UNICEF wakitathmini uharibifu wa tetemeko la ardhi katika kijiji cha Karinal, mkoani Herat nchini Afghanistan.

UNICEF inazisaidia familia zilizoathirika

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF katika ukurasa wake wa X limesema Limetuma vifaa 10,000 vya usafi, seti 5,000 za vifaa vya familia, seti 1,500 za nguo za msimu wa baridi, pamoja na mablanketi, maturubai 1,000 na vifaa vya michezo ya watoto navya msingi vya matumizi ya nyumbani vinavyohitajika sana.

Shirika hilo limeongeza kuwa msaada huo utaunganishwa na misaada inayotolewa na mshirika mingine ya Umoja wa Mataifa na washirika wake kuwapunguzia madhila Waafghanistan walioathirika na tetemeko hilo kubwa.

Takriban familia 1,700 zimeathirika na tetemeko hilo kwa mujibu wa UNICEF na nyingi zimepoteza kila kitu.

Mwakilishi wa UNICEF nchini Afghanistan Fran Equiza amesema UNICEF iko tayari kushikamana na watu wa Afghanistan katika wakati huu mgumu. 

Mfanyakazi wa UNICEF akitoa msaada kufuatia tetemeko la ardhi kwenye jimbo la Herat Afghanistan
© UNICEF/Rebecca Phwitiko
Mfanyakazi wa UNICEF akitoa msaada kufuatia tetemeko la ardhi kwenye jimbo la Herat Afghanistan

Familia 700 zimepokea msaada wa UNHCR na IOM

Nayo mashirika ya Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR na la wahamiaji IOM kwa kushirikiana na wadau wengine wa misaada wanatoa makazi makazi ya dharura kusaidia familia 700, msaada huo ukijumuisha mahema 640, mablanketi na vifaa vingine visivyo chakula ambavyo vinahitajika sana na waathirika.

Mashirika hayo yamesema yataendelea kufanyakazi kwa karibu na mashirika mengine ya Umoja wa Mataifa nay a misaada ili kuhakikisha waathirika wanapatiwa msaada wanaouhitaji sana.

Zaidi ya kliniki tembezi 50 zinawahudumia waathirika

Nalo shirika la afya la Umoja wa Mataifa WHO limesema kutokana na ukubwa wa tetemeko lenyewe athari ni kubwa sana.

Akizungumza na UN News leo Alaa Abouzeid kiongozi wat imu ya dharura ya WHO nchini Afghanistan amesema "Kwa bahati mbaya, kiwango cha dharura ni kikubwa na ukubwa ni wa hali ya juu. Sio kama wengine walivyofikiria mwanzoni kwamba uharibifu ni mdogo, na idadi ya waathiriwa ni ndogo. Mamlaka za eneo la hapa Kabul zimetangaza kuwa vifo ni zaidi ya 2,400. Hizi ni takwimu za jana. Hatujapokea takwimu mpya."

Alaa Abouzeid  ameongeza kuwa "Zaidi ya timu 50 tembezi za huduma za afya zinatoa huduma za aina tofauti kwa watu katika ngazi ya afya ya msingi. Kuna magari ya kubeba wagonjwa kumi na mbili ambayo hutumika kuhamisha wagonjwa walio jeruhiwa vibaya hadi hospitalini”