Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tetemeko la ardhi nchini Afghanistani: Umoja wa Mataifa uko tayari kusaidia

Waafghani wengi ambao wamekimbia makazi yao kutokana na migogoro wamehamia Herat magharibi mwa Afghanistan.
© OCHA/Linda Tom
Waafghani wengi ambao wamekimbia makazi yao kutokana na migogoro wamehamia Herat magharibi mwa Afghanistan.

Tetemeko la ardhi nchini Afghanistani: Umoja wa Mataifa uko tayari kusaidia

Tabianchi na mazingira

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesikitishwa sana na watu kupoteza maisha katika tetemeko la ardhi lililotokea karibu na mji wa Herat magharibi mwa Afghanistani Jumamosi. 

Hayo yamesemwa katika taarifa iliyotolewa na msemaji wake, "Katibu Mkuu anaeleza mshikamano na watu wa Afghanistani, anatoa rambirambi za dhati kwa familia za kwa waathirika na anawatakia ahueni ya haraka waliojeruhiwa." 

Kulingana na makadirio ya awali, tetemeko la ardhi lenye ukubwa wa 6.3 huko Herat limeua wakazi wasiopungua mia moja wa vijiji nane na kujeruhi watu wengine 500. Kwa mujibu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Masuala ya Kibinadamu (OCHA), nyumba 465 zimesambaratishwa na nyingine 135 kuharibiwa. 

Ofisi ya Msemaji wa Katibu Mkuu inaeleza kwamba Umoja wa Mataifa na wadau wake nchini Afghanistan wanashirikiana na viongozi wan chi ili kwa haraka kutathimini mahitaji ya msaada na kuanza kutoa msaada.  

Katibu Mkuu ametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuungana na kusaidia watu walioathiriwa na tetemeko la ardhi Afghanistani na akasisitiza kwamba wengi wa walioathirika tayari walikuwa katika uhitaji wa msaada hata kabla ya janga hilo la asili hususani katika kipindi hiki ambacho majira ya baridi yanakaribia.