Tushikamane tusaidie Afghanistan - Guterres

22 Juni 2022

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameeleza kusikitishwa na tukio baya la vifo viliyosababishwa na tetemeko la ardhi lililoikumba Afghanistan mapema leo  karibu na mji wa Khost na akahamisha mshikamano kutoka jumuiya ya kimataifa.  

Mamia ya watu wameripotiwa kufariki dunia na wengine kujeruhiwa, na idadi hii ya kusikitisha inaweza kuendelea kuongezeka. 

Kupitia taarifa iliyotolewa leo jumatano jijini New York, Marekani, na msemaji wake, Bwana Gurerres kwa masikitiko amesema moyo wake uwaendee watu wa Afghanistan ambao tayari wanateseka kutokana na athari za miaka mingi ya migogoro, matatizo ya kiuchumi na njaa. 

“Natuma salamu zangu za rambirambi kwa familia za waathirika na kuwatakia ahueni ya haraka waliojeruhiwa,” amesema akiongeza kuwa, “Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan umejipanga kikamilifu. Timu zetu tayari ziko katika eneo kutathmini mahitaji na kutoa usaidizi wa awali.” Ameeleza Guterres.  

Aidha Guterres ameeleza kuwa wanategemea jumuiya ya kimataifa kusaidia mamia ya familia zilizokumbwa na janga hili la hivi punde. “Sasa ni wakati wa mshikamano.” Amesisitiza Guterres.  

Kilichotokea

Kwa mujibu wa taarifa ya OCHA iliyotolewa mjini Geneva Uswisi tetemeko hilo lililotokea usiku wa manane kuamkia leo kwa saa za Afghanistan lilikuwa na ukubwa wa 5.9 katika kipimo cha Richa na lilitikisa pia maeneo mengine ikiwa ni pamoja na mji mkuu wa Afghanistan, Kabul, halikadhalika, Islamabad nchini  Pakistan pamoja na India. 

Juhudi za misaada limesema shirika hilo zinaijumuisha pia ofisi ya Afghanistan ya masuala ya kibinadamu na kudhibiti majanga ANDMA. 

Wilaya nyingi za majimbo hayo mawili zimeathirika sana ikiwemo Bermal, Zerok, Nika na  Gayan jimboni Paktika na Spera jimboni Khost.  

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter