Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto na familia wako hatarini baada ya tetemeko la ardhi Afghanistani: UNICEF

Wafanyakazi wa UNICEF wakitathmini uharibifu wa tetemeko la ardhi katika kijiji cha Karinal, mkoani Herat nchini Afghanistan.
© UNICEF/Rebecca Phwitiko
Wafanyakazi wa UNICEF wakitathmini uharibifu wa tetemeko la ardhi katika kijiji cha Karinal, mkoani Herat nchini Afghanistan.

Watoto na familia wako hatarini baada ya tetemeko la ardhi Afghanistani: UNICEF

Msaada wa Kibinadamu

Jana Jumamosi kwenye saa tano asubuhi saa za Afghanistani, tetemeko la ardhi la kipimo cha 6.3 na mitetemeko kadhaa mikali ya baadaye ilitikisa magharibi mwa Afghanistani katika majimbo ya Herat, Badghis na Farah. Baadhi ya maeneo yaliyoathirika zaidi ni kilomita 40 tu kutoka mji wa Herat. 

“Kiwango kamili cha uharibifu bado hakijajulikana, lakini makadirio ya awali yanaonyesha kuwa mamia kadhaa ya watu wakiwemo wanawake na watoto, wamepoteza maisha au kujeruhiwa.” Inaeleza taarifa ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto, UNICEF iliyotolewa katika mji Mkuu wa Afghanistani, Kabul.  

"Ngoja nitoe rambirambi zetu za dhati kwa familia zinazoomboleza kupoteza wapendwa wao," anasema Fran Equiza, Mwakilishi wa UNICEF nchini Afghanistani. "Pamoja na washirika wetu, tutafanya kila juhudi kuleta nafuu ya haraka kwa walioathirika," anaeleza. 

Timu za UNICEF ziko tayari kusaidia kufanya tathmini za ziada. Waliojeruhiwa wanatibiwa katika vituo vya afya vilivyo karibu, na dawa za dharura zinazotolewa na UNICEF na wadau. UNICEF pia inatoa mahema ya dharura kwa kliniki za afya zilizoelemewa na mizigo. 

UNICEF imetuma vifaa 10,000 vya usafi, seti 5,000 za familia, seti 1,500 za nguo za msimu wa baridi, pamoja na blanketi, turubai 1,000 na vifaa vya nyumbani, ambavyo vitasaidia msaada unaotolewa na mashirika mengine ya Umoja wa Mataifa na washirika. 

"Kama kawaida, UNICEF inasimama katika mshikamano na watu wa Afghanistani wakati huu mgumu," anahitimisha Equiza.