Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Idhinisheni ujumbe wa kuimarisha usalama Haiti; Biden aliambia Baraza la Usalama UN

Rais Joe Biden wa Marekani akihutubia Mjadala Mkuu wa mkutano wa 78 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani 19 Septemba 2023.
UN /Cia Pak
Rais Joe Biden wa Marekani akihutubia Mjadala Mkuu wa mkutano wa 78 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani 19 Septemba 2023.

Idhinisheni ujumbe wa kuimarisha usalama Haiti; Biden aliambia Baraza la Usalama UN

Masuala ya UM

Kuunga mkono utayari wa Kenya kuongoza ujumbe wa kipolisi unaoungwa mkono na Umoja wa Mataifa nchini Haiti na suala la nafasi ya umoja katika kukabili changamoto zinazokabili dunia hivi sasa ni miongoni mwa mambo aliyogusia Rais wa Marekani Joe Biden wakati akihutubia siku ya kwanza ya Mjadala Mkuu wa mkutano wa 78 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani.

Tweet URL

Rais Biden amesema “na tunakumbatia mataifa ambayo yanaingilia kati kuongoza njia mpya na kusaka majawabu ya mambo magumu. Mfano kuhusu Haiti Jumuiya ya  Wakaribea wanaoratibu maelewano baina ya wahaiti, namshukuru Rais Ruto wa Kenya, namshukuru kwa utayari wake wa kuwa taifa ongozi la ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa usaidizi wa usalama.”

Ametoa wito kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuidhinisha ujumbe huo hivi sasa kwani wananchi wa Haiti hawawezi kusubiri zaidi. 

Mwezi Oktoba mwaka jana, kiongozi wa Haiti alitoa wito kwa jamii ya kimataifa kusaidia kuunda kikosi maallum cha kukabili ghasia za magenge nchini humo ambazo zinaongezeka kila uchao, ombi ambalo Kenya ilipokea na likakaribishwa pia na Katibu Mkuu wa UN.

Katika hotuba yake hiyo ya takribani nusu saa, Rais Biden amesema kwa changamoto za sasa zinazokabili dunia, hakuna taifa linaloweza kuzikabili pekee, bali kwa ushirikiano.

Lakini amesema kukabili changamoto hizo, taasisi za zamani lazima ziende na wakati, kwa kuleta uongozi kutoka maeneo mengine ambayo yamekuwa yakienguliwa kwenye chombo  kama vile Baraza la Usalama.

“Nikihutubia mkutano kama huu mwaka jana nilitangaza msimamo wa Marekani wa kuunga mkono kupanua Baraza la Usalama kwa kuongeza idadi ya wajumbe wa kudumu na wasio wa kudumu,” amesema Rais Biden akiongeza kuwa tayari wamekuwa na majadiliano ya kina na nchi nyingi na wataendelea kujadili marekebisho na kufanikisha hoja hiyo miaka ijayo.

Ametaka Umoja wa Mataifa uendelee kulinda amani na kuzuia mizozo na wakati huo huo kusimamia manufaa na changamoto za teknolojia zinazoibuka ikiwemo Akili Mnemba, AI.

Kutazama hotuba yote bofya hapa