Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sikufahamu jinsi ya kuzungumza na mwanangu kumuepusha na mimba za utotoni- Mzazi Haiti

Mwanamke akiwa amesimama mbele ya nyumba yake kwenye eneo la watu waliohamishwa huko Port-au-Prince, Haiti.
IOM
Mwanamke akiwa amesimama mbele ya nyumba yake kwenye eneo la watu waliohamishwa huko Port-au-Prince, Haiti.

Sikufahamu jinsi ya kuzungumza na mwanangu kumuepusha na mimba za utotoni- Mzazi Haiti

Afya

Hebu fikiria kutarajia kupata mtoto wakati ambapo hata hufahamu neno ujauzito lina maana gani. Hicho ndicho kilichomfika mtoto mwenye umri wa miaka 14 nchini Haiti ambaye alijikuta anapewa ujauzito na kaka wa rafiki ya kiume wa rafiki yake. Hakuwa anajitambua akakubali kumsindikiza rafiki yake na zaidi ya yote akakubali urafiki na kijana huyo mwenye umri wa miaka 16. 

Nina umri wa miaka 14, ndivyo anavyoanza kusema mtoto huyu wa kike mkazi wa jimbo la Kusini-Mashariki nchini Haiti.

Yeye ni miongoni mwa watoto waliotumbukia kwenye ujauzito katika umri mdogo. Anaendelea na simulizi yake akiwa amefichwa sura kwenye video hii ya shirika la Umoja wa Mataifa la Afya  Uzazi na Idadi ya watu duniani, UNFPA nchini Haiti.

Anasema niko darasa la tano. Siku moja rafiki yangu aliniomba nimsindikize kumtembelea rafiki yake wa kiume. Bila kusita nikakubali. Tukiwa huko akaniomba nianze urafiki na kaka ya rafiki yake huyo wa kiume. Nami nilikubali.Kaka huyo alikuwa na umri wa miaka 16.”

Akiwa nyumbani kwao mtoto huyu anazungumza akiwa amefunika uso wake, na mama yake aitwaye Fifi amepigwa butwaa amesimama kwenye mlango nje ya nyumba yao, taswira ya uso wake ni dhahiri kuwa amegubikwa na sintofahamu.  

Fifi anasema “ni mwanangu wa nne kuzaliwa. Nilimfuatilia kwa wiki kadhaa nikaona wiki zimepita bila ya yeye kupata hedhi. Nikagundua kuwa hakupata hedhi na alikuwa mjamzito.”

Mama amzuia mwanae kwenda shuleni kisa ujauzito

Kisha video ya UNFPA inatuonesha Fifi na binti yake wakiingia ndani na sasa binti huyu amegeukia ukuta anasema, “mama hakuniruhusu tena kwenda shuleni. Marafiki zangu nao walinitelekeza, hawakuniona tena mimi kama rafiki yao. Sikufahamu kuwa mjamzito kulimaanisha nini. Hivyo mama yangu alinifafanulia kinagaubaga. Mama alinieleza kuwa maana yake ni kwamba nitapata mtoto.”

Ujauzito wa binti huyo ukiwa katika wiki ya 33 alipata shinikizo la damu na hivyo ililazimu madaktari wamfanyie upasuaji kumtoa mtoto tumboni ili kuokoa uhai wa mama na mtoto.

UNFPA inasema shinikizo la damu ni miongoni mwa sababu kuu zinazotishia uhai kwa watoto wenye ujauzito. Fifi mama yake binti huyu akiwa nyumbani kwao anazungumza kwa hisia Kali akisema “tulimpeleka hospital ya Anse-Pitre. Na alikuwa hajitambui kwa siku nane. Sikufahamu jinsi ya kuzungumza na binti yangu kuhusu wanaume na kujamiiana, au uhusiano na wanaume ili kuepusha mimba katika umri mdogo.?"

Baada ya kujifungua sasa anataka kurejea shule na ndoto ya udaktari

Wahenga walisema kukosea si kosa bali kosa ni kurudia kosa! Sasa binti huyu ambaye jina lake limehifadhiwa, halikadhalika sura yake anasema, nataka kurejea shuleni nikaendelee na masomo. Na nikiwa mkubwa ndoto yangu ni kuwa daktari.”

Katika video hii, tamati yake ni darasa ambamo anaonekana mtaalamu akiendesha somo kwa watoto wa kike na wasichana.

Ujauzito utotoni unagharimu fursa, uhai na maendeleo ya mtoto wa kike

UNFPA inasema mimba katika umri mdogo zinaweza gharimu watoto wa kike uhai wao, elimu na kujiendeleza kiajira.

Ni kwa mantiki hiyo, shirika hili la Umoja wa Mataifa la Idadi ya watu na Afya ya uzazi linapigia chepuo elimu ya kina kuhusu viungo vya uzazi na afya ya uzazi ili watoto wa kike waweze kufikia kiwango cha juu kabisa cha ustawi wao.