Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Dunia iko kitanzini katika mabadiliko ya tabianchi yaonya UN

Wanasayansi wanaamini kwamba mabadiliko ya tabianchi yanasababisha matukio memngi mabaya ya hali ya hewa
NOAA/Jerry Penry
Wanasayansi wanaamini kwamba mabadiliko ya tabianchi yanasababisha matukio memngi mabaya ya hali ya hewa

Dunia iko kitanzini katika mabadiliko ya tabianchi yaonya UN

Tabianchi na mazingira

Viongozi wa dunia lazima wachukue hatua sasa na kuiweka sayari kwenye njia inayojali mazingira kwa sababu "tunaelekea kitanzini", ameonya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres leo katika hotuba yake kwenye mkutano wa mabadiliko ya tabianchi ulioitishwa na Rais wa Marekani Joseph Biden.

Guterres ameongeza kuwa "Mama asili hasubiri, kwani muongo mmoja uliopita ulikuwa wenye joto zaidi katika historia na dunia inaendelea kushuhudia kupanda kwa vina vya bahari, joto kali kupita kiasi, vimbunga vikubwa vya kitropiki na moto waaina yake wa nyikani.
Amesisitiza kuwa "Tunahitaji sayari yenye mazingira bora lakini ulimwengu uko kwenye hatua ya hatari. Tuko kwenye hatihati ya kutumbukia shimoni. Lazima tuhakikishe hatua inayofuata iko katika mwelekeo sahihi. Viongozi kila mahali lazima wachukue hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi”

Katibu Mkuu wa UN Antonio Guterres akihutubia mkutano wa viongozi kusuhu mabadiliko ya tabianchi ulioitishwa na Rais Joe Biden wa Marekani
UN Photo/Evan Schneider
Katibu Mkuu wa UN Antonio Guterres akihutubia mkutano wa viongozi kusuhu mabadiliko ya tabianchi ulioitishwa na Rais Joe Biden wa Marekani


Ahadi na uwekezaji wa Marekani

Katibu Mkuu amemshukuru Rais Biden wa Marekani kwa kuandaa mkutano huo wa siku mbili wa viongozi kuhusu mabadiliko ya tabianchi, na amepongeza ahadi ya Marekani kupunguza uzalishaji wa gesi chafuzi.
Katika hotuba yake ya ufunguzi wa mkutano, Rais Biden ametangaza kuwa nchi yake itapunguza uzalishaji wa hewa chafuzi kwa nusu, ifikapo mwaka 2030. 
Amezungumzia juu ya "ubunifu wa fursa za ajira na fursa za kiuchumi ambazo zinaletwa na hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi, akipendekeza uwekezaji katika sekta kama nishati, usafirishaji, ujenzi na kilimo.”
Rais Biden amekiri kwamba hakuna taifa linaloweza kutatua hali ya dharura ya mabadiliko ya tabianchi peke yake, na ametaka viongozi wa uchumi mkubwa zaidi ulimwenguni waongeze juhudi katika kinyang'anyiro hicho ili kuwa na mustakabali endelevu.
“Wanasayansi wanatuambia kwamba huu ni muongo wa maamuzi. Huu ni muongo ambao lazima tuchukue maamuzi ambayo yataepusha athari mbaya za mgogoro wa mabadiliko ya tabianchi” amesema Rais Biden.

Kijiji kikiwa kimeathiriwa na mafuriko katika jimbo al Khartoum, Sudan.
UNOCHA
Kijiji kikiwa kimeathiriwa na mafuriko katika jimbo al Khartoum, Sudan.

Muungano wa kutozalisha hewa ukaa

Bwana Guterres ametumia mkutano huo kusisitiza wito wake wa muungano wa kimataifa wa kufanikisha lengo la kutozalisha kabisa hewa ukaa ifikapo mwaka 2050, na kwa nchi kuongeza ahadi zao chini ya mkataba wa kihistoria wa Paris kuhusu mabadiliko ya tabianchi.
Mkataba wa mwaka 2015 unakusudia kupunguza kiwango cha joto ulimwenguni hadi chini ya nyuzi joto 1.5 Celsius juu ya viwango vilivyokuwa kabla ya mapinduzi ya viwanda, na unahitaji serikali kujitolea kuchukua hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi yanayozidi kuongezeka kupitia mpango unaojulikana kama michango ya kitaifa (NDCs).
Katibu Mkuu ameongeza kuwa "Nchi zote kuanzia watoaji wakubwa wa hewa chafuzi zinapaswa kuwasilisha michango yao mipya na yenye malengo ya kitaifa ya kupunguza kwa kiasi kikubwa hewa ukaa, kukabiliana na changamoto za fedha kwa kuwekeza, na kuweka mipango na sera za  miaka 10 ijayo ili kuweza kutimiza lengo la mwak 2050".
Ahadi hizi pia zinapaswa kutafsirika kuwa "hatua thabiti, na za haraka", ameongeza Guterres, kwani inakadiriwa kuwa chini ya robo ya matumizi ya kujikwamua na janga la COVID-19 zitaenda katika kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa au kuimarisha mitaji ya asili.

Mfugaji kaskazini mwa Somalia katika jimbo lililokumbwa na ukame, alipoteza takribani nusu ya kondoo wake ambao walikuwa wamefikia 70.
Photo: UNICEF/Sebastian Rich
Mfugaji kaskazini mwa Somalia katika jimbo lililokumbwa na ukame, alipoteza takribani nusu ya kondoo wake ambao walikuwa wamefikia 70.


Kukopa kutoka siku zijazo

“Matrilioni ya dola zinahitajika ili kujikwamua na athari za COVID-19,  ni pesa tunazokopa kutoka vizazi vijavyo. Hatuwezi kutumia rasilimali hizi kuweka sera ambazo zitawabebesha mzigo wa madeni katika sayari iliyosambaratika. " Amesema Katibu Mkuu.
Pia ametoa wito kwa viongozi kuweka bei kwenye hewa ukaa kupitia ushuru. Ametoa wito wa kumaliza ruzuku kwa mafuta kisukuku na badala yake, kuongeza uwekezaji katika nishati mbadala na miundombinu inayojali mazingira.
“Acheni ufadhili wa makaa ya mawe na ujenzi wa mitambo mipya ya umeme wa makaa ya mawe. Komesheni makaa ya mawe ifikapo mwaka 2030 katika nchi tajiri zaidi, na ifikapo mwaka 2040 kila mahali pengine. Hakikisheni mabadiliko ya haki kwa watu walioathirika na jamii ” amesema Katibu Mkuu.