Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Changamoto zetu haziwezi kutatuliwa kwa mtutu wa bunduki: Biden

Rais Joseph R. Biden  Jr wa Marekani akizungumza katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa UNGA76
UN Photo/Cia Pak
Rais Joseph R. Biden Jr wa Marekani akizungumza katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa UNGA76

Changamoto zetu haziwezi kutatuliwa kwa mtutu wa bunduki: Biden

Masuala ya UM

Nguvu za kijeshi za Marekani zinapaswa kuwa ni suluhu la mwisho kutumikana sio suluhu ya kwanza, amesema Rais wa Marekani Joe Biden alipowahutubia  viongozi wa dunia katika mkutano mkuu wa ngazi ya juu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa UNGA76 mjini New York Marekani. 

Katika mjadala wa wazi ulioanza rasmi hii leo Biden amesema "leo hii masuala mengi yanayotutia hofu hayawezi kutatuliwa au hata kushughulikiwa kupitia mtutu wa bunduki. ” 

Rais Biden ameongeza kuwa “Marekani inajikita na siku za usoni na badala ya kuendelea kupigana vita vya zamani, tunainua macho yetu juu na kuelekeza rasilimali zetu kwenye changamoto ambazo zina ufunguo wa mustkabali wetu.” 

Katika changamoto hizo, Biden amezitaja kuwa ni pamoja na janga la COVID-19, changamoto ya mabadiliko ya tabianchi, kusimamia mabadiliko katika nguvu za ulimwengu, kuunda sheria za kimataifa juu ya maswala muhimu kama biashara, changamoto za mtandao, teknolojia zinazoibuka na kukabiliwa na tishio la ugaidi, kama ilivyo hivi sasa.  

Katika suala la ushirikiano wa kimataifa, Rais huyo wa Marekani amesema "Ni ukweli wa kimsingi wa karne ya 21, ndani ya kila nchi zetu na kama jamii ya kimataifa kwamba mafanikio yetu yamefungwa katika mafanikio mengine pia. Ili kuwafanikishia watu wetu wenyewe lazima pia tuhusike kwa undani na dunia nzima ili kuhakikisha kuwa mustakbali wetu lazima tufaanye kazi pamoja na washirika wengine, kuelekea mustakbali wa pamoja. Usalama wetu, ustawi wetu, na uhuru wetu umeunganishwa, kwa maoni yangu haijawahi kutokea. Ninaamini lazima tufanye kazi pamoja kuliko hapo awali," amesema Biden  

Tutaendelea kujilinda 

Biden amesisitiza kuwa "Marekani itaendelea kujilinda, kulinda washirika wetu na maslahi yetu dhidi ya mashambulio, ikiwa ni pamoja na vitisho vya kigaidi. Tunapojiandaa kutumia nguvu, endapo kuna ulazima lakini ni kwa kutetea masilahi yetu muhimu ya kitaifa, pamoja na kujilinda dhidi ya vitisho. ” 

Rais huyo wa taifa lenye nguvu zaidi duniani ametaja masharti ya mustakbali wa ushirikiano kuwa ni "dhamira lazima iwe wazi na inayoweza kufanikiwa kwa idhini ya watu wa Marekani na wakati wowote inapowezekana, kwa kushirikiana na washirika wetu." 

Pia ameongeza kuwa "Tuna haki ya kujibu kikamilifu dhidi ya mashambulio ya mtandao ambayo yanatishia watu wetu, washirika wetu na maslahi yetu. Tutafuata sheria mpya za biashara ya kimataifa na ukuaji wa uchumi, kujitahidi kusawazisha mambo, ili kusiwe na kupendelea nchi yoyote moja kwa hasara ya zingine. Na kila taifa lina haki na nafasi ya kushindana kwa usawa. ” 

Kuhusu Iran, Rais wa Marekani amesema nchi yake "inaendelea kujitolea kuizuia Iran kupata silaha za nyuklia" kwa kufanya kazi na kundi la nchi  tano wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa P5 + 1 ambazo zinajumuisha (Marekani, Uingereza, Ufaransa, Shirikisho la Urusi na China pamoja na Ujerumani) "kushirikisha Iran kidiplomasia na kutafuta kurudi kwenye JCPOA. Tuko tayari kurudi kamili ikiwa Iran itafanya vivyo hivyo. ” 
 
Pamoja na Marekani kujiengua kwenye vita vya Afghanistan, ni mara ya kwanza kwa takriban miaka ishirini kwa Rais wa Marekani kusimama mbele ya Mkutano Mkuu wa Baraza Kuu ,wakati Marekani haishiriki kwenye vita yoyote amesema  Biden. 

"Tumegeuza ukurasa. Nguvu zote zisizo na kifani na kujitolea, mapenzi na rasilimali za taifa letu sasa zimeelekezwa kikamilifu na kwa usawa juu ya kile kilicho mbele yet una sio nyuma yetu. " 

Rais Biden amehitimisha hotuba yake kwa kusema "Ninajua kwamba tunapotazama mbele, tutaongoza. Tutaongoza katika changamoto zote kubwa za wakati wetu kuanzia COVID-19 hadi mabadiliko ya tabianchi, amani na usalama, utu wa binadamu na haki za binadamu, lakini hatutakwenda peke yetu. Tutaongoza kwa pamoja na wadau na washirika wetu na kwa kushirikiana na wale wote ambao wanaamini tunapofanya hivyo kuwa hii iko ndani ya uwezo wetu, ili kukabiliana na changamoto hizi. "