Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa lifanyiwe marekebisho - Rais Ruto

Rais William Samoei Ruto wa Jamhuri ya Kenya akihutubia mjadala mkuu wa kikao cha 78 cha Baraza Kuu.
UN Photo/Cia Pak
Rais William Samoei Ruto wa Jamhuri ya Kenya akihutubia mjadala mkuu wa kikao cha 78 cha Baraza Kuu.

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa lifanyiwe marekebisho - Rais Ruto

Amani na Usalama

Takwa la muda mrefu la viongozi wengi hususani kutoka Barani Afrika la Baraza la Usalama la Umoja wa lililoundwa tarehe 25 Octoba mwaka 1945 kufanyiwa marekebisho makubwa limeendelea kuchukua nafasi katika hotuba za viongozi wa ngazi za juu wanaohutubia katika mkutano wa 78 wa Baraza Kuu wa Umoja wa Mataifa jijini New York Marekani ambapo hii leo Rais wa Kenya amesema sababu zote za kulifanyia marekebisho zipo wazi. 

“Iwapo uthibitisho wowote uliwahi kuhitajika kwamba Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa halina utenda kazi nzuri, halina demokrasia, sio jumuishi, halina uwakilishi na kwa hivyo halina uwezo wa kuleta maendeleo ya maana kwenye ulimwengu wetu kama ilivyo sasa, kutokujali kwa baadhi ya watendaji duniani kunathibitisha suala hilo.” Amesema Rais William Ruto katika hotuba yake. 

Kwa dakika 23 za hotuba yake Rais Ruto amegusia masuala mbalimbali ikiwemo mabadiliko ya tabianchi, hitaji la kuwa na ushirikiano, malengo ya maendeleo endelevu na migogoro inayoendelea katika maeneo mbalimabli duniani. 

Suala la mabadiliko katika taasisi za fedha nalo amelizungumzia ambapo ametaka mageuzi katika taasisi za fedha za kimataifa, akibainisha kuwa, Kwa mujibu wa shirika la fecha duniani IMF, kufikia mwezi uliopita wa Agosti, nchi 10 za kipato cha chini zilikuwa na dhiki ya madeni, na 52 ziko katika hatari kubwa na ya wastani ya kuangukia katika dhiki.

Rais huyo ameeleza kuwa, “Jumuiya ya kimataifa lazima iandae mpango wa kurekebisha madeni ambao haungojei mataifa kutumbukia kwenye shida kabla ya kutoa ahueni.” Badala yake, usanifu mpya wa deni kuu unapaswa kupanua kiwango vya madeni na kutoa muda wa msamaha wa miaka 10 kwa nchi ambazo ziko kwenye dhiki ya madeni.

Mkuu huyo wa nchi ya Kenya pia aliangazia hali ya usalama nchini Haiti, nakusema, "Tunahimiza Umoja wa Mataifa kutoa haraka mfumo unaofaa ili kuwezesha kutumwa kwa Msaada wa Usalama wa Kimataifa kama sehemu ya jibu kamili kwa changamoto za Haiti. "

Kutazama hotuba nzima ya Rais William Ruto bofya hapa.