Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Viongozi wa dunia wanakutana UN; Ni kupima ‘mapigo ya moyo’ wa dunia

Nembo za SDG katika Ukumbi wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mnamo 2022.
UN /Manuel Elias
Nembo za SDG katika Ukumbi wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mnamo 2022.

Viongozi wa dunia wanakutana UN; Ni kupima ‘mapigo ya moyo’ wa dunia

Masuala ya UM

Wakati ule umewadia tena! Macho na masikio ya dunia kuelekezwa makao makuu ya UN jijini New York, Marekani baadaye mwezi huu wakati Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, (UNGA) litakapokaribisha marais, malkia na wafalme, mawaziri wakuu na wakuu wa nchi kutoka nchi 193 wanachama wa Umoja wa Mataifa.

Mitaa karibu na makao makuu ya UN yaliyoko mjini kati Manhattan, itafungwa, huku vizuizi vikishamiri, usalama ukiimarishwa, wakati viongozi kutoka pande mbalimbali za dunia wakikutana kupima ‘mapigo ya moyo’ ya sayari dunia wakati wa wiki ya vikao vya ngazi ya juu na kukutana pia kusaka majawabu ya changamoto za dunia. 

Mkutano wa 78 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, UNGA78 umeanza tarehe 6 Septemba na utafuatiwa na mfululizo wa mikutano muhimu na mikutano ya wakuu wa nchi wanachama, bila kusahau Mjadala Mkuu ambamo kwamo kila kiongozi wa nchi anapata fursa ya kuhutubia kuhusu masuala muhimu ya kimataifa. Yafuatayo ni mambo ya kutarajia wakati wa UNGA78:

1. Kutathmini hali ya dunia

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres (kulia)  akikutana na Balozi Dennis Francis, kutoka Trinidad na Tobago, ambaye ndiye  amechaguliwa kuwa Rais wa UNGA78
UN /Eskinder Debebe
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres (kulia) akikutana na Balozi Dennis Francis, kutoka Trinidad na Tobago, ambaye ndiye amechaguliwa kuwa Rais wa UNGA78

Rais wa UNGA 78  Dennis Francis, kutoka Trinidad na Tobago, tarehe 19 mwezi Septemba atatumia rungu lake kuanzisha rasmi Mjadala Mkuu, ambako viongozi wa dunia watajadili kusongesha kasi ya Malengo ya Maendeleo Endelevu, (SDGs) ikibeba maudhui, Kujenga upya kuaminiana na kuchochea mshikamano wa dunia.

Nchi zote wanachama wa UN pamoja na wale wenye hadhi ya utazamaji kama vile Holy See na Palestina, wana haki ya kutoa hotuba zao hadi tarehe 25 mwezi Septemba, wawakilishi wao watawasilisha majawabu ya changamoto lukuki ili kusongesha amani, usalama, na maendeleo endelevu.

 Mwenendo ulioanzishwa mwaka 1955 na UNGA10 unaendelea hadi leo, ambapo Brazil inakuwa ya kwanza kuhutubia ikifuatiwa na Marekani, kama nchi mwenyeji wa Umoja wa Mataifa na kisha wanachama wengine wanafuatia.

Fuatilia Mubashara au tembelea wavuti wa Mikutano ya UN ambako huku utapata muhtasari wa vikao kwa lugha za Kiingereza na Kifaransa, lugha mbili zinazotumika kwenye kazi za Umoja wa Mataifa.

2. Malengo ya Maendeleo Endelevu  – Mkutano wa Viongozi kuhusu SDG 

Wanafunzi katika shule moja ya msingi mashariki mwa Nigeria wakisubiri mwalimu aingie masomo yaanze.
© UNICEF/Mackenzie Knowles-Cour
Wanafunzi katika shule moja ya msingi mashariki mwa Nigeria wakisubiri mwalimu aingie masomo yaanze.

Kama kitovu cha wiki ya vikao vya ngazi ya juu vya UNGA78, Mkutano wa viongozi kuhusu SDGs utakuwa jukwaa kuu kwa viongozi wa nchi na serikali kuonesha uongozi wao wa kisiasa katika utekelezaji wa Ajenda 2030, mpango wa hatua wenye malengo 17.

Ikiwa ndio mkutano unaoanzisha wiki ya vikao vya ngazi ya juu kuanzia tarehe 18 hadi 19 Septemba, mkutano wa SDGs unalenga kuanzisha zama mpya ya kusongesha malengo hayo, ambayo kasi yake ya utekelezaji inasuasua, na mkutano huo utatamatishwa kwa kupitishwa kwa azimio la kisiasa.

Ajenda ya 2030 ni ahadi na si hakikisho. Ikiwa sasa hivi imeshapita nusu ya kipndi cha kufikia ukomo wa utekelezaji wake, (Ajenda hii ilizinduliwa 2015) utekelezaji wake uko kwenye kiza. Kasi ya utekelezaji wake inakumbwa na majanga ya tabianchi, mizozo, kudorora kwa uchumi, na madhara ya COVID-19 ambayo bado yanaonekana.

“Mkutano wa viongozi wa SDGs mwezi Septemba lazima uwe ni fursa ya umoja ya kuchechemua kasi ya kusongesha SDgs,” amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres.

Mkutano huo wa siku mbili utakuwa ni fursa ya kupaza sauti ili kuchochea kasi ya utekelezaji. Halikadhalika unalenga kutoa fursa ya mwongozo wa kisiasa, kutambua maendeleo na changamoto zinazoibuka, na pia kuhamasisha ufadhili wa fecha kuelekea ukomo wa utekelezaji mwaka 2030.

Bofya hapa kufahamu zaidi kuhusu Mkutano wa Viongozi kuhusu SDGs.

3. Haki kwa tabianchi, watekelezaji na watendaji

Mfanyakazi wa UN akipita mbele ya bango linalotoa wito kwa viongozi wa dunia kutoa ahadi jasiri za hatua kwa tabianchi.
UN /Daniel Dickinson
Mfanyakazi wa UN akipita mbele ya bango linalotoa wito kwa viongozi wa dunia kutoa ahadi jasiri za hatua kwa tabianchi.

Tarehe 20 mwezi Septemba viongozi wa dunia watajikita katika kubadili vitendo kuwa hatua kwenye Mkutano wa viongozi kuhusu tabianchi. Fursa ya kisiasa ya kutekeleza kwa vitendo hatua dhidi ya janga kubwa zaidi la tabianchi, tukio ambalo litajikita katika maeneo matatu: mipango ya kiwango cha juu, uhaliali na utekelezaji.

Hoja kuu: Ni kwa jinsi gani dunia itajiondoa kutoka uzalishaji wa mafuta kisukuku Kwenda kwenye nishati isiyochafua mazingira, nishati safi na salama.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa “kwenye orodha yake ya mambo ya kufanya anasema kuwa hatua za kina zinahitajika kutoka kwenye serikali, wafanyabiashara na viongozi wa ufadhili, kutoka kwenye Ajenda yake ya kuchochea kasi dhidi ya tabianchi kuelekea mwongozo wa hatua 5 ambazo dunia inapaswa kuchukua ili kuhamia kwenye nishati jadidifu.

“Sasa ni wakati wa kuchukua hatua za hali ya juu,” amesema Katibu Mkuu akiongeza kuwa “nasubiri kwa hamu kukaribisha wachukua hatua na watendaji katika mkutano wangu wa viongozi kuhusu Hatua kwa Tabianchi. Dunia inatazama na sayari haiwezi kusubiri.                        

 Fahamu zaidi kuhusu mkutano huo wa Hatua kwa Tabianchi hapa.

4. Kuandaa dunia iliyo tayari kusonga mbele hata baada ya majanga

Mtoto akitibiwa katika kituo cha afya  nchini Nigeria
© UNOCHA/Adedeji Ademigbuji
Mtoto akitibiwa katika kituo cha afya nchini Nigeria

Viongozi wa dunia watazingatia njia bora zaidi ya siku za usoni ya kujenga uchumi endelevu hata baada ya kukumbwa na majanga ya magonjwa, hatua za uchumi ambazo zitakuwa na afya sio tu kwa binadamu bali pia kwa sayari dunia.

Dunia salama: Rais wa UNGA na Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya ulimwenguni, (WHO) wataitisha kikao cha jinsi ya kujiandaa dhidi ya magonjwa ya milipuko, mkutano utakaohusisha viongozi wa nchi na serikali na utafanyika tarehe 20 Septemba. Viongozi hao wanatarajiwa kuhitimisha kikao cha kwa kupitisha azimio  linalolenga kuhamasisha utashi wa kisiasa katika ngazi ya kitaifa, kikanda na kimataifa. Fahamu zaidi hapa.

Afya kwa wote:Mkutano kuhusu Huduma ya Afya kwa Wote utafanyika tarehe 21 Septemba na utazingatia kile ambacho nchi zimejifunza kutokana na COVID-19 sambamba na mapendekezo yatokanayo na ushahidi kwa lengo la kuchagiza mipango ya afya kwa wote kuelekea mwaka 2030. 

Kwa kina kuhusu mkutano huo bofya hapa.

Maneno kuwa vitendo: Halikadhalika tarehe 20 Septemba, mazungumzo ya ngazi ya juu kuhusu ufadhili kwa maendeleo yatafanyika kwa lengo la kuonesha uongozi wa kisiasa na mwongozo wa utekelezaij wa Ajenda ya Addis Ababa ya mwaka 2015, ambao ni mpango wa Umoja wa Mataifa wenye lengo la kuhamasisha ufadhili wa rasilimali ili kufanikisha SDGs. Mkutano huo unatarajiwa pia kuainisha maendeleo na changamoto zilizoibuka pamoja na mbinu za kuchagiza maendeleo zaidi. Bofya hapa kufahamu zaidi.

Kukabili janga la Kifua Kikuu (TB): Mkutano wa ngazi ya juu kuhusu mbinu za kukabiliana Kifua Kikuu (TB) utafanyika tarehe 21 na lengo kuu ni kutathmini maendeleo ya utekelezaji wa azimio la kisiasa la mwaka 2018 halikadhalika SDGs. Bofya hapa kufahamu zaidi.

5. Maandalizi ya Mkutano wa Viongozi kuhusu mkutano wa Zama zijazo

Mama nchini India akimsaidia binti yake na mafunzo kwa njia ya mtandao wakati shule zilipofungwa kutokana na COVID-19.
© UNICEF/Vinay Panjwan
Mama nchini India akimsaidia binti yake na mafunzo kwa njia ya mtandao wakati shule zilipofungwa kutokana na COVID-19.

Tarehe 21 mwezi Septemba kutafanyika mkutano wa mawaziri ikiwa ni wa maandalizi kuhusu mkutano wa viongozi wa zama zijazo wa mwezi Septemba mwaka 2024.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anataka mkutano huo wa ngazi ya mawaziri ujenge maridhiano ya kimataifa tayari kwa siku zijazo zilizosheheni changamoto, hatari lakini vile vile fursa.

Mawaziri watajadili jinsi gani mfumo wa ushirikiano wa kimataifa unawza kushughulikia changamoto na hatari zinazoibuka na kuwasilisha majawabu ya kina, mapendekezo ya hali ya juu ili kuimarisha na kurekebisha mfumo wa dunia.

Mpango wa zama zijazo wenye hatua za utekelezaji unatarajiwa kupitishwa na nchi wanachama. 

Kufahamu zaidi juu ya mkutano huu wa maandalizi bofya hapa.

Unaweza kufuatilia matangazo kupitia wavuti wetu news.un.org/sw lakini vile vile pakua apu ya Habari za UN.