Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNGA78: Mkuu wa UN apuuza kutokuwepo kwa viongozi wakuu, asema lazima ahadi za maendeleo na mabadiliko ya tabianchi zitimizwe

Katibu Mkuu António Guterres (Kulia) akihojiwa na Mita Hosalia (Kushoto) Naibu Mkurugenzi wa kitengo cha Habari na Vyombo vya Habari katika idara ya mawasiliano ya Umoja wa Mataifa.
UN Photo/Mark Garten
Katibu Mkuu António Guterres (Kulia) akihojiwa na Mita Hosalia (Kushoto) Naibu Mkurugenzi wa kitengo cha Habari na Vyombo vya Habari katika idara ya mawasiliano ya Umoja wa Mataifa.

UNGA78: Mkuu wa UN apuuza kutokuwepo kwa viongozi wakuu, asema lazima ahadi za maendeleo na mabadiliko ya tabianchi zitimizwe

Masuala ya UM

Huku viongozi kadhaa wa ngazi za juu duniani wakijiondoa kwenye kuhudhuria kikao cha ufunguzi cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa wiki ijayo, Katibu Mkuu wa Umoja huo António Guterres amesema hajali ni nani anayekuja New York na kikubwa zaidi kwake ni kuhusu nini kifanyike, hasa kufufua hali inayodemadema ya utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo (SDGs).

"Haya sio maonyesho ya ubatili. Hiki ni chombo cha kisiasa ambacho serikali zinawakilishwa,” ameiambia UN News katika mahojiano maalum.

Ameongeza kuwa "Kilicho muhimu ni kwamba nchi zinawakilishwa na mtu ambaye anaweza kufikia na kwenda na wakati uliopo. Kwa hivyo sina wasiwasi sana kuhusu nani anakuja. Ninachohofia ni kuhusu kuhakikisha kuwa nchi ambazo ziko hapa ziko tayari kuwajibika kwa ahadi zinazohitajika ili kufanya Malengo ya Maendeleo Endelevu ambayo kwa bahati mbaya hayasongi katika mwelekeo sahihi kuwa ukweli."

Bwana Guterres amesisitiza haja ya kurekebisha mfumo wa sasa wa fedha "usio wa haki, usiofanya kazi na uliopitwa na wakati ili kuhakikisha mafanikio ya SDGs ifikapo 2030.”

Almekumbusha pendekezo lake la kichocheo cha SDGs cha dola bilioni 500 kusaidia mataifa yanayoendelea kuhakikisha yana rasilimali wanazohitaji ili kufikia malengo ya SDGs.

Hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi

Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amesema zaidi kwamba mkutano wake wa kilele wa Matarajio ya mabadiliko ya tabianchi 2023, utatoa fursa kwa nchi, wafanyabiashara, na mashirika ya kiraia kuongeza juhudi zao za udhibiti katika mabadiliko ya tabianchi unaokwenda kombo hivi sasa.

Katika kuondoka kwenye mazoea ambapo nchi ziko mbele na katikati ya changamoto hii, mkutano huu utatoa jukwaa kwa kile ambacho Katibu Mkuu amekitaja kama "walio msitari wa mbele” ambao wamejitolea zaidi kwa hatua za dhidi ya mabadiliko ya tabianchi, na wanaweza kushirikisha wengine uzoefu wa mazoea bora.  

Ameonya kwamba "Tunaelekea hadi kwenye nyuzi joto 2.6-2.8 ° C ya ongezeko la joto duniani ifikapo mwishoni mwa karne," 

Ameendelea kwa kusisitiza kwamba kuna udharura wa kurejea kwa lengo la kupunguza ongezeko la joto hadi nyuzi joto 1.5 ° C juu ya viwango vya kabla ya maendeleo ya viwanda.

"Bado inawezekana kwa utashi wa kisiasa  lakini mengi yanahitajika kufanywa," amesisitiza Bwana Guterres.

Kutoa msukumo wa amani nchini Ukraine

Kuhusu vita vinayoendelea nchini Ukraine, Katibu Mkuu amesema lengo kuu ni kupata amani, ambayo ni ya haki na kwa mujibu wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa na sheria za kimataifa.

Hata hivyo, ametahadharisha dhidi ya matumaini yasiyofaa, akikiri kwamba mazingira ya sasa yanaweza kutopendekeza mazungumzo ya kina kuhusu amani.

Lakini amesisitiza kuwa"Nadhani pande kinzani ziko mbali na uwezekano huo kwa sasa lakini asilani  hatutasimamisha juhudi zetu za kuhakikisha kuwa amani inakuja Ukraine," 

Kuangazia afya ya umma

Bwana Guterres pia amezungumza kuhusu mijadala mitatu ya ngazi ya mawaziri itakayofanyika wiki ijayo ambayo hayajawahi kushuhudiwa kuhusu afya ya umma duniani, kujiandaa kwa majanga, fursa ya afya kwa wote, na kifua kikuu.

Amesema "Utoaji huduma za afya kwa wote ni lengo muhimu la Umoja wa Mataifa. Hauhitaji tu mfumo wa Umoja wa Mataifa kufanya kazi, unahitaji mifumo ya kifedha kuwa ya haki zaidi kuliko ilivyo leo."

Katibu Mkuu pia alisisitiza kwamba "moja ya mambo ambayo ninaamini ni muhimu ni kuongeza rasilimali na nguvu za shirika la afya la Umoja wa Mataifa duniania.”