Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Pazia la mjadala mkuu wa UNGA78 lafungwa, umuhimu wa UN bado dhahiri

Rais wa Baraza Kuu laUN Balozi Dennis Francis akifunga mjadala mkuu wa mkutano wa 78 wa Baraza Kuu la UN tarehe 26 Septemba 2023
UN /Cia Pak
Rais wa Baraza Kuu laUN Balozi Dennis Francis akifunga mjadala mkuu wa mkutano wa 78 wa Baraza Kuu la UN tarehe 26 Septemba 2023

Pazia la mjadala mkuu wa UNGA78 lafungwa, umuhimu wa UN bado dhahiri

Masuala ya UM

Mjadala Mkuu wa mkutano wa 78 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ulioanza tarehe 19 mwezi huu wa Septemba umekunja jamvi letu Jumanne tarehe 26 Septemba ambapo viongozi wa dunia wameeleza kuwa ingawa Umoja wa Mataifa unakabiliwa na changamoto za kitaasisi, bado unasalia kuwa jukwaa kuu la kuumba majawabu shida zinazomkabili binadamu hivi sasa.

Kwa wiki nzima iliyopita, marais, wakuu wa serikali na wawakilishi wa Baraza hilo Kuu linaloundwa na nchi zote 193 wanachama  walieleza bayana changamoto mbalimbali, kuanzia janga litokanalo na mabadiliko ya tabianchi hadi matumizi yasiyo sahihi ya Akili Mnemba, au AI.

Katika hotuba yake ya kufunga mjadala huo mkuu, Rais wa Baraza Kuu Balozi Dennis Francis ameelezea umuhimu wa uwepo wa Baraza Kuu na ahadi isiyoteterekaya Umoja wa Mataifa ya kusongesha amani, ustawi, maendeleo na uendelevu wa watu duniani kote.

“Maendeleo haya ni mambo yanayotumbusha kuwa Umoja wa Mataifa unasalia kujikita katika changamoto za pamoja zinazotukumba zama hizi,” amesema Balozi Francis.

Akimulika mizozo na vita vinavyoendelea hivi sasa, Balozi Francis amesema yuko tayari kusaidia uwezeshaji mazungumzo ya usuluhishi wa amani na urafiki kati ya nchi na makundi yaliyo kwenye mizozo, akisisitiza kuwa “kuweni na uhakika kuwa niko hapa kuwahudumia.”

Idadi ya viongozi walijitokeza lakini wanawake wachache

Takwimu za awali zinaonesha kuwa wiki ya ngazi ya juu imeshuhudia mkusanyiko mkubwa zaidi wa viongozi walioshiriki vikaoni kwenye makao makuu ya UN, New York, tangu janga la COVID19 mwaka 2020 lililosababisha vikao kufanyika kwa mtandao au mtandaoni na mjengoni.

Wakuu wa nchi 88 wameshiriki, Wakuu 42 wa serikali na zaidi ya mawaziri 650.

Ingawa hivyo idadi ya viongozi wanawake ilipungua kutoka 23 mwaka jana hadi 20 mwaka huu ambapo Balozi Francis amesema, “wakati wa wiki ya vikao vya ngazi ya juu niliweza kuitisha jukwaa la viongozi wanawake, nikifuata nyayo za watangulizi wangu. Nimezungumza na viongozi wengi kuhusu umuhimu wa kutambua kuwa sauti za wanawake, matarajio na haki zao zina umuhimu mkubwa kila ngazi, kuanzisha mashinani hadi jukwaa la kimataifa. Na hii inaanzia na kuwekeza kwenye elimu, hasa kwa wasichana.”

Maafisa wa ngazi ya juu walitumia uwepo wa viongozi hao kushiriki katika zaidi ya mikutano 2,000 ya nchi na nchi.

Halikadhalika, wajumbe kutoka nchi wanachama walikuwa zaidi ya 13,000, waandishi wa habari 2,600 na washiriki zaidi ya 40,000 walijisajili kushiriki mjadala mkuu pamoja na matukio mengine 100 ya kando.

Miongoni mwa matukio hayo ya kando ni Hatua kwa SDG lililofanyika mwishoni mwa wiki tarehe 16 na 17 Septemba, lililoleta pamoja mashirika ya kiraia, wafanyabiashara, vijana, wanasayansi, viongozi wa serikali za mitaa na wadau wengine ili kufanikisha ajenda 230 ya malengo ya maendeleo endelevu, SDG ambayo ilipitishwa na nchi wanchama mwaka 2015.

Tumeazimia kufanikisha SDGs

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa MAtaifa, Amina Mohmmed amesema wakati wa wiki hiyo ya ngazi ya juu, ilikuwa dhahiri kuwa washiriki wameazimia kufanikisha Ajenda 2030, hasa wakati huu ambapo nusu ya kwanza imemalizika na imesalia nusu ya pili kufikia 2030.

Akitoa tathmini ya wiki hiyo amezungumzia pia jinsi washiriki wamesisitiza umuhimu wa rasilimali, akitaja pia mzigo wa madeni uliogubika nchi nyingi, ukizizuia kupeleka fedha za kutosha kwenye huduma muhimu kama vile afya na elimu.

Amewaambia waandishi wa habari kuwa “hatuna rasilimali za kutosha na ndio maana tunataka kuweko kwa fungu maalum la kuchochea usongeshaji wa SDGs. Hicho ni kitu cha kupata kwa urahisi. Hicho ni kitu tunaweza kukipata kwa kutumia rasilimali zilizoko na taasisi. Na ninatumaini kuwa ifikapo mwisho wa mwaka huu, tutakuwa na kitu cha kuzungumzia.”

Amegusia pia Bi. Mohammed kuwa ahadi za kutia moyo pia zilipitishwa kwenye mkutano wa viongozi kuhusu tabianchi.