Je wajua mapana na marefu ya rungu la kuongozea mikutano ya UNGA?

20 Septemba 2019

 Rungu la rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, UNGA, linalotumiwa kuongozea mikutano lilitolewa kama zawadi ya Iceland kwa Umoja wa Mataifa.

RUNGU LINATOKA ICELAND

Demokrasia ya taifa la Iceland inaaminiwa kuwa ndiyo kongwe zaidi kuliko ya mataifa mengine duniani. 
 
Bunge la nchi hiyo, Althing, lilifanya kikao cha kwanza mwaka 930, na hivyo linachakuliwa kama, “babu” wa mabunge ya zama za sasa.
 
Kutokana na urithi wa kidemokrasia, watu wa Iceland waliamua kuwa yeyote anaongoza vikao vya “bunge la dunia” yaani Umoja wa Mataifa ni lazima awe ‘amejihami’ na nyundo ya Iceland.

Vyumba vingi vya mikutano katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, kila kimoja, kina rungu dogo la mbao. Lakini lile linalotumiwa katika ukumbi wa Baraza Kuu ambako mataifa 193 wanachama wa Umoja huo hukutana na kuzungumzia  masuala mbalimbali ya dunia ni tofauti. Ni kubwa, lenye madoido na lenye rangi ya kahawia.
 
Rungu la rais ni sehemu ya vikao vya Baraza Kuu kwa kuwa hutumika kuashiria mwanzo na mwisho wa kikao; kukubaliwa kwa ajenda; kuchaguliwa kwa maafisa na kuidhinishwa kwa maazimio.Pia wakati fulani hutumiwa kunyamazisha wajumbe.

RUNGU LA THOR 

Rungu hilo lilitumiwa katika Baraza Kuu kwa kipindi cha miaka minane. Mwakilishi wa kudumu wa zamani wa Iceland katika Umoja wa Mataifa, Hjálmar W. Hannesson, anagusia historia ya rungu la rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa akisema kuwa,  “Mwaka 1952, wakati  jengo la makao makuu ya Umoja wa Mataifa lilipofunguliwa kando mwa mto wa Mashariki, mjini New York, Mwakilishi wa kwanza wa Iceland katika Umoja wa Mataifa,Bw. Tor Thors, alimzawadia rais wa Baraza Kuu rungu la kungozea mikutano. Na kutokana na hilo lilipatiwa jina la “rungu la Thor”.

RUNGU LAVUNJIKA 

Rungu lilifanya kazi kwa kipindi cha miaka nane.  Bwana Hannesson anaeleza sababu akisema kuwa “mwezi wa Oktoba mwaka wa 1960, rungu letu liligonga vichwa vya habari duniani kote kwani lilivunjika…aliyelivunja alikuwa rais wa baraza hilo kwa wakati huo, raia kutoka Ireland,Frederick Boland.”
 
Anaendelea kusema kuwa “Balozi Boland alikuwa anataka kumnyamazisha  kiongozi wa Urusi ya wakati huo, Nikita Kruschchev, hususan alikuwa anamzuia  kukoma kugonga meza akitumia kiatu chake.  Kulikuwa na kelele nyingi katika ukumbi na Boland alitaka kurekebisha mambo alipogonga meza na rungu hilo ndivyo likavunjika.”
 
Kwa mujibu taarifa za vyombo vya habari, baada ya tukio hilo, wajumbe wengi, wakiwa na mshikamano na balozi Boland, walimtumia marungu kadhaa ya kujaza pengo la rungu lililovunjika ili achague moja.
 
Hata hivyo, Umoja wa Mataifa uliamua kuiomba Iceland kuleta rungu kama lile lililovunjika.
 
Tofauti na la mwanzo, balozi  Hannesson anasema,  rungu lililoletwa liliweza kuhimili kugongwa gonjwa kwenye meza na kuhimili kwa karibu nusu karne na kuendelea. 

UN /Loey Felipe
Rais wa mkutano wa 73 wa Baraza Kuu la UN Maria Espinosa (kulia) akimkabidhi Rais wa mkutano 74 wa Baraza Kuu Balozi Tijjani Muhammad-Bande (kushoto) rungu la kuongozea kikao. Anayetazama kwa mbali ni Katibu Mkuu Antonio Guterres.

 

“Huo haukuwa mwisho wa visanga vya  rungu hilo. Mwaka wa 2005, rungu hilo lilipotea na afisa mmoja wa Umoja wa Mataifa alituarifu na  bila kusita tukajibu kuwa Iceland italeta rungu lingine.  Mara hii aliyechonga rungu hili ni mmoja wa mastadi wa kuchonga kwa jina la Sigridur Kristiandottir.”

JE WAJUA MTI ULIOCHONGWA KUPATA RUNGU LA SASA

Serikali ilimuomba mchongaji  mahiri atumie kifaa kigumu ndipo akatumia mbao za mti wa mpeasi.
 
Je lilikuwa sawa? Ingawa hadi sasa ni mwaka wa 2018, hebu na tusubiri tuone.
.
Balozi Hannesson anaeleza kuwa katika rungu hilo kuna maneno ambayo yako katika lugha za Iceland na kilatini na maneno yenyewe yanahusu matukio ya Iceland yaliyotokea katika karne ya 10.
Balozi anasema, ‘wakati huo tulikubali ukristo ambao ulichangia kukomesha machafuko mengi ya ndani na kuliunganisha taifa. Na mmoja wa kiongozi wakati huo akasema, “jamii ni lazima ijengwe kwa misingi ya sheria.”Na fungu hilo la maneno ndio liko katika rungu hiyo."

Kimuundo, “rungu la Thor” halionekani kama chombo cha amani, na kumfanya mtu afikirie wakati wa ghasia wa enzi za maharamia. Lakini kama historia inavyoonyesha  hata katika bunge  la dunia, katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, mara kwa mara, kunahitajika aina fulani ya nguvu za wakati wa maharamia wa kiskandinavia ili kuwatuliza viongozi.
 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud