Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Rais mpya wa Baraza Kuu Balozi Dennis Francis kutanguliza ‘Amani, Ustawi, Maendeleo na Uendelevu’ 

Balozi Dennis Francis kutoka Jamhuri ya Trinidad na Tobago kuwa Rais wa kikao cha 78 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
UN Photo/Loey Felipe
Balozi Dennis Francis kutoka Jamhuri ya Trinidad na Tobago kuwa Rais wa kikao cha 78 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

Rais mpya wa Baraza Kuu Balozi Dennis Francis kutanguliza ‘Amani, Ustawi, Maendeleo na Uendelevu’ 

Masuala ya UM

Nchi Wanachama wa Umoja wa Mataifa leo (1 Juni) wamemchagua Balozi Dennis Francis kutoka Jamhuri ya Trinidad na Tobago kuwa Rais wa kikao cha 78 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa. 

Balozi Dennis Francis ambaye mi Mwakilishi wa kudumu wa Trinidad na Tobago katika Umoja wa Mataifa, amechaguliwa kwa shangwe na Baraza Kuu ambalo linajumuisha Nchi zote 193 Wanachama wa Umoja wa Mataifa ambazo zina kura sawa.  

Baada ya kuchaguliwa, Balozi Fransisko amesema kuwa “utekelezaji wa sera zinazounga mkono na kuhimiza kuwekeza kwa watu na kwa hiyo, katika uundaji wa mitaji ya kijamii, katika muda wa kati na mrefu, bila shaka ni miongoni mwa mikakati madhubuti ya kukuza na kufikia maendeleo endelevu.” 

"Ni elimu iliyonileta mahali hapa, na hatimaye kwenye jukwaa hili, na ninajivunia na kufurahishwa na kuzaliwa katika nchi ya Trinidad na Tobago, ambayo kwa karibu miaka 70 imeweka thamani ya juu zaidi kwa elimu," Rais mteule ameongeza. 

Akihutubia Nchi Wanachama, Balozi Francis amesema, "Ni matumaini yangu kwa usaidizi na uungaji mkono wenu kuleta hali mpya ya upatanisho, ushirikiano na kujitolea kwa pamoja katika kushughulikia changamoto nyingi na kuchukua kila fursa, hata kama ni changa, mbele ya Baraza Kuu. 

Rais Mteule pia amesema kwamba "atatafuta kuimarisha mbinu za sasa na kupitisha mpya na suluhu zinazowezekana tunapojaribu kutoa, au angalau kuimarisha, msingi wa kuleta amani, ustawi, maendeleo na uendelevu." 

Rais wa Baraza Kuu huchaguliwa kwa mujibu wa kanuni ya mzunguko kati ya makundi matano ya kikanda. Kikao kijacho kilikuwa kikiongozwa na mwakilishi kutoka Kundi la Mataifa ya Amerika Kusini na Karibea lakini kundi hilo liliamua kutoweka mngombea mwingine sipokuwa huyu mmoja kutoka Trinidad and Tobago. 

Balozi Dennis Francis amekuwa katika uga huu wa Diplomasia kwa takriban miaka 40 kwa ajili ya nchi yake ya Trinidad na Tobago. 

Kwa miaka kumi na minane kati ya hiyo, alishika wadhifa wa Ubalozi hadi alipostaafu kwa mjibu wa sheria kutoka katika utumishi mwaka 2016, na kumpa tuzo ya kuwa Balozi aliyekaa muda mrefu zaidi nchini mwake. 

Rais anayemaliza muda wake 

Rais wa sasa wa Baraza Kuu, Csaba Kőrösi wa Hungaria, amebainisha kuwa mrithi wake analeta utajiri wa maarifa na uzoefu kwenye wadhifa huo. 

"Dira ya Bwana Francis kwa ajili ya kikao cha 78 - 'Amani, Ustawi, Maendeleo na Uendelevu' - inatoa mtazamo wa kina wa kazi ya Baraza Kuu tunapojenga upya imani ndani ya taasisi hii, kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kujitahidi kurejesha SDGs kwenye mstari.” Amesema Csaba Kőrösi. 

Huku siku 100 zikiwa zimesalia katika utawala wake, Bwana Kőrösi amesema ataendelea kuhimiza matumizi ya sayansi kwa mageuzi endelevu katika maandalizi ya Mkutano wa SDG wakati wa Wiki ya Ngazi ya Juu ya Baraza Kuu mwezi Septemba. 

Katibu Mkuu António Guterres akihutubia nchi wanachama wakati wa hafla ya Balozi Dennis Francis wa Trinidad na Tobago kuchaguliwa kwa shangwe kuwa Rais wa kikao cha 78 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
UN Photo/Loey Felipe
Katibu Mkuu António Guterres akihutubia nchi wanachama wakati wa hafla ya Balozi Dennis Francis wa Trinidad na Tobago kuchaguliwa kwa shangwe kuwa Rais wa kikao cha 78 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

Katibu Mkuu UN 

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres ameongeza kuwa uongozi wa Bwana Francis unakuja katika "wakati wenye changamoto kubwa", huku kukiwa na migogoro, machafuko ya tabianchi, na kuongezeka kwa umaskini, njaa na ukosefu wa usawa - wakati SDGs pia "zinateleza nje ya kufikiwa". 

Guterres amesema Rais anayekuja pia analeta mtazamo muhimu kwani masuala mengi yaliyoshughulikiwa katika Baraza Kuu - kama vile mabadiliko ya tabianchi na mfumo usio wa haki wa kifedha duniani - yanaathiri zaidi visiwa vidogo vinavyoendelea kama Trinidad na Tobago. 

"Tunatazamia kwa Rais Mteule kuendeleza kauli mbiu ya urais wake Amani, Ustawi, Maendeleo na Uendelevu - katika mwaka ujao, na kuleta pamoja Baraza ili kuimarisha ushirikiano wa kimataifa katika wakati huu mgumu," amesema Guterres.