Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Afrika ni ufunguo wa ulimwengu ujao - Rais Tinubu

Rais wa Nigeria Bola Ahmed Tinubu wakati akihutubia katika mjadala Mkuu wa Mkutano wa 78 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
UN Photo/Laura Jarriel
Rais wa Nigeria Bola Ahmed Tinubu wakati akihutubia katika mjadala Mkuu wa Mkutano wa 78 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

Afrika ni ufunguo wa ulimwengu ujao - Rais Tinubu

Masuala ya UM

“Afrika sio tatizo la kuepukwa na wala sio lakuonewa huruma. Afrika ni ufunguo wa ulimwengu ujao.” Ni kauli iliyotolewa na Rais wa Nigeria Bola Ahmed Tinubu wakati akihutubia katika mjadala Mkuu wa Mkutano wa 78 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa au UNGA78 jijini New York Marekani.

Katika hotuba yake Rais Tinubu amesema Afrika inatafuta ushirikiano wa kimataifa ili kutekeleza malengo ya maendeleo endelevu SDGs ifikapo mwaka 2030 na kwamba changamoto nyingi zinazo likabili bara hilo zimetokana na sababu ndani ya bara hilo pamoja na nje. 

 “Kutokuwepo na utawala bora kumeikwamisha Afrika, lakini ahadi zisizotimizwa, kutotendewa haki na unyonyaji wa moja kwa moja kutoka nje pia kumesababisha madhaara makubwa katika uwezo wetu wa kuendelea.” 

Mambo makuu 5

Rais huyo wa Nigeria ambaye pia ni mwenyekiti wa umuiya ya Uchumi ya nchi za Afrika Magharibi, ECOWAS ametaja mambo makuu watano katika hotuba yake. 

Mosi, Mashirika ya kimataifa, nchi nyingine na sekta binafsi lazima zichukulie maendeleo ya Afrika kama kipaumbele sio tu kwa afrika bali kwao pia. 

Pili, lazima kuhakikishwe kuna utawala wa kidemokrasia na kupinga mapinduzi ya kijeshi. 

Kuhusu Niger, tunajadiliana na viongozi wa kijeshi. Kama Mwenyekiti wa ECOWAS, ninajaribu kusaidia kusimamisha tena utawala wa kidemokrasia kwa njia ambayo inashughulikia changamoto za kisiasa na kiuchumi zinazokabili taifa hilo, ikiwa ni pamoja na watu wenye msimamo mkali wanaotaka kuzua ukosefu wa utulivu katika eneo letu.”

Tatu, Misimamo mikali, imesababisha watu kushiriki katika biashara haramu za kuuza binadamu wenzao na kuwasafirisha kiharamu. Ameeleza pia kuhusu safari za hatari zinazofanywa na waafrika kupitia ukanda wa Sahel kwenda kusaka maisha bora barani Ulaya na kwamba nchi hizo zinajitahidi kuboresha uchumi ili watu wasiendelee kutumbukia kwenye safari hizo za hatari na kugharimu maisha yao. 

Nne, uaminifu na mshikamano wa kimataifa katika kulinda maeneo yenye utajiri wa madini ya barani Afrika ambayo kwa sasa yamegubikwa na wizi na vita. “Maeneo mengi kama hayo yamekuwa makaburi ya taabu na unyonyaji.”

Tano, Mabadiliko ya tabianchi nchi za Afrika zinapambana na athari za mabadiliko ya tabianchi na zitaendelea kufanya hivyo kwa masharti yao wenyewe. 

Kutazama hotuba nzima ya Rais Tinubu bonyeza hapa.