Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN yataka kukomeshwa haraka mauaji ya wale wanaokimbia El Geneina Sudan

Wakimbizi wa Sudan wakielekea nchi jirani.
© WFP/Jacques David
Wakimbizi wa Sudan wakielekea nchi jirani.

UN yataka kukomeshwa haraka mauaji ya wale wanaokimbia El Geneina Sudan

Amani na Usalama

Msemaji wa ofisi ya Haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa amesema kuwa mahojiano yaliyofanywa na wale waliokimbia kutoka El Geneina, jimbo la Darfur Magharibi nchini Sudan, hadi Adre nchini Chad, yamefichua ukweli wa kutisha kuhusu wanamgambo wa Kiaarabu, wanaoungwa mkono na vikosi vya msaada wa Haraka wa kuwaua wale wanaokimbia jiji  hilo kwa miguu.

Msemaji huyo Ravina Shamdasani ameongeza kuwa wafanyakazi wa ofisi ya haki za binadamu OHCHR wamesikia shuhuda nyingi zilizothibitishwa za wanamgambo wa Kiaarabu wakiwalenga hasa wanaume watu wazima kutoka jamii ya Masalit.

Bi. Shamdasani, amendelea kusema kwamba “wote waliohojiwa pia wamezungumzia kuona maiti zimetapakaa kando ya barabara na harufu kali ya uvundo wa kuoza miili ya watu".

Idadi ya watu waliripoti kuona makumi ya maiti ni katika eneo linalojulikana kama Shukri, takriban kilomita 10 kutoka mpakani, ambapo wanamgambo mmoja au zaidi wa Kiarabu wanaripotiwa kuwa na kambi.

Msemaji huyo ameelezea wasiwasi wake mkubwa kuhusu mauaji haya ya kutisha na akataka hatua za haraka zichukuliwe ili kuyakomesha. 

Na amesisitiza haja “ya kutoa njia salama kwa wale wanaokimbia El Geneina, na kuruhusu mashirika ya kibinadamu kufikia eneo hilo ili kukusanya mabaki ya wafu.”

Mkimbizi mjane mwenye miaka 25 kutoka Sudan aliyekimbia machafuko Darfur akiwa na watoto wake kwenye makazi ya wakimbizi ya Goungour nchini Chad
© UNHCR/Aristophane Ngargoune
Mkimbizi mjane mwenye miaka 25 kutoka Sudan aliyekimbia machafuko Darfur akiwa na watoto wake kwenye makazi ya wakimbizi ya Goungour nchini Chad

Ushuhuda wa mauaji ya kutisha

Kati ya watu 16 ambao ofisi ya Haki za binadamu imekutana nao hadi sasa huko Adre Chad, 14 kati yao wamesema walishuhudia mauaji ya kiholela yaani bila kufuata utaratibu na kulengwa kwa vikundi vya raia kwenye barabara kati ya El Geneina na mpakani ama kwa risasi kutoka umbali mfupi na watu waliamuriwa kulala chini au kwa kufyatua risasi kwenye umati.

Mashuhuda walizungumzia mauaji yaliyotokea Juni 15 na 16, pamoja na wiki iliyopita. "Tunachoelewa ni kwamba mauaji na aina nyingine za unyanyasaji zinaendelea na kuambatana na kauli za chuki zinazoendelea dhidi ya jamii ya Masalit, ikiwa ni pamoja na wito wa kuuawa na kufukuzwa kutoka Sudan," amesema msemaji huyo.

Mwanamume mwenye umri wa miaka 37 alisema alikuwa miongoni mwa kundi la watu 30 wanaojaribu kukimbilia mpaka wa Chad, lakini ni 17 pekee waliofanikiwa kuvuka mpaka.

Mtu huyo alisema kuwa watu wengine kadhaa, waliokuwa pamoja naye, waliuawa baada ya kupigwa risasi kutoka kwenye magari ya wanajeshi wa Rapid Support Forces RSF na wanamgambo wa Kiarabu karibu na mpaka wa Chad, huku wengine wakiuawa kwa mauaji ya kiholela.

Ameongeza kuwa walionusurika waliibiwa pesa na simu zao na watu wenye silaha ambao walikuwa wakiimba "Ninyi ni watumwa, ninyi ni Wanubi."

IOM ni miongoni mwa mashirika yanayosaidia wakimbizi wa ndani waliotawanjwa El Geneina kwenye jimbo la Darfur Magharibi nchini Sudan
© IOM/Muse Mohammed
IOM ni miongoni mwa mashirika yanayosaidia wakimbizi wa ndani waliotawanjwa El Geneina kwenye jimbo la Darfur Magharibi nchini Sudan

Watu walazimika kuwaacha wenzao bila msaada

Kulingana na taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na msemaji wa ofisi ya Haki za binadamu, mwanamke mwenye umri wa miaka 22 alizungumzia matukio kama hayo ya uhasama.

Alisema kundi lake lililazimika kumwacha kijana aliyejeruhiwa vibaya njiani kwa sababu hakukua na njia ambayo wangeweza kumbeba hadi mahali salama kuvuka mpaka.

Aliongeza kuwa, "Ilitubidi kumwacha, kwani tulikuwa na punda mmoja tu." Taarifa hiyo iliashiria ugumu wa kukadiria idadi ya majeruhi walioachwa kufa katika mazingira kama hayo.

 Watu wawili waliohojiwa tofauti walisema walishuhudia RSF ikiwaamuru wao na kundi lingine la watu kuondoka El Geneina. 

Mmoja wao alisema kuwa alipigwa kwa fimbo huku akiambiwa, "Inuka uende Chad, hii si nchi yako."

RSF kemeeni na kukomesha mauaji

Kamishna Mkuu wa Haki za binadamu ametoa wito kwa uongozi wa RSF kulaani mara moja na bila shaka kukomesha mauaji ya wale wanaokimbia El Geneina na vitendo vingine vya unyanyasaji na kauli za chuki dhidi yao kwa misingi ya ukabila.

Msemaji wa Kamishna mkuu amesisitiza haja ya kuwawajibisha waliohusika na mauaji na ghasia hizo. 

Amesema “El Geneina imekuwa sehemu isiyoweza kukaliwa na watu”. Akieleza kuwa miundombinu imeharibiwa, huku misaada ya kibinadamu ikiendelea kuzuiwa.

Ofisi ya haki za binadamu imehimiza kuanzishwa mara moja kwa ukanda wa kibinadamu kati ya El Geneina na Chad, na njia salama kwa raia wanaotaka kutoka nje ya maeneo yaliyoathiriwa na uhasama.