Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watu kati ya 10,000 na 20,000 wamefungasha virago Sudan na kuingia Chad kukimbia mapigano: UNHCR

Wakimbizi wa Sudan wakiwasili nchini Chad mwanzoni wa mwaka 2023 kufuatia mlipuko wa ghasia katika jimbo la Darfur, Sudan. (Maktaba)
© UNHCR/Suzette Fleur Ngontoog
Wakimbizi wa Sudan wakiwasili nchini Chad mwanzoni wa mwaka 2023 kufuatia mlipuko wa ghasia katika jimbo la Darfur, Sudan. (Maktaba)

Watu kati ya 10,000 na 20,000 wamefungasha virago Sudan na kuingia Chad kukimbia mapigano: UNHCR

Amani na Usalama

Kufuatia mapigano yanayoendelea Khartoum nchini Sudan, tangu Jumamosi Aprili 15, kati yavikosi vya msaada wa haraka (RSF) vinavyoongozwa na Jenerali Mohammed Hamdane Daglo na jeshi la kitaifa linaloongozwa na Jenerali Abdel Fattah al-Burhane, maelfu ya wakimbizi wa Sudan wamewasili katika nchi jirani ya Chad tangu mwishoni mwa wiki kwa mujibu wa taarifa ya  shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR iliyotolewa usiku wa kuamkia leo.

Mashirika ya Umoja wa Mataifa yanaripoti kwamba "Makadirio ya wakimbizi wapya ambao wamewasili Mashariki mwa Chad katika siku mbili zilizopita ni kati ya 10,000 hadi 20,000", ameandika kupitia ukurasa wake wa Twitter Laura Lo Castro, mwakilishi wa Shirika la UNHCR nchini Chad.

Ujumbe wa pamoja wa UNHCR, Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF na  shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani WFP uliweza "Kushuhudia wimbi la wakimbizi wapya wa Sudan wanaokimbia mapigano nchini mwao katika maeneo matatu ya kwanza ambayo ulitembelea siku ya Jumanne” amesema Bi Castro.

Mwanzoni wa mwaka 2023, wakimbizi wa Sudan walitafuta usalama. (Maktaba) katika nchi jirani ya Chad kufuatia kuzuka kwa ghasia katika jimbo la Darfur.
© UNHCR/Suzette Fleur Ngontoog
Mwanzoni wa mwaka 2023, wakimbizi wa Sudan walitafuta usalama. (Maktaba) katika nchi jirani ya Chad kufuatia kuzuka kwa ghasia katika jimbo la Darfur.

Kuelekea utekelezaji wa mpango wa hatua kwa wakimbizi

Lengo la ujumbe huu wa sasa wa Umoja wa Mataifa katika eneo hili la Mashariki mwa Chad ni “kutathmini mahitaji ya dharura na kukubaliana juu ya mpango wa wa dharura wa kuchukua hatua na uwezekano wa kuingia kwa wimbi kubwa la wakimbizi wa Sudan.”

Katika taarifa yake iliyotolewa jana Jumanne UNHCR hapo awali ilidokeza kwamba "Haifahamu kuhusu harakati zozote za wakimbizi kwenda nchi jirani". Hata hivyo, timu za kamishna mkuu Filippo Grandi zimeonyesha azimio lao la "kuitikia na kutoa msaada kwa Sudan na nchi za eneo hilo ikiwa ni lazima".

Katika taarifa hiyo hiyo, UNHCR imeeleza wasiwasi wake mkubwa kuhusu usalama wa raia katika maeneo yaliyoathiriwa na mapigano, yakiwemo ya wakimbizi na wakimbizi wa ndani.

"Kuongezeka huku kwa ghasia kunaweza tu kuzuia hatua za msaada wa kibinadamu kwa watu wanaohitaji nchini kote na kuhatarisha utulivu na harakati za kutafuta suluhu kwa mamilioni ya watu waliolazimika kukimbia katika eneo hilo", lilisema shirika la Umoja wa Mataifa la wakimbizi likibainisha kuwa kudhibiti hali hiyo ni dharura inayohitajika haraka.

Moshi ukiongezeka kufuatia shambulio la bomu katika kitongoji cha Al-Tayif mjini Khartoum, Sudan.
Open Source
Moshi ukiongezeka kufuatia shambulio la bomu katika kitongoji cha Al-Tayif mjini Khartoum, Sudan.

Hospitali 16 zikiwemo 9 za Khartoum hazitumiki

UNHCR inasema Chad ni nyumbani kwa zaidi ya wakimbizi 600,000, wakiwemo karibu 400,000 kutoka Sudan.

Na kati ya wakimbizi hawa 600,000, baadhi yao 145,000 karibu asilimia 24 wamewasili Chad tangu mwaka 2018, na makundi mapya yanaendelea kuwasili kila mwaka, hasa kutoka Sudan lakini pia kutoka Jamhuri ya Afrika ya Kati CAR na Nigeria.

Kwa upande wake, Shirika la Umoja wa Mataifa la afya duniani WHO limetoa tahadhari kuhusu kuzorota kwa hali ya afya nchini humo tangu mapigano na vikosi vya usaidizi wa haraka yalipozuka siku ya Jumamosi. Kutokana na mashambulizi hayo, hospitali 16 zikiwemo 9 za Khartoum sasa hazina huduma kabisa.

"Hospitali 16 za Khartoum na majimbo mengine, ikiwa ni pamoja na majimbo ya Darfur, pia ziko katika hatihati ya kutofanya kazi kutokana na uchovu wa wafanyikazi na ukosefu wa vifaa," amesema jana jioni Dkt. Ahmed Al-Mandhari, mkurugenzi wa Kanda ya Mediterania Mashariki wa WHO.

WHO inalaani vikali mashambulizi yanayoripotiwa dhidi ya wafanyakazi wa afya, vituo vya afya na magari ya kubebea wagonjwa nchini Sudan.

Mashambulizi haya ambayo yanaonekana kuongezeka, tayari yamesababisha vifo vya wahudumu watatu na wawili kujeruhiwa.

Pia yanapunguza fursa za ufikiaji wa huduma muhimu za afya, na kuweka maisha mengine ya watu hatarini.

Mama akiwa na binti yake mwenye umri wa miezi 9 akipata msaada kutoka kwa diwani katika Jimbo la Kassala, Sudan.
© UNICEF/Mojtba Moawia Moawi
Mama akiwa na binti yake mwenye umri wa miezi 9 akipata msaada kutoka kwa diwani katika Jimbo la Kassala, Sudan.

Mashambulizi ya kijeshi dhidi ya vituo vya afya

"Ripoti za mashambulizi ya kijeshi dhidi ya vituo vya afya, utekaji nyara wa magari ya kubeba wagonjwa yaliyokuwa na wagonjwa na wahudumu wa afya kwenye ndege, uporaji wa vituo vya afya na uvamizi wa vituo vya afya unaofanywa na vikosi vya jeshi ni jambo la kutia wasiwasi sana," amesema Dkt. Al-Mandhari akikumbusha kwamba mashambulizi dhidi ya huduma za afya. ni ukiukwaji wa wazi wa sheria za kimataifa na haki ya afya.

Kwa WHO, “pande zinazohusika katika mzozo huo lazima zihakikishe kwamba wagonjwa, wafanyakazi wa afya na magari ya kubebea wagonjwa wanaweza kufika hospitalini kwa usalama na wakati wote.”

Wagonjwa lazima wapate huduma za afya sio tu kutibu majeraha yao, lakini pia kwa huduma zingine muhimu na za kuokoa maisha.

Dk Al-Mandhari alihitimisha tarifa yake kwa kusema "Kadiri changamoto za upatikanaji wa huduma za afya zinavyoongezeka na wafanyikazi wa afya wanakabiliwa na rasilimali chache za kutibu wagonjwa. Usalama na utoaji wa huduma ya afya lazima ulindwe kila wakati, haswa katika hali za migogoro ambapo ufikiaji wa huduma muhimu unakuwa muhimu zaidi,".