Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

OHCHR: Makaburi ya watu wengi yagunduliwa nchini Sudan

Shule ya Al-Imam Al-Kadhim kwenye mji wa Al-Geneina jimbo la Darfur Magharibi nchini Sudan, ambayo imekuwa hifadhi kwa wakimbizi wa ndani iliteketezwa kwa moto wakati huu ambapo mapigano yanaendelea nchini Sudan.
© Mohamed Khalil
Shule ya Al-Imam Al-Kadhim kwenye mji wa Al-Geneina jimbo la Darfur Magharibi nchini Sudan, ambayo imekuwa hifadhi kwa wakimbizi wa ndani iliteketezwa kwa moto wakati huu ambapo mapigano yanaendelea nchini Sudan.

OHCHR: Makaburi ya watu wengi yagunduliwa nchini Sudan

Haki za binadamu

Miili ya takriban watu 87 ya kabila la Masalit na wengine wanaodaiwa kuuawa mwezi uliopita na vikosi vya msaada wa haraka RSF na washirika wao huko Darfur Magharibi nchini Sudan, imezikwa kwenye kaburi la pamoja huko El-Geneina kwa amri ya vikosi hivyo kulingana na taarifa za kuaminika ambazo Ofisi ya Haki za Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa imezipata. 

Taarifa ya ofisi hiyo kutoka Geneva Uswisi imesema miili mingine 50 ilizikwa katika eneo moja tarehe 21 Juni. Miili ya wanawake saba na watoto saba ilikuwa miongoni mwa waliozikwa kwenye kaburi la pamoja.

Kamishna Mkuu wa Haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa OHCHR Volker Türk amesema “Ninalaani kwa nguvu zote mauaji ya raia na ninashangazwa zaidi na jinsi wafu, pamoja na familia na jamii zao, walivyotendewa.”

Duru za habari zimesema takriban miili ya watu 37 ilizikwa tarehe 20 Juni, 2023 katika kaburi la pamoja lenye kina cha mita moja katika eneo la wazi linaloitwa Al-Turab Al Ahmar (Udongo Mwekundu), katika eneo la polisi kufanyia mazoezi ya kurusha risasi, ambalo liko takriban kilomita mbili hadi nne kutoka kaskazini-magharibi mwa makao makuu ya polisi wa hifadhi ya Kati magharibi mwa El-Geneina.

Türk amesema lazima kuwe na uwajibikaji “Lazima kuwe na uchunguzi wa haraka, wa kina na huru kuhusu mauaji hayo, na wale waliohusika lazima wawajibishwe."

Watu wa eneo hilo walilazimishwa kutupa miili hiyo katika kaburi la pamoja, na kuwanyima haki marehemu ya kuzikwa kwa heshima katika moja ya maeneo rasmi ya makaburi ya jiji hilo. 

Kamishna huyo wa OHCHR amekitaka kukosi cha RSF na pande zote kwenye mzozo huo kuruhusu na kuwezesha utafutaji wa haraka wa watu waliofariki, kuwakusanya na kuwahamisha bila ubaguzi, ikiwa ni pamoja na kuruhusu mambo hayo kufanyika kwa misingi ya kikabila, na kueleza hilo ni suala ambalo wanapaswa kuliruhusu kwa kuzingatia sheria ya kimataifa.

Walichokiona mashuhuda

Walioshuhudia hali hiyo wameeleza kuwa juhudi za upatanishi wa eneo hilo za kutaka kupata ruhusa ya kwenda kuwazika marehemu zimechukua muda mrefu, na kuacha miili mingi ikiwa mitaani kwa siku nyingi.

Familia moja ilisema ilibidi kusubiri siku 13 kabla ya kuruhusiwa kuchukua mwili wa mwanafamilia, ambaye ni mtu mashuhuri wa Masalit aliyeuawa mnamo au karibu 9 Juni na wanamgambo wa RSF.

Mashahidi waliiambia Ofisi ya Haki za Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa kwamba katika matukio ambapo RSF imeruhusu kukusanywa kwa wafu - kufuatia upatanishi kati ya viongozi wa Kiarabu na jumuiya nyingine - wamekataa kuruhusu majeruhi kuondolewa hospitalini kwa matibabu.

"Uongozi wa RSF na wanamgambo washirika wao pamoja na pande zote kwenye mzozo wa kivita wanatakiwa kuhakikisha kuwa wafu wanashughulikiwa ipasavyo, na utu wao unalindwa," Türk alisema.

Wanaopigana vita lazima wazingatie sheria za kimataifa 

Ofisi ya haki za binadamu imeikumbusha RSF kuwa lazima warekodi, au kuruhusu wafanyakazi wa kutoa misaada ya kibinadamu kurekodi, taarifa zote zilizopo kuhusiana na wafu, ikiwa ni pamoja na kuchukua picha sahihi za miili na kuweka alama eneo la makaburi, kwa nia ya utambuzi ili kuwezesha kurejeshwa kwa mabaki ya marehemu kwa familia.

Chini ya sheria ya kimataifa ya kibinadamu na sheria ya kimataifa ya haki za binadamu, pande zote kwenye mzozo lazima zihakikishe waliojeruhiwa wanapata matibabu.

Kamishna Mkuu alitoa wito kwa uongozi wa RSF mara moja na bila shaka kulaani na kukomesha mauaji ya watu, na kukomesha vurugu na matamshi ya chuki dhidi ya watu kwa misingi ya kikabila.