Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ghasia West Darfur Sudan zimewaathiri maelfu-OCHA

18 Machi 2014. Saraf Omra: Kikundi cha wanawake katika makazi mapya ya watu waliohamishwa karibu na makao ya UNAMID Saraf Omra, North Darfur.
UNAMID/Albert González Farran
18 Machi 2014. Saraf Omra: Kikundi cha wanawake katika makazi mapya ya watu waliohamishwa karibu na makao ya UNAMID Saraf Omra, North Darfur.

Ghasia West Darfur Sudan zimewaathiri maelfu-OCHA

Amani na Usalama

Ghasia kati ya jamii ndani na nje ya El Geneina, mji mkuu wa jimbo la West Darfur nchini Sudan yanaripotiwa kusababisha vifo vya takriban watu 54, kuwajeruhi 60  na kusababisha 40,000 kuhama makwao tangu Desemba 28.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa hii leo na Jens Laerke, msemaji wa shirika la Umoja wa Kimataifa la kuratibu huduma za kibinadamu OCHA, mjini Geniva Uswisi, watu  32,000 ya waliohama ni wale ambao tayari walikuwa ni wakimbizi wa ndani.

Bwana Laerke amesema kuwa maelfu ya watu wamevuka mpaka na kuingia Chad na kutafuta hifadhi katika vijiji karibu na mpaka na Sudan.

“Waliohama makwao katika jimbo la West Darfur wamepata hifadhi katika shule kadhaa na majengo ya serikali kwenye mji wa El Geneina.” Amesema Laerke.

Umoja wa Mataifa na washirika wanaunga mkono jitihada za serikali na za shirika la msalaba mwekundu la Sudan.

Hali katika eneo lililoathiriwa kwa sasa imetulia na kuwa thabiti huku mashirika ya Umoja wa Mataifa yakiwa yanasambaza maji, sabuni na kusaidia katika ukusanyaji taka kutoka maeneo yanayowapa watu hifadhi.

Misaada mingine ni pamoja usambazaji wa chakula na msaada wa lishe kwa watoto na pia usambazaji wa vyandarua vya mbu, blanketi na matandiko.