Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watu wapya zaidi ya 222,000 watawanywa na machafuko Kivu Kaskazini pekee: UN

Wakimbizi wa ndani katika kambi ya Loda iliyoko Fataki jimboni Ituri nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC
© UNICEF/Roger LeMoyne
Wakimbizi wa ndani katika kambi ya Loda iliyoko Fataki jimboni Ituri nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC

Watu wapya zaidi ya 222,000 watawanywa na machafuko Kivu Kaskazini pekee: UN

Amani na Usalama

Mashirika na misaada ya kibinadamu ya Umoja wa Mataifa yamesema machafuko na ukosefu wa usalama vinavyoendelea kwa miezi kadhaa sasa Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC kwenye majimbo ya Ituri na Kivu ya Kaskazini yamewaweka mamilioni ya watu katika ukingo wa janga kubwa la kibinadamu.

Akizungumza na waandishi wa habari hii leo mjini New York Marekani msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric amesema katika jimbo la Kivu Kaskazini pekee mapigano yanayoendelea baina ya kundi la M23 na jeshi la serikali ya Congo FARDC, yametawanya watu wapya zaidi ya 222,000 na idadi hiyo ni kwa mwezi wa Januari na Februari mwaka huu pekee na hivyo kufanya jumla ya wanaume, wanawake na watoto waliotawanywa tangu kuzuka kwa machafuko Machi mwaka jana kufikia zaidi ya watu 880,000.

Umoja wa Mataifa umesema zaidi ya nusu ya watu hawa wanaishi katika mazingira magumu kwenye miji ya Nyira-gongo na Goma na viunga vyake. 

Wakimbizi wa ndani milioni 6.1

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa miongoni mwa wakimbizi wa ndani milioni 6.1 nchini DRC, asilimia 65 kati yao wako Ituri na Kivu Kaskazini.

Stephane amesema “Kwa mujibu wa wenzetu DRC machafuko yanasambaa nchini humo hadi katika sehemu ambazo zimekuwa na utulivu kwa miaka iliyopita. Maeneo hayo ni Pamoja na majimbo ya Magharibi ya Mai-Ndome na Kwilu, ambayo yamechochewa na machafuko ya kijamii yangu mwezi Juni mwaka jana.”

Ameongeza kuwa na kutokana na matokeo ya machafuko hayo hali ya kutokuwa na uhakika wa chakula inaongezeka katika nchi ambayo tayari ni maskani ya watu zaidi ya milioni 26.4 ambao wanahaha kila uchao kupata chakula cha kutosha.

Pia wagonjwa wa utapiamlo na magonjwa mengine kama surau na kipindupindu wanaongezeka na kuongeza shinikizo kwa uwezo wa jumuiya ya misaada ya kibinadamu kuweza kukidhi mahitaji ya kukabiliana na changamoto hizo.

Msemaji hiyo wa Umoja wa Mataifa amesisitiza kuwa “Sisi Pamoja na washirika wetu tunafanya kila juhudi kusaidia lakini mahitaji yanayoongezeka kwa kasi yanazidi uwezo wetu wa kuyakabili na kuna haja ya haraka ya mashirika yote ya kibinadamu kuongeza jitihada katika maeneo ambako mahitaji ni ya muhimu nay a haraka zaidi hususani Mashariki mwa nchi.”

Hadi sasa Umoja wa Mataifa unasema ombi la dola bilioni 2.25 kwa ajili ya DRC limefadhiliwa kwa asilimia 10 pekee hivyo fedha zinahitajika haraka.