Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNHCR yaomba msaada zaidi kuwasaidia wakimbizi wa ndani DRC

Sabuni zinaandaliwa kusambazwa na UNHCR kwenye maghala yaliyoko Mashiriki mwa Jamuhuri ya Kidemokrasia Congo.
© UNHCR/Michelle Ehouman
Sabuni zinaandaliwa kusambazwa na UNHCR kwenye maghala yaliyoko Mashiriki mwa Jamuhuri ya Kidemokrasia Congo.

UNHCR yaomba msaada zaidi kuwasaidia wakimbizi wa ndani DRC

Msaada wa Kibinadamu

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR limeomba msaada wa haraka wa fedha kwa wahisani ili kuweza kuendelea na shughuli zake nchini Jamhuri ya kidemokrasia Congo, DRC. 

Akizungumza na waandishi wa habari akiwa Geneva Uswisi, msemaji wa UNHCR Boris Cheshirkov amesema mpaka sasa imepokea asilimia 51 ya dola milioni 205 wanahitaji kwa mwaka huu, ili waweze kuendelea na shughuli zao za kuwasaidia wananchi wa nchi hiyo ambao kila uchao wanaendelea kuteseka, kufa, na kufanyiwa vitendo kinyume na haki za binadamu. 

Amesema UNHCR inaendelea kutiwa hofu na mashambulizi dhidi ya raia yanayofanywa na vikundi vya wanamgambo Mashariki mwa nchi hiyo ambapo shirika hilo na wadau wengine wamerekodi vifo vingi. 

“Mpaka sasa zaidi ya raia 1,200 wamekufa, na kwa mwaka huu pekee watu 1,100 wamebakwa katika majimbo mawili yaliyoathirika zaidi ya Kivu kaskazini na Ituri. UNHCR pia tumerekodi vitendo vya kinyume na haki za binadamu zaidi ya 25,000 kwa mwaka huu.”
Cheshirkov amesema kwa ujumla zaidi ya wananchi wa DRC milioni moja wameyakimbia makazi yao katika ukanda wa mashariki mwa nchi hiyo. 

Watoto walioyakimbia makazi yao kutokana na vita wakicheza nje ya shule huko Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia Congo
© UNHCR/Justin Kasereka
Watoto walioyakimbia makazi yao kutokana na vita wakicheza nje ya shule huko Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia Congo

 Wanaowapokea wakimbizi wa ndani wamechoka

Amesema watu wanao yakimbia makazi yao wamekuwa wakipokelewa vyema katika maeneo wanayokimbilia lakini, hali ilivyo sasa wenyeji wanaonesha kuhemewa na kuhitaji msaada ili waweze kuendelea kuwasaidia. 

“Ugumu wa maisha na ukosefu wa chakula mara nyingi unasababisha makundi ya wakimbizi wa ndani kurejea katika makazi yao ya asili hali inayozidisha kuwaweka katika hatari, unyanyasaji na vurugu. Watu hawa wanaorejea makwao wamerekodiwa wakiathirika kwa zaidi ya asilimia 65 na uvunjifu wa haki za binadamu kwa mujibu wa UNHCR na washirika wake”, amesema msemaji huyo wa UNHCR.

Akitolea mfano wa vitendo hivyo viovu Cheshirkov amesema “Tarehe 06 Septemba 2021, kundi la wanamgambo liliripotiwa kuwabaka wanawake 10 katika eneo la Djugu jimboni Ituri. UNHCR na wadau wake waliwapeleka wanwake hao katika hospitali ya karibu ambapo walipatiwa matibabu na ushauri wa kisaikolojia.”

UNHCR imerejea wito wake wa kuchukuliwa hatua za haraka za kulinda raia. Pia wameomba vyombo vya usalama nchini humo pamoja na vikundi vya kijamii ambao wamekuwa wakiwasaidia watu wnaoyakimbia makazi yao mara kwa mara kuendelea kuokoa maisha, kuendelea kuwapa usaidizi wa kisaikolojia na misaada mingine watu wanaohitaji.