Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu
Watoto wakiwa kwenye kituo chao cha kucheza ambacho ni salama. Kituo kimeanzishwa na UNICEF.

Mtoto asimulia alivyoona rafiki yake akiuawa na waasi DRC

© UNICEF/Sibylle Desjardins
Watoto wakiwa kwenye kituo chao cha kucheza ambacho ni salama. Kituo kimeanzishwa na UNICEF.

Mtoto asimulia alivyoona rafiki yake akiuawa na waasi DRC

Amani na Usalama

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF Catherine Russell ametoa wito wa azimio la haraka la kisiasa ili kukomesha ghasia zinazoendelea Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC.

Russell ametoa wito huo baada ya kumaliza ziara yake jimboni Ituri, eneo ambalo limekumbwa na mashambulizi dhidi ya raia.

UNICEF imeonya kuhusu hali mbaya katika kambi ya Rhoe. Ghasia ambazo zimesababisha watu wengi kuhama katika eneo hilo zimeendelea kwa muda wa wiki mbili zilizopita na hazioneshi dalili ya kupungua. 

“Maelfu ya watoto na familia wamekwama kwenye mlima wenye ulinzi mdogo sana na upatikanaji hafifu wa makazi na huduma muhimu kama vile maji salama, usafi wa mazingira, elimu, afya na lishe," alisema Russell na kuongeza kuwa “Tayari tumeona milipuko ya magonjwa ya kupumua, kuhara na malaria. Juhudi zote zinapaswa kufanywa ili kuimarisha utoaji wa huduma kwa watu wanaoishi katika kambi ya Rhoe na kuwalinda dhidi ya vurugu.”

Kambi hiyo, iliyoko kilometa 45 kaskazini mashariki mwa mji mkuu wa jimbo la Bunia, hadi hivi karibuni ilikuwa ikifikiwa na mashirika ya misaada kwa helikopta kwa sababu ya ukosefu wa usalama na mashambulizi dhidi ya wafanyakazi wa mashirika ya kibinadamu. Eneo linalozunguka kambi hiyo linaendelea kushambuliwa na makundi mengi yenye silaha.

 Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF Catherine Russell akitangamana na mwanafunzi katika darasa la muda lililojengwa katika kambi ya Rhoe mashariki mwa DRC.
© UNICEF/UN0621005/ Josue Mulala
Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF Catherine Russell akitangamana na mwanafunzi katika darasa la muda lililojengwa katika kambi ya Rhoe mashariki mwa DRC.

Mtoto aeleza alivyo shuhudia mauaji ya rafiki yake wa karibu

Wakati akiwa ziarani Ituri, Russell alisafiri hadi Rhoe, eneo la kambi ambayo sasa inakadiriwa kuwa watu 63,000, kut yao watoto wakiwa ni 36,000, ambao wamekimbia makazi yao kwa sababu ya migogoro na vurugu.

Wengi wa wakimbizi wa ndani katika kambi hiyo waliwasili Novemba 2021 baada ya kufukuzwa kutoka kambi tofauti ya wakimbizi wa ndani katika mji wa karibu wa Drodro ambayo ilishambuliwa na watu waliokuwa na mapanga. Tukio hilo lilikuwa moja ya matukio ya hivi karibuni ya ghasia ambayo yameikumba DRC Mashariki kwa miongo kadhaa na kusababisha takriban watu milioni tano kuyakimbia makazi yao.

Mkuu huyo wa UNICEF alizungumza na watoto na familia zilizoathiriwa na vurugu hizo, akiwemo Blukwa - mvulana mwenye umri wa miaka 14 ambaye aliponea chupuchupu kuuawa huko Drodro, lakini alishuhudia mauaji ya kikatili ya rafiki yake kipenzi katika shambulio hilo.

“Blukwa aliniambia baada ya kushuhudia mauaji ya rafiki yake kipenzi, alitaka kufa pia,” amesema Russell. "Hakuna mtoto anayepaswa kupata msiba na hofu kama hiyo. Katika miongo miwili iliyopita, watoto wengi mashariki mwa DRC wameteseka vibaya kutokana na migogoro na mashambulizi ya mara kwa mara dhidi ya raia. Wanahitaji suluhu la dharura la kisiasa kwa mgogoro huu ili waweze kuishi kwa amani.”

Wakati wa shambulio la Drodro, Blukwa na watoto wengine walitenganishwa na familia zao katikati ya machafuko. Blukwa na karibu watoto wengine 60 tangu wakati huo wameunganishwa na familia zao kupitia kazi ya AJEDEC – Asasi ya kiraia ya Kongo inayofadhiliwa na UNICEF.

Wanafunzi hushiriki katika shughuli ya kuongeza ufahamu kuhusu ujenzi wa amani, kwa msaada kutoka kwa mpango wa Kujifunza kwa Amani wa UNICEF.
© UNICEF
Wanafunzi hushiriki katika shughuli ya kuongeza ufahamu kuhusu ujenzi wa amani, kwa msaada kutoka kwa mpango wa Kujifunza kwa Amani wa UNICEF.

Misaada ya UNICEF kwa watoto walioko kambini DRC

UNICEF kwa kushirikiana na washirika wake wanaendelea kupanua wigo wa kazi zao za kusaidia watoto na familia zako katika kambi ya Rhoe, ikiwa ni pamoja na usambazaji wa hivi majuzi wa vifaa zaidi ya 5,000 vinavyojumuisha blanketi, ndoo, vyombo vya jikoni na sabuni. 

UNICEF pia inafanya kazi na washirika wengine kutoa elimu na usaidizi wa kisaikolojia kwa watoto katika kambi hiyo.
Mpango wa elimu wa UNICEF katika kambi hiyo umewanufaisha watoto 1,200 walio yakimbia makazi yao na wenyeji wa shule za msingi za jumuiya. Mpango huo unachukua wanafunzi kutoka shule tano ambazo zililazimika kuachwa kwa sababu ya kuwepo na wakimbizi wengi.

Watoto wengi wanahudhuria darasani katika mahema kadhaa makubwa yaliyo karibu na shule ya jumuiya ya mwenyeji ambayo inaangalia kambi.