Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNHCR imeomba dola milioni 137 kusaidia waliokimbia makazi yao Pembe ya Afrika

Mamama na watoto wake 10 wamehamia kwenye kambi ya wakimbizi Kenya mwaka 2022 baada ya ukame kusambaratisha mazao na mifugo yake Somalia
© UNHCR/Charity Nzomo
Mamama na watoto wake 10 wamehamia kwenye kambi ya wakimbizi Kenya mwaka 2022 baada ya ukame kusambaratisha mazao na mifugo yake Somalia

UNHCR imeomba dola milioni 137 kusaidia waliokimbia makazi yao Pembe ya Afrika

Msaada wa Kibinadamu

Ukanda wa Pembe ya Afrika ukiingia msimu wa sita bila mvua, ukimbizi wa ndani unazidi kushamiri kwa kuwa mamilioni ya watu kutoka Somalia, Ethiopia na Kenya wanaendela kuhaha katikati ya uhaba wa maji, njaa, ukosefu wa usalama na mizozo, amesema Olga Sarrado, msemaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR akizungumza na waandishi wa habari hii leo huko Geneva, Uswisi. 

Kwa sasa UNHCR inapanga kuwapatia wakimbizi wapya wa ndani na wanaovuka mpaka kutoka nchi hizo tatu, misaada ya kimsingi ikiwemo makazi ya dharura na fedha taslimu. 

Sarrado ameongeza kuwa “Katika nchi hizo tatu zaidi ya watu milioni 8 wanahitaji msaada wa chakula na takribani watu 332,000 wanahitaji msaada huo wa chakula haraka la sivyo Maisha yao yako hatarini.”

Afisa huyo wa UNHCR ameendelea kusema kuwa “watu 8 kati ya 10 waliokimbia makazi yao ni wanawake na watoto,” huku shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji, IOM, likionya kwamba kushindwa kwa misimu ya mvua na migogoro nchini Somalia, "kunaweza kulazimisha makumi ya maelfu ya watu kutafuta hifadhi katika miji mikubwa na miji, hasa Baidoa na Mogadishu ambako IOM inakadiria kwamba takriban watu 300,000 wanaweza kuwa wakimbizi wapya ifikapo Julai 2023”.

Kuhusu ombi hilo la dola milioni 137 ili kudumisha mipango muhimu ya program za misaada ya kibinadamu mwaka huu, Bi. Sarrado amesema zaidi ya wakimbizi na wakimbizi wa ndani milioni tatu tayari wamelazimika kuyahama makazi yao Somalia, Ethiopia na Kenya.

Maelfu ya wanyama wameangamia kutokana na ukame uliokithiri unaoikumba Somalia na maeneo mengine ya Pembe ya Afrika.
IOM
Maelfu ya wanyama wameangamia kutokana na ukame uliokithiri unaoikumba Somalia na maeneo mengine ya Pembe ya Afrika.

Kupambana kuweza kuishi

Kwa mujibu wa shirika hilo la Umoja wa Mataifa la wakimbizi kuishi ni mapambano kwa jamii hizi zilizolazimika kuhama makwao, huku kukiwa na uhaba wa vyanzo vya maji, njaa, ukosefu wa usalama na migogoro.

Wakimbizi hao wanahitaji usalama na usaidizi, kama ilivyo kwa jumuiya zinazowakaribisha zinavyofanya pia.

"Wakati baa la njaa hadi sasa limeepukwa nchini Somalia, zaidi kutokana na kuongezeka kwa hatia za misaada ya kibinadamu, watu wanaendelea kupambana na uhaba wa chakula na maji unaotishia maisha kunaotokana na hasara kubwa ya mavuno, mifugo, na mapato," Bi. Sarrado ameelezea.

Kupanda kwa gharama ya bidhaa

Msemaji wa UNHCR ameonya hata hivyo kwamba bei za vyakula muhimu na bidhaa nyingine zinasalia katika kiwango cha juu kabisa, nje ya uweze wa wengi kumudu.

Mchanganyiko hatari wa mabadiliko ya tabianchi na migogoro katika eneo hilo unazidisha hali ya kibinadamu ambayo tayari ni mbayá kuwa mbayá zaidi.

Nchini Somalia pekee, tangu kuanza kwa mwaka huu wa 2023, watu 288,000 wamekuwa wakimbizi wa ndani, kwa sababu ya migogoro na ukame, kwa mujibu wa takwimu za UNHCR.

Zaidi ya wakimbizi 180,000 kutoka Somalia na Sudan Kusini pia wamevuka mpaka katika maeneo yaliyoathiriwa na ukame ya Kenya na Ethiopia, limesema shirika hilo.

Katika jimbo la Somalia nchini Ethiopia ambalo tayari linakabiliwa na ukame  karibu watu 100,000 wamewasili Doolo katika wiki za hivi karibuni, baada ya kukimbia vita katika eneo la Laascaanood nchini Somalia.

Sahara, mumewe na watoto watatu wa kiume, walikimbia ukame nchini Somalia ili kuokoa mbuzi wao wachache waliobaki. Waliwasili katika kambi za wakimbizi za Dadaab nchini Kenya mwezi Oktoba.
© UNHCR/Charity Nzomo
Sahara, mumewe na watoto watatu wa kiume, walikimbia ukame nchini Somalia ili kuokoa mbuzi wao wachache waliobaki. Waliwasili katika kambi za wakimbizi za Dadaab nchini Kenya mwezi Oktoba.

Ushuhuda wa kukata tamaa

Katika kambi za Dadaab nchini Kenya, UNHCR pia imeliripoti ushuhuda wa mwanamke mwenye umri wa miaka 60 kutoka Somalia ambaye alisema alivumilia miongo mitatu ya vita kusini mwa Somalia, lakini njaa kali ndiyo iliyomlazimu kukimbia kuokoa maisha yake.

"Wengi wa waliokimbia makazi yao huenda wasirudi tena katika maeneo yao ya asili kwa sababu ardhi haiwezi kutoa tena chochote, na ukosefu wa usalama utaongezeka tu kadiri ushindani wa rasilimali ambazo tayari ni adimu unavyoongezeka," limesema shirika la IOM katika tahadhari yake kuhusu rekodi kubwa ya watu milioni 3.8 ambao sasa wamelazimika kukimbia makazi yao nchini Somalia.

"Matokeo yake, familia nzima itazaliwa na kukulia katika makazi yasiyo rasmi huku kukiwa na hali mbaya ya maisha."

Hatua za kibinadamu

Kama sehemu ya hatua zake za kibinadamu UNHCR inapanga kutoa msaada zaidi wa msingi ikiwa ni pamoja na malazi ya dharura na vifaa vya nyumbani kwa wakimbizi wapya wanaowasili na waliokimbia makazi yao nchini Somalia, Ethiopia na Kenya.

Pia shirika hilo limesema usambazaji wa malori ya maji utaongezwa, wakati visima vya ziada vitachimbwa na mifumo iliyopo ya maji na mifereji ya maji taka itafanyiwa ukarabati.

Usaidizi wa fedha utapewa kipaumbele kwa walio hatarini zaidi ili kuwasaidia kujiongezea mahitaji ya chakula, huku pia likiwahimiza wafanyabiashara kutoa chakula na mahitaji mengine.

Vituo vya afya pia vitasaidiwa kuongeza msaada wa lishe kwa wanawake na watoto kupitia ulishaji wenye virutubisho vingi na matibabu kwa magonjwa yanayohusiana na ukosefu wa lishe.

"Msaada huu wa ziada na ulinzi unahitajika haraka ili kuokoa mamilioni ya maisha," amesema Bi. Sarrado ambaye amebainisha kuwa ombi la mwaka jana ilipata chini ya nusu ya kiasi kinachohitajika kukabiliana na ukame.