Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baa la njaa lanyemelea Afrika Mashariki ukitabiriwa ukame kwa mwaka wa tano mfululizo:UN

Ukame unaathiri mamilioni ya watu Kenya, Ethiopia na Somalia
© FAO/Patrick Meinhardt
Ukame unaathiri mamilioni ya watu Kenya, Ethiopia na Somalia

Baa la njaa lanyemelea Afrika Mashariki ukitabiriwa ukame kwa mwaka wa tano mfululizo:UN

Tabianchi na mazingira

Mashirika sita ya Umoja wa Mataifa na wadau wengine wa kibinadamu leo wametoa tahadhari ya baa la njaa kunyemelea Afrika Mashariki baada ya miaka minne ya ukame mkali huku ikitabiriwa uhaba wa mvua kwa mwaka mwingine wa tano mfululizo. 

Taarifa hiyo ya pamoja iliyotolewa mjini Nairobi Kenya na mashirika ya Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani WFP, la chakula na kilimo FAO, la kuhudumia Watoto UNICEF, la kuhudumia wakimbizi UNHCR, la utabiri wa hali ya hewa WMO na la kuratibu masuala ya kibinadamu na misaada ya dharira OCHA na washirika wengine kama UKaid imesema ukame uliokithiri na unaoendelea ukiathiri misimu mingi ya mvua Somalia, Kenya, na maeneo ya wafugaji ya mashariki na Kusini mwa Ethiopia haujawahi kutokea. 

Misimu minne ya mvua mfululizo imeshindwa, halii hi ya mabadiliko ya tabianchi  halijaonekana katika maeneo hayo kwa takribani miaka 40.  

Hali huenda ikawa mbaya zaidi 

Mabadiliko ya tabianchi na hali mbaya ya hewa vinachochea mamilioni ya watu kutawanywa na ongezeko la mahitaji ya kibinadamu Pembe ya Afrika
© UNFPA Ethiopia/Paula Seijo
Mabadiliko ya tabianchi na hali mbaya ya hewa vinachochea mamilioni ya watu kutawanywa na ongezeko la mahitaji ya kibinadamu Pembe ya Afrika

Kwa mujibu wa taarifa hiyo utabiri wa msimu wa mvua ukiungwa mkono na makubaliano ya kina kutoka kwa wataalamu wa hali ya hewa, unaonyesha kuwa sasa kuna hatari kubwa kwamba msimu wa mvua wa Oktoba-Desemba mwaka huu (OND) unaweza pia kushindwa. 

Taarifa hiyo imeonya kwamba iwapo utabiri huu utatokea, hali ya dharura ya kibinadamu ambayo tayari ni mbaya katika eneo hilo itakuwa mbaya zaidi. 

Msimu wa mvua wa Machi-Mei wa mwaka huu 2022 unaonekana kuwa ndio ukame zaidi kuwahi kurekodiwa, na kuathiri vibaya hali mbaya ya maisha na kusababisha ongezeko kubwa la kutokuwa na uhakika wa chakula, maji na uhaba wa lishe. 

Mifugo milioni 3.6 imeshakufa hadi sasa ambapo milioni 1.5 nchini Kenya na milioni 2.1 nchini Ethiopia. 

Nako nchini Somalia katika maeneo yaliyoathirika zaidi na ukame shirika la FEWS NET/FSNAU linakadiria kuwa kwa upande wa mifugo kila 1 kati ya 3 amekufa tangu katikati yam waka 2021. 

Wati zaidi ya milioni moja wametawanywa 

Mabadiliko ya tabianchi yanaweza kusababisha hasara ya mabilioni ya dola katika uchumi na kukatili maelfu ya maisha ya watu kila mwaka
© Unsplash
Mabadiliko ya tabianchi yanaweza kusababisha hasara ya mabilioni ya dola katika uchumi na kukatili maelfu ya maisha ya watu kila mwaka

Taarifa hiyo ya pamoja imesema kuwa zaidi ya watu milioni moja wamekimbia makazi yao Somalia na kusini mwa Ethiopia.  

Upungufu wa maji uliopo umechochewa na hali mbaya ya joto la juu sana ambalo linatabiriwa kuendelea hadi msimu wa kiangazi wa Juni-Septemba. 

Hali katika maeneo ya malisho inatarajiwa itazorota haraka kuliko kawaida, na kusababisha vifo vingi vya mifugo, na pia kuhama kwa idadi ya watu. 

Taarifa imeendelea kusema katika maeneo ya kilimo, mavuno yatakuwa chini ya wastani, na hivyo kusababisha utegemezi mkubwa wa watu kununua chakukla sokoni kwa muda mrefu, ambapo kaya nyingi zitashindwa kukidhi mahitaji ya chakula kutokana na bei ya juu ya chakula. 

Watu milioni 16.7 wana uhaba wa chakula 

Kituo cha kusambaza maji maeneo yaliyo na ukame Somalia.
© IOM Somalia 2022/ Ismail Osma
Kituo cha kusambaza maji maeneo yaliyo na ukame Somalia.

Kikosi kazi cha uhakika wa chakula na lishe (FSNWG) kinakadiria kuwa watu milioni 16.7 kwa sasa wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula katikia kiwango cha IPC daraja la 3+ na takwimu zinakadiriwa idadi hiyo itaongezeka hadi watu milioni 20 kufikia Septemba mwaka huu. 

Nchini Somalia, tathimini iliyofanywa mwezi Aprili 2022 ilibaini hatari ya njaa viwango vya IPC daraja la 5 na ilionyesha kuwa zaidi ya watu 80,000 walikuwa wakikabiliwa na njaa kali, dalili ya baa la njaa viwango vya IPC daraja la 5. 

Taarifa hiyo inasema nchini Kenya na Somalia, karibu watu milioni 2.5 wanakabiliwa na hali ya dharura ya viwango vya IPC daraja la 4. Na dharura na janga linalohusishwa na ongezeko la vifo. 

Ethiopia, Somalia na Kenya pia zimerekodi idadi kubwa zaidi ya watoto wenye utapiamlo waliolazwa kwa matibabu katika robo ya kwanza ya mwaka 2022 ikilinganishwa na miaka iliyopita. 

Mbali na ukame, ukosefu wa uhakika wa chakula na utapiamlo uliokithiri umechangiwa na majanga mengine yanayotokea wakati mmoja, ikiwa ni pamoja na migogoro, ukosefu wa usalama, kupanda kwa bei ya mafuta duniani, chakula na mbolea kutokana na mzozo wa Ukraine, changamoto za uchumi na janga la COVID-19

Familia za Turkana zinatumia kilimo cha umwagiliaji kulima mazao ya chakula wakati wa ukame wa muda mrefu nchini Kenya.
UNDP/Ngele Ali
Familia za Turkana zinatumia kilimo cha umwagiliaji kulima mazao ya chakula wakati wa ukame wa muda mrefu nchini Kenya.

Hatua za haraka zinahitajika 

Kwa mujibu wa taarifa msimu wa mvua za chini ya wastani uliotabiriwa utasababisha kuzorota kwa hali mbaya ya uhakika wa chakula na utapiamlo katika mwaka wa 2023.  

Hata hivyo, bila kujali mvua kati ya Oktoba na Desemba, hali hazitarejea haraka vya kutosha kuona uboreshaji wa uhakika wa chakula kabla ya katikati ya 2023. 

Taarifa imesisitiza kuwa hatua za haraka zinahitajika sasa ili kuokoa maisha na kuepusha baa la njaa na vifo.  

Hata hivyo, maombi ya sasa ya msaada wa kukabiliana na ukame taarifa inasema bado hazijafadhiliwa vya kutosha. 

Hatua za kukabiliana na ukame zinahitaji kuongezwa mara moja ili kuzuia dharura ya chakula ambayo tayari ni mbaya, kuwa janga zaidi ikiwa ni pamoja na hatari ya baa la njaa nchini Somalia, kutoka hali mbaya kuwa janga kubwa.