Kujiadhari kabla ya shari ndio dawa mujarabu ya majanga: FAO
Kuchukua tahadhari za mapema katika nchi zinazotabiriwa kukumbwa na majanga ya asili kunaweza kuzuia tishio la kutokea zahma ya kibinadamu au kunaweza kudhibiti athari kwa mujibu wa ripoti mpya iliyotolewa leo na shirika la chakula na kilimo duniani , FAO.
Kwa mujibu wa shirika hilo ushahidi umedhihirisha kwamba tahadhari na hatua za mapema zilisaidia kupunguza athari za ukame wa mwaka 2017 ulioikumba Kenya, Somalia na Ethiopia.
Ushahidi mpya kuwa uingiliaji wa mapema ulipunguza athari za ukame wa mwaka 2017 katika eneo la pembe ya Afrika uko katika ripoti mpya.
Ripoti hiyo iliyotolewa leo mjini Roma Italia inasema kila dola moja iliyotumiwa na FAO kusaidia mifugo mapema nchini Kenya, Somalia na Ethiopia mapema mwaka 2017 wakati wafugaji wakijiandaa na msimu mwingine mbaya wa ukame, kila familia ilipata faida ya hadi dola 9 kwa sababu mifugo waliokufa kutokana na njaa, ukame, au magonjwa walikua wachache na uzalishaji wa maziwa ulipanda mara tatu zaidi.
Mkurugenzi wa kitengo cha dharura na mipango ya ukarabati wa FAO, Dominique Burgeon, amesema kuwekeza katika mikakati ya mapema katika kukabili majanga sio tu ni kitendo cha kiutu na cha kutumia akili bali pia kinapunguza gharama. Ameongeza kuweza kulinda maisha ya watu kabla janga halijatokea ina maanisha ni kujenga mnepo kwa siku za usoni na kupunguza shinikizo katika masuala ya rasilimali.
Amesisitiza kuwa kuchukua hatua mapema ni muhimu na inawezekana na pia ni suala la uwajibikaji, kwanu ushahidi unaonyesha kwamba “ jinsi tunavyochukua hatua mapema ndivyo uwezo wa jamii kukabili majanga unavyokuwa mkubwa..”
Mathalani ripoti imetolea mfano wa Kenya ikisema kwa wastani wanyama wengine wawili kwa kila mkulima aliyepata msaada waliweza kuokolewa ikilinganishwa na wale ambao hawakupata msaada; kila mtoto aliyekuwa chini ya umri wa miaka mitano aliweza kunywa nusu lita ya maziwa kwa siku jambo ambalo ni sawa na robo ya virutubisho wanavyostahili kuvipata kwa siku na kuwapa watoto asilimia 65 ya protini wanazohitaji kwa siku.
FAO inasema mpango huo wa kuzisadia jamii kabla ya kutokea majanga ya asili ni wa umuhimu sana kwani huokoa masiha ya watu na mifugo yao na pia ni uwekezaji muhimu kwa maisha yao ya baade.