Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watu milioni 15 wanahitaji msaada wa haraka kutokana na ukame katika Pembe ya Afrika

Kituo cha kusambaza maji maeneo yaliyo na ukame Somalia.
© IOM Somalia 2022/ Ismail Osma
Kituo cha kusambaza maji maeneo yaliyo na ukame Somalia.

Watu milioni 15 wanahitaji msaada wa haraka kutokana na ukame katika Pembe ya Afrika

Tabianchi na mazingira

Shrikia la Umoja wa Mataifa la uhamiaji IOM limesema Pembe ya Afrika inakabiliwa na ukame mbaya zaidi kuwahi kushuhudiwa katika kipindi cha miongo kadhaa hali ya ukame, kuongezeka kwa uhaba wa chakula na kusababisha watu wengi kuhama makazi yao.

Taarifa ya IOM kutoka Nairobi Kenya imesema msaada wa dharura na wa ufanisi wa kibinadamu ni muhimu ili kuepuka kuzorota kwa hali kwa kiasi kikubwa katika eneo lote linalotarajiwa kufikia katikati ya mwaka. 

Takriban watu milioni 15 wameathiriwa pakubwa na ukame nchini Kenya, Somalia, na Ethiopia - takriban watu milioni 3, 5 na 7 katika kila nchi, mtawalia. 

Msaada gani unaohitajika?

IOM imeeleza mahitaji ya haraka yanayo hitajika ni pamoja na chakula, maji, usafi wa mazingira na usafi (WASH), afya, bidhaa zisizo za chakula, vitu vitakavyosaidia kuwapatia wananchi riziki pamoja na  kuwasaidia wananchi wenyewe kwa wenyewe kudhibiti migogoro mfano baina ya wakulima na wafugaji.

Kwa muda mrefu, mgogoro wa mabadiliko ya tabianchi duniani umekuwa ukisisitiza haja ya kuwa na ujumuishi katika kupambana na athari zake. Mapambano hayo lazima yajumuishe kushughulikia mahitaji ya kimuundo ya kimaendeleo ya watu walio katika mazingira magumu na kuweka kipaumbele katika upatikanaji wa rasilimali asilia.

Namna nchi zilivyoathirika

Shughuli kubwa ya kuwaingizia kipato wananchi wa Pembe ya Afrika ni Kilimo na Ufugaji, ukame wa muda mrefu umesababisha maeneo mengi upatikanaji wa maji kukauka na hivyo mbali na maelfu ya ekari za mazao kuharibiwa vibaya na ukame, pia jamii zimeshuhudia mifugo yao ikipoteza maisha.

Mvulana akichota maji kutoka mto uliokauka Somalia.
© UNICEF/Sebastian Rich
Mvulana akichota maji kutoka mto uliokauka Somalia.

SOMALIA:

Kulingana na uchambuzi wa hivi karibuni uliofanywa na shirika hilo la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji IOM, hali ya ukame inaweza kuongeza idadi ya wakimbizi wa ndani  kwa zaidi ya watu milioni 1 nchini Somalia, ambayo tayari mpaka ina zaidi ya watu milioni 2.9 ambao wameyakimbia makazi yao.

Serikali ya Somalia ilitangaza hali ya hatari mnamo Novemba 2021.

Kiujumla Somalia imeshuhudia uhaba mbaya zaidi wa maji kuwahi kutokea katika kipindi cha miaka 40 katika baadhi ya maeneo ya nchi.

Kulingana na hali ya awali ya ukame nchini Somalia, idadi ya watu walioathirika wana uwezekano mkubwa wa kuhama kutoka vijijini kwenda mijini. Haki hi ya watu kuhamia mijini  inafanya miji mikuu kuhemewa  kwenye huduma muhimu kama vile huduma za afya, kuongezeka kwa uwezekano wa maambukizi, na kusababisha milipuko ya magonjwa na masuala mengine makubwa yanayohusiana na ukosefu wa huduma za afya.

KENYA:

Maelfu ya ekari za mazao zimeharibiwa kutokana na ukame nchini humo. Athari kwa upande wa mifugo pekee zimeelezwa kuwa mifugo milioni 1.4 walikufa katika robo ya mwisho mwaka jana 2021 kutokana na ukame.

Makumi ya maelfu ya familia wanalazimika kuondoka majumbani mwao kutafuta chakula, maji na malisho, na hivyo kuongeza shinikizo kwa maliasili ambazo tayari zimepunguzwa. Ukame pia umeongeza hatari ya migogoro baina ya jumuiya za wakulima na wafugaji zikishindana kwa ajili ya kupungua kwa maji.

ETHIOPIA:

Utafiti wa IOM katika nchi hii umerekodi ongezeko la harakati za watu kuhama kutokana na kutoka Somalia hadi Ethiopia ili kusaka maji na malisho.

Hata hivyo, Ethiopia pia inakabiliwa na matokeo mabaya ya ukame. Kusini na kusini-mashariki mwa Ethiopia, ukame umeathiri maisha ya angalau jamii milioni 4 za wafugaji na wale ambao wanafanya shughuli zote ufugaji na ukulimo.

Juhudi za pamoja za IOM

Kiujumla IOM inafanya kazi kwa karibu na serikali, mashirika ya Umoja wa Mataifa na washirika wengine katika kila nchi kushughulikia mahitaji makubwa ya maji kwa wakimbizi wa ndani, wahamiaji na makundi yaliyo hatarini ili kuzuia maafa ya kibinadamu.

Kwa pamoja kupitia shughuli uwekezaji wa shughuli zake katika nchi hizo  pamoja na uwezo wa uendeshaji, vifaa, pamoja na ushirikiano wa ndani nchini Kenya, Somalia na Ethiopia, nchini Ethiopia, IOM imejipanga vyema kukabiliana na watu walioongezeka kutokana na kuathiriwa na ukame katika eneo lote la Pembe ya Afrika.