Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Walinda amani wa UN kutoka Tanzania wafanya doria barabara inayounganisha DRC na Uganda

Walinda amani wa Umoja wa Mataifa, Kikosi cha 9 kutoka Tanzania, TANZBATT 9 katika doria ya barabara ya Mbau-Kamango
TANZBATT 9
Walinda amani wa Umoja wa Mataifa, Kikosi cha 9 kutoka Tanzania, TANZBATT 9 katika doria ya barabara ya Mbau-Kamango

Walinda amani wa UN kutoka Tanzania wafanya doria barabara inayounganisha DRC na Uganda

Amani na Usalama

Kufuatia mashambulizi yanayofanywa na makundi mbalimbali ya waasi kwa raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC hususani mashariki mwa nchi hiyo ya pili kwa ukubwa wa eneo barani Afrika, walinda amani wa Umoja wa Mataifa wa kikosi cha 9 kutoka Tanzania, TANZBATT 9 kinachohudumu katika kikosi cha Umoja wa Mataifa cha kujibu mashambulizi cha FIB-MONUSCO, wamefanya doria katika barabara ya Mbau-Kamango nje ya mji wa Beni jimboni Kivu Kaskazini. 

Kapteni Ahmad Waziri Said ambaye ni kamanda wa msafara anaanza kwa kueleza umuhimu wa barabara hiyo akisema ni barabara inayounganisha nchi ya DRC na Uganda "kwa hiyo raia wengi wanaitumia barabara hii kwa shughuli za kibiashara  na kujiongezea kipato." 

Kuhusu lengo la doria hii, Kapteni Said anasema, "tunafanya hivi kwa lengo la kumnyima adui uhuru wa kufanya mauaji kwa kuwa adui amekuwa akifanya uvamizi dhidi ya raia ikiwemo kuwaua watu, kuchoma moto magari na nyumba zao."

Sajenti Fredrick John Mwandri ni mmoja wa walinda amani ambaye ameshiriki doria hii anatoa wito kwa wananchi wa DRC lakini kwanza anaeleza namna ambavyo adui amekuwa akibadilishabadilisha mbinu za mashambulizi akisema "kuna matukio ya ulipukaji wa mabomu kwa hiyo tunawaomba endapo wataona kuna kiashiria chochote ambacho hawajakizoea watoe taarifa kwenye vyombo ambavyo vinahusika ambavyo ni vyombo vya ulinzi. Ninafikiri itatusaidia haya matukio ambayo adui amebadilika kuyafanya yasiweze kujitokeza. Wito wangu kwa raia ni kwamba waendelee kuwa na amani waendelee kufanya shughuli zao ambazo wamekuwa wakizifanya siku zote. Tunaamini kwa jukumu hili ambalo tumeliandaa la ulinzi wa hii barabara hakutakuwa tena na yale matukio ambayo wamekuwawakiyaona mara kwa mara."