Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkakati wa UN na DRC wapaswa kushughulikia changamoto za usalama:Tume

Walinda amani wa MONUSCO kutoka Uruguay akitoa ulinzi kama sehemu ya kukabiliana na Ebola Kivu Kaskazini mwashariki mwa DRC
UN Photo/Martine Perret
Walinda amani wa MONUSCO kutoka Uruguay akitoa ulinzi kama sehemu ya kukabiliana na Ebola Kivu Kaskazini mwashariki mwa DRC

Mkakati wa UN na DRC wapaswa kushughulikia changamoto za usalama:Tume

Amani na Usalama

Serikali nchini Jamhuri ya Kidemkrasia ya Congo DRC na mpango wa Umoja wa Mataifa nchini humo MONUSCO wametakiwa kuunda mkakati wa kina wa pamoja ili kushughulikia changamoto za usalama kwenye eneo la Beni, jimboni Kivu Kaskazini, Mashariki mwa DRC.

Mapendekezo hayo yamefuatia tathimini huru iliyofanyika kufuatia mashambulizi yaliyokatili maisha ya raia ambayo yalifanywa na kundi lenye silaha la ADF mwishoni mwa mwaka jana na kuwa chachu ya maandamano makubwa dhidi ya serikali ya DRC na Umoja wa Mataifa.

Timu ya tathimini ambayo ilijumuisha wataalam wa masuala ya kisiasa, kijeshi na kiufundi ilitaka kubaini mazingira ya shambulio hilo mjini Beni kwenye jimbo la Kivu ya Kaskazini na pia mashambulizi ya eneo la Mambasa jirani na jimbo la Ituri yakilenga juhudi za kitaifa na kimataifa za kukabiliana na mlipuko wa Ebola.

Wajumbe wa timu hiyo wametathimini uwezo wa vikosi vya MONUSCO kutekeleza majukumu yake ya kulinda raia , kukabili makundi yenye silaha na kuweka mazingira salama  kwa wale wanaopambana na mlipuko wa Ebola kwenye eneo hilo.

Tathimini imebaini kwamba kundi la ADF lilikatili Maisha ya watu 260 wengi wakiwa wanawake na watoto katika mwezi wa Novemba na Desemba pekee na mashambulizi mengi yalifanyika usiku. “Idadi kubwa ya vifo vya raia ndio ilikuwa chachu ya kuzuka kwa maandamano yaliyoambatana na machafuko dhidi ya MONUSCO Kivu ya Kaskazini ikiwemo uharibifu mkubwa na uporaji katika ofisi ya MONUSCO Beni mnamo tarehe 25 Novemba.”

Timu hiyo imeongeza kuwa “Mashambulizi dhidi ya raia yaliyokea wakati kjeshi la serikali lilikuwa limeanzisha mashambulizi makubwa dhidi ya ADF tarehe 30 Oktoba 2019. Tangu mwaka 2014 kundi la ADF limekuwa likijibu mashambulizi kwa kushambulia raia kama kulipiza kisasi dhidi ya operesheni za jeshi la serikali ya Congo dhidi yao.”

Mbali ya mkakati wa pamoja timu hiyo ya tathimini imependekeza pia kwamba Umoja wa Mataifa nan chi ya Congo watoe vikosi kwa ajili ya opereshjeni ya pamoja kusaidia kikosi cha MONUSCO cha kujimbu mashambulizi ili kiweze kushughulikia vyema tishio hilo kubwa la wapiganaji wa ADF hasa kwenye mazingira magumu ya changamoto kubwa.

Pia wametaka ushirikiano baina ya MONUSCO na jeshi la serikali ya Congo na polisi uimarishwe zaidi kwani ni muhimu sana katika kuhakikisha hatua zilizopigwa na vikosi vya Congo wakati wa mashambulizi ya hivi karibuni dhidi ya ADF zinaendelea.

Idara ya Umoja wa Mataifa ya operesheni za ulinzi wa amani inaandaa mpango wa kuchukua hatua ili kutekeleza mapendekezo ya timu ya tathimini.