Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ushirikiano kati ya walinda amani wa UN na wananchi utachochea kasi ya kufikia amani DRC

Mlinda amani wa Umoja wa Mataifa kutoka Tanzania akiwa na wanawake kwenye jimbo la Kivu Kaskazini nchini DRC.
TANZBATT_8/Kapteni Tumaini Bagambo.
Mlinda amani wa Umoja wa Mataifa kutoka Tanzania akiwa na wanawake kwenye jimbo la Kivu Kaskazini nchini DRC.

Ushirikiano kati ya walinda amani wa UN na wananchi utachochea kasi ya kufikia amani DRC

Amani na Usalama

Wananchi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC na Walinda amani wa Umoja wa Mataifa kutoka Tanzania wameendelea kuhamasishana kuimarisha ushirikiano kati yao ili kufikia leo kuu la kuleta amani nchini humo.

Anayetuletea taarifa hii kwa kina ni Kapteni Denisia Lihaya ambaye ni Afisa Habari wa Kikundi cha 9 cha walinda amani kutoka Tanzania, TANZBATT 9 wanaohudumu kwenye kikosi cha kujibu mashambulizi, FIB na kile cha utayari QRF chini ya ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini DRC, MONUSCO

Ashantie Sengemoja ni mmoja wa wananchi wa eneo la Beni, Mavivi kaskazini mashariki mwa DRC, yeye ni miongoni mwa wanaotoa wito kwa wananchi wenzake wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kushirikiana na majeshi ya wananchi wa Tanzania walioko katika jukumu la ulinzi wa amani katika eneo la Beni.

“Wananchi wa DRC tushikamane na hawa askari wa Tanzania. Sisi sote ni ndugu tusifanye ubaguzi kwa askrai wa Tanzania. Sisi sote tuko vizuri kabisa.” Anasema Bi. Sengemoja.  

Naye Koplo Janet Mbinda mmoja wa walinda amani kutoka Tanzania anasema, “ujumbe wangu kwa wananchi wa DRC tushirikiane vizuri ili kufanikisha jukumu letu lililotuleta mahali hapa. Na sisi tunaahidi kwamba tutafanya kazi vile ipasavyo.” 

Luteni Kanali Barakaeli Jackson Mley ni Mkuu wa Kikundi cha 9 cha ulinzi wa amani kutoka Tanzania, TANZBATT 9 anasema mpango wao ni kwamba wana mpango mkakati kwa kushirikiana pamoja na “majeshi rafiki kwa maana ya Jeshi la Jmahuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC (FRDC) na MONUSCO, tumejipanga vizuri na moja ya kazi ya majeshi ni kufanya mafunzo na mafunzo tunayoyafanya pamoja na operesheni tunazozifanya ni za pamoja. Kwa hiyo tutaendelea kushirikiana.” 

Kamanda huyo anaeleza zaidi kwamba hawana mpango wa kukata tamaa kuhusu mpango wao wa kuleta kutimiza lengo lililowapeleka nchini humo kwani, “Jeshini hakuna kukata tamaa, tutahakikisha mpaka nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo inapata amani.”