Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mashirika 5 ya UN yaunganisha nguvu kushughulikia tatizo la watoto kuwa na uzito usiolingana na urefu wa miili yao

Afra akiwa amembeba mtoto wake Therese, Mtoto huyo anapimwa utapiamlo katika hospitali ya watoto ya Al Shahhah iliyopo Juba nchini Sudan Kusini
UNICEF/UN0232174/Njiokiktjien VII Photo
Afra akiwa amembeba mtoto wake Therese, Mtoto huyo anapimwa utapiamlo katika hospitali ya watoto ya Al Shahhah iliyopo Juba nchini Sudan Kusini

Mashirika 5 ya UN yaunganisha nguvu kushughulikia tatizo la watoto kuwa na uzito usiolingana na urefu wa miili yao

Afya

Mashirika hayo matano ya Umoja wa Mataifa ni lile la afya ulimwenguni, WHO, la kushughulikia masuala ya watoto UNICEF, Mpango wa chakula duniani WFP, Chakula na Kilimo FAO pamoja na lile linaloshughulikia wakimbizi UNHCR. 

Katika taarifa yao ya pamoja kutoka jijini New York Marekani, Rome Italia na jijini Geneva Uswisi imeeleza kuwa zaidi ya watoto milioni 30 wanakabiliwa na tatizo la kuwa na uzito mdogo na kati yao watoto milioni 8 wana hali mbaya zaidi na kueleza kuwa hali hiyo ni tishio kwa afya na maisha ya watoto hao kwa sasa, na maendeleo ya maisha yao yote na hili pia litaleta athari kwa jamii zao na nchi zao kwa ujumla.

Mtoto mwenye umri wa miezi 7 akichnguzwa utapiamlo unaochochewa na ukame mkali nchiin Somalia.
© UNICEF/Sebastian Rich
Mtoto mwenye umri wa miezi 7 akichnguzwa utapiamlo unaochochewa na ukame mkali nchiin Somalia.

Mpango wa haraka wa kuokoa watoto wenye utapiamlo

Uzito mdogo kwa watoto, unaofafanuliwa  kwa ulinganifu na urefu wa miili yao. uzito mdogo aina mbaya zaidi, kwani watoto hawa wana uwezekano wa kufa mara 12 zaidi kuliko mtoto anayelishwa vizuri.

Mashirika hayo ya UN kwa kauli moja yanataka kuharakishwa kwa Mpango Kazi wa Kimataifa wa uzto mdogo kwa Watoto ambao lengo lake ni mosi kuzuia watoto wasipate uzito mdogo, lakini pia kuwatambua wale walio na uzito mdogo na kuwatibu.

Mataifa yaliyoathirika zaidi ni Kenya, Jamhuri ya Kidemokrasia Kongo DRC, Sudan Kusini, Sudan, Somalia, Ethiopia, Madagascar, Niger, Nigeria, Mali, Burkina Faso, Chad, Yemen, Haiti na Afghanistan.

Miongoni mwa visababishi vya hali hiyo mbaya kwa watoto kutoka mataifa hayo imeelezwa kuwa ni pamoja na vita vinavyoendelea katika nchi hizo, athari zitokanazo na mabadiliko ya tabianchi, muendelezo wa athari za janga la COVID19 lililoikumba dunia pamoja na kuongezeka mara dufu kwa gharama za maisha ambazo zimewaacha watoto wengi katika hali ya kukosa lishe bora na hivyo kukmbwa na utapiamlo wakati ambao hata ufikiwaji wa huduma muhimu za afya za kuokoa maisha yao imekuwa ni ngumu au kutofikika kirahisi.

Mpango huo wa pamoja unahusisha utekelezaji wa kimataifa ambao unaleta pamoja sekta nyingi ili kwa pamoja waweze kuangazia hatua zipi zinafaa kupewa kipaumbele. Hatua hizo zinaanzia kwenye lishe ya mama kwa ajili ya mtoto aliye tumboni kuhakikisha mtoto anapata chakula, unaangazia pia afya, maji safi na usafi wa mazingira bila kusahau mifumo ya ulinzi wa kijamii.

Katika kukabiliana na mahitaji yanayoongezeka, mashirika ya Umoja wa Mataifa yalibainisha hatua tano za kipaumbele ambazo zitakuwa na ufanisi katika kukabiliana na utapiamlo mkali katika nchi zilizoathiriwa na migogoro na majanga ya asili na katika dharura za kibinadamu.

Mashirika hayo yanaamini hatua hizi zikiwa pamoja kama kifurushi kilichoratibiwa itakuwa muhimu kwa kuzuia na kutibu utapiamlo mkali kwa watoto, na kuepusha hasara mbaya ya maisha yao yote.

UNICEF/UN0640824/Dejongh
Picha: UNICEF/UN0640824/Dejongh
UNICEF/UN0640824/Dejongh

Kauli za viongozi wakuu wa mashirika hayo matano

Mashirika ya Umoja wa Mataifa yanatoa wito wa kuchukua hatua madhubuti na kwa wakati ili kuzuia tatizo hili kuwa janga kwa watoto walio hatarini zaidi duniani. Mashirika yote yanahimiza uwekezaji mkubwa zaidi katika kuunga mkono jitihada hizo zilizoratibiwa na Umoja wa Mataifa ambazo zitakidhi mahitaji ambayo hayajawahi kushuhudiwa katika mzozo huu unaokua, kabla haijawa hatari zaidi kwakuwa watu watakuwa wamechelewa kuleta suluhu.

WHO

Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt. Tedros Adhamon Ghebreyesus amesema mgogoro wa chakula duniani pia ni janga la afya na huu ni mzunguko mbaya kwani ukosefu wa lishe husababisha magonjwa, na magonjwa husababisha lishe duni. “Msaada wa haraka unayohitajika sasa katika nchi zilizoathirika zaidiili kulinda maisha na afya za watoto, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha upatikanaji muhimu wa vyakula vyenye afya na huduma za lishe, hasa kwa wanawake na watoto.”

UNICEF

Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF Catherine Russell amesema “Machafuko yanayoendalea yanafanya kuwa ngumu kuwafikia milioni ya watoto wenye utapiamlo mkali kufikiwa na huduma muhimu. Utapiamlo mkali ni uchungu kwa mtoto, na katika hali mbaya husababisha kifo au kuleta madhara katika Maisha yake yote. Tunaweza na ni lazima tuondoe tatizo hili la lishe kupitia suluhu zilizothibitishwa za kuzuia, kugundua, na kutibu utapiamlo wa watoto mapema.”

Mtoto akiwa amebebwa na mama yake wakati pia akipatia chakula cha lishe ambacho pia ni tiba ya utapiamlo huko nchini Somalia.
UNICEF/UN0591078/Taxta
Mtoto akiwa amebebwa na mama yake wakati pia akipatia chakula cha lishe ambacho pia ni tiba ya utapiamlo huko nchini Somalia.

UNHCR

Fillipo Grandi, Kamishna Mkuu wa shirika la kuhudumia wakimbizi “Sisi UNHCR tunafanya kazi kwa bidii ili kuboresha uchanganuzi na tunalenga kuhakikisha kwamba tunawafikia watoto walio katika hatari zaidi, ikiwa ni pamoja na wakimbizi wa ndani na wakimbizi wote kwa ujumla.”

FAO

QU Dongyu, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Chakula FAO amesema hali inaweza kuwa mbaya zaidi mwaka huu wa 2023. "Lazima tuhakikishe kuna upatikanaji, uwezo wa kununua na ufikiwaji wa vyakula vyenye afya kwa watoto wadogo, wasichana, wanawake wajawazito na wanaonyonyesha. Tunahitaji kuchukua hatua za dharura sasa ili kuokoa maisha, na kukabiliana na sababu kuu za uzito mdogo, tukifanya kazi pamoja katika sekta zote.”

WFP

David Beasley, Mkurugenzi Mkuu wa Mpango wa chakula duniani WFP anasema lazima tuchukue hatua sasa na kwakushirikiana. “Zaidi ya watoto milioni 30 wana uzito  mdogo katika nchi 15 zilizoathirika zaidi, hivyo ni lazima tuchukue hatua sasa na tuchukue hatua kwa pamoja. Ni muhimu kwamba tushirikiane kuimarisha mitandao ya usalama wa kijamii na usaidizi wa chakula ili kuhakikisha Vyakula Maalumu vya Lishe vinapatikana kwa wanawake na watoto wanaovihitaji zaidi.”

Mtoto anayeugua utapiamlo akipata matibabu katika hospitali Sana'a.
UNICEF
Mtoto anayeugua utapiamlo akipata matibabu katika hospitali Sana'a.

Utapiamo mkali ni nini?

Uzito mdogo ni aina ya utapiamlo unaosababishwa na mtoto kutokuwa na afya kwasababu ya  kupata chakula kidogo / au ugonjwa unaosababisha uzito wa mtoto kupungua ghafla au uvimbe.

Watoto walio na uzito mdogo ikilinganishwa na urefu wao wanaweza pia kuwa ishara nyingine za kiafya.

Uzito mdogo unadhoofisha kinga ya mwili na watoto wenye ugonjwa huu wako katika hatari kubwa ya kufa kutokana na magonjwa ya kawaida ya utotoni. Wale ambao wanaweza kuishi wanaweza kukabiliana na changamoto za ukuaji katika kipindi chote cha maisha yao pamoja na changamoto nyingine za maendeleo.

Watoto hawa wanaweza kuwa ni wagonjwa mara kwa mara, shuleni wanakuwa na maendeleo duni na pia familia zao zinaweza kuwa na ufukara.