Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mabadiliko ya tabianchi na majanga mengine yaweka njiapanda SDGs:UN

Mkazi wa  Kirbet Tabbanmoja ya jamii 13 zilizo katika hatari ya kuhamishwa kwa lazima kwenye mji wa Masafer Yatta, kwenye Ukingo wa Magharibi, 16 Juni 2022
OCHA
Mkazi wa Kirbet Tabbanmoja ya jamii 13 zilizo katika hatari ya kuhamishwa kwa lazima kwenye mji wa Masafer Yatta, kwenye Ukingo wa Magharibi, 16 Juni 2022

Mabadiliko ya tabianchi na majanga mengine yaweka njiapanda SDGs:UN

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Ripoti mpya ya malengo ya maendeleo endelevu SDGs kwa mwaka 2022 iliyotolewa leo na Umoja wa Mataifa imesema mgogoro wa mabadiliko ya tabianchi, janga la COVID-19 na ongezeko la idadi ya migogoro na vita kote duniani vimeyaweka malengo yote 17 ya maendeleo endelevu njiapanda.

Ripoti hiyo inatanabaisha kiwango na ukubwa wa changamoto zilizo mbele yetu, na migogoro hii inayoendelea na inayoleta changamoto ikiwemo athari za mabadiliko katika chakula na lishe, afya, elimu, mazingira, na amani na usalama, na kuathiri malengo yote ya SDGs ambayo ni mwongozo wa jamii imara zaidi, zenye mnepo, amani na usawa.

Mambo muhimu yaliyoainishwa na ripoti

Familia wakibeba mali zao kufuatia mafuriko Bentiu, Sudan Kusini.
© UNICEF/Sebastian Rich
Familia wakibeba mali zao kufuatia mafuriko Bentiu, Sudan Kusini.

• Ripoti imesema janga la coronavirus">COVID-19 limeleta changamoto kubwa katika malengo  ya maendeleo na athari zake bado hazijaisha.

• Duniani kote kumekuwa na Vifo vya kupita kiasi vya moja kwa moja na kwa njia isiyo ya moja kwa moja vinavyotokana na janga la COVID-19 na hadi kufikia mwishoni mwa mwaka 2021 idadi ya vifoo ilikuwa milioni 15.

• Zaidi ya miaka minne ya hatua zilizopigwa katika maendeleo kwenye nyanja ya kupunguza umaskini imeondolewa na changamoto hizo na kusukuma watu milioni 93 zaidi duniani kote katika umaskini uliokithiri mwaka 2020.

•Ripoti pia imesema dunia iko katika hatihati ya zahma kubwa ya mabadiliko ya tabianchi ambapo mabilioni ya watu tayari wanayahisi matokeo yake.

• Pia uzalishaji wa hewa ukaa unaohusiana na nishati uliongezeka kwa asilimia 6 kwa mwaka 2021 na kufikia kiwango  cha juu kabisa kuwahi kushuhudiwa na kufunika kabisa mapungufu yanayohusiana na janga la COVID-19.

• Ripoti pia imeainisha kwamba vita nchini Ukrainia vinaleta moja ya matatizo makubwa zaidi ya wakimbizi kwa nyakati za sasa.

Hadi kufikia Mei 2022, zaidi ya watu milioni 100 wamelazimika kuyahama makazi yao.

 

Janga la mabadiliko ya tabianchi

Ukame unaathiri mamilioni ya watu Kenya, Ethiopia na Somalia
© FAO/Patrick Meinhardt
Ukame unaathiri mamilioni ya watu Kenya, Ethiopia na Somalia

Ripoti imetanabaisha kwamba dunia iko katika hatihati ya janga la mabadiliko ya tabianchi kwani mabilioni ya watu kote duniani tayari wanakabiliwa na matokeo ya ongezeko la  joto na hali ya hewa inayozidi kuwa mbaya.

Ili kuepusha athari mbaya zaidi za mabadiliko ya tabianchi uzalishaji wa gesi chafu duniani ripoti inasema lazima ukomeshwe  kabla ya 2025 na kisha upungue kwa asilimia 43 ifikapo 2030, na kutozalishwa kabisa ifikapo 2050.

Hata hivyo ripoti inasema badala yake, katika ahadi za sasa za hiari za kitaifa (NDCs) dhidi ya mabadiliko ya tabianchi, uzalishaji wa gesi chafuzi unatarajiwa kuongezeka kwa karibu asilimia 14 katika muongo ujao.

Na mwaka huu, wastani wa tani milioni 17 za plastiki ziliingia baharini  idadi ambayo inatarajiwa kuongezeka mara mbili au tatu ifikapo 2040.

Madhara ya vita vya Ukraine

Mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 9 akiwa na mdogo wake wa kiume mwenye umri wa miaka 3 wakiwasili katika kituo cha muda cha makazi nchini Romania baada ya kukimbia vita Ukraine
© UNICEF/Ioana Moldovan
Mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 9 akiwa na mdogo wake wa kiume mwenye umri wa miaka 3 wakiwasili katika kituo cha muda cha makazi nchini Romania baada ya kukimbia vita Ukraine

Wakati huo huo, vita vya Ukraine vinasababisha moja ya migogoro mikubwa kabisa ya wakimbizi ya wakati wa sasa, kulingana na ripoti hiyo.

Kufikia Mei, zaidi ya watu milioni 100 wamelazimika kuyakimbia makazi . Na mzozo huo umesababisha bei ya chakula, mafuta na mbolea kupanda kwa kasi, kutatiza zaidi minyororo ya ugavi na biashara ya kimataifa, kuyumba kwa masoko ya fedha, na kutishia uhakika wa chakula na usambazaji wa misaada duniani.

Waathirika wakubwa

Kwa mujibu wa ripoti nchi na makundi ya watu walio hatarini ndio waathirika wakubwa wa changamoto hizi wakiwemo wanawake ambao wamepoteza kazi zao na kubebeshwa mzigo mkubwa ukiwemo wa kazi za nyumbani.

Na janga la COVID-19 limezidisha ukatili dhidi ya wanawake na wasichana. Nchi zenye maendeleo duni zimekuwa zikihaha kutokana na ukuaji mdogo wa uchumi, kupanda kwa mfumuko wa bei, kuathirika kwa mnyororo wa usambazaji, madeni yasiyotarajiwa, fursa finyu za ajira kwa vijana, na ongezeko la ndoa za utotoni na ajira kwa watoto.

Katika nchi za kipato cha chini ripoti inaonyesha kuwa kiwango cha madeni ya umma kiliongezeka kwa wastani wa asilimia 3.1 mwaka 2011 na kufikia asilimia 8.8 mwaka 2020.