Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hatuwezi kutatua zahma zinazotukabili katika dunia iliyogawanyika bila mshikamano: Guterres

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akihutubia kongamano la kiuchumi duniani WEF, mjini Davos, Uswisi.
© World Economic Forum
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akihutubia kongamano la kiuchumi duniani WEF, mjini Davos, Uswisi.

Hatuwezi kutatua zahma zinazotukabili katika dunia iliyogawanyika bila mshikamano: Guterres

Ukuaji wa Kiuchumi

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema dunia haiwezi kutatua changamoto kubwa inazokabiliwa nazo hivi sasa kuanzia mabadiliko ya tabianchi, vita ya Ukraine, mdororo wa uchumi na athari zinazoendelea za janga la COVID-19 katikia hali ya sasa ya mgawanyiko na kutokuwa na mshikamano hivyo wakati wa kufumbia macho changamoto hizi umepita na wanaochangia wawajibishwe.  

Katibu Mkuu Guterres ameyasema hayo mjini Davos Uswis katika hotuba yake kuhusu hali ya dunia kwenye siku ya pili ya jukwaa la uchumi duniani akibainisha kwamba wakati dunia inahitaji ushirikiano zaidi katika masuala ya mabadiliko ya tabianchi , upunguzaji wa mzigo wa madeni na afya uya kimataifa kuna mgawanyiko na changamoto inaongezeka linapokuja suala ya vita ya Ukraine  akisema "Hasa uvamizi wa Urusi kwa Ukraine sio tu kwa sababu ya mateso yasiyoelezeka kwa watu wa Ukraine, lakini kwa sababu ya athari zake kubwa za kimataifa kwa bei ya chakula na nishati, kwenye minyororo ya biashara na usambazaji na maswala ya usalama wa nyuklia, kwa misingi hiyo hiyo ya sheria za kimataifa”.  

Kuhusu changamoto zote hizi zinazoizonga dunia amesema “Tunaangalia jicho la kimbunga kilicho katika daraja la 5.” 

Katika Asasi za Kiraia na Siku ya Nishati katika mkutano wa COP27, wanaharakati wanaandamana kupinga utafutaji wa mafuta na gesi barani Afrika.
UN News/Laura Quinones
Katika Asasi za Kiraia na Siku ya Nishati katika mkutano wa COP27, wanaharakati wanaandamana kupinga utafutaji wa mafuta na gesi barani Afrika.

Wachochea mabadiliko ya tabianchi wawajibishwe 

Bwana Guterres akisisitiza kuhusu suala la mabadiliko ya tabianchi amelaani makampuni makubwa ya mafuta kwa kupuuza sayansi kuhusu mabadiliko ya tabianchi, na kushutumu sekta ya mafuta na gesi kwa kutafuta kupanua zaidi wigo wa uzalishaji licha ya kujua kwamba kwamba mtindo wao wa biashara hauendani na maisha ya binadamu.   

Ametoa wito kwa viongozi wa dunia kuweka mbele mipango ya mpito ya kuaminika na ya uwazi ili kufikia lengo la kutozalisha kabisa hewa ukaa na kuwasilisha mipango yao kabla ya mwisho wa mwaka.  

"Kutozalisha kabisa hewa ukaa lazima iwe msingi katika kupunguza uzalishaji wa hewa chafuzi na sio kutegemea mikopo ya hewa ukaa na soko kivuli. Ndio maana sisi Umoja wa Mataifa tuliunda kikundi cha wataalamu wa ahadi za zzalishaji sufiri wa hewa ukaa au Net-Zero." 

Pia amewataka wafanyabiashara kufuata miongozo ya kikundi hicho kwa ahadi za kuaminika, zinazowajibika bila uzalishaji wa hewa ukaa. 

Akilinganisha na sekta ya tumbaku katika miaka ya 1970 ambapo makampuni yalijua madhara ya hatari ya kiafya ya tumbaku amesema "Makampuni makubwa ya mafuta lazima yazingatie madhara ya nishati ya mafuta kisukuku kwenye sayari yetu. Baadhi ya makampuni makubwa ya mafuta wanadanganya kwa kiasi kikubwa na kama vile ilivyo kwa sekta ya tumbaku, wale wanaohusika kuchochea mabadiliko ya tabianchi lazima wawajibishwe."  

Migawanyiko kila kona  

Kuhusu vitisho muhimu vinavyoikabili dunia, Guterres amesema mojawapo ya hatari zaidi ni kile alichokiita "Msukosuko Mkubwa”, au mgawanyiko wa mataifa mawili makubwa ya kiuchumi duniani, Marekani na China akiuita ni "mpasuko wa kitektoni” ambao utaunda kambi mbili tofauti za sheria za biashara, sarafu mbili kuu, mitamndao miwili ya intaneti na mikakati miwili inayokinzana juu ya akili bandia. 

Kulingana na shirika la fedha la Kimataifa, IMF kugawanya uchumi wa dunia katika kambi mbili kunaweza kupunguza pato la taifa kwa dola trilioni $1.4 "Hili ni suala la mwisho tunalohitaji," amesema. 

Ameendelea kusema migawanyiko hiyo mikubwa ni baina ya Mashariki na Magharibi hasa Marekani na Uchina hususan katika suala la haki za binadamu na usalama wa kikanda na mgawanyiko wa Kaskazini na Kusini ambao amesema hashawishiki kwamba Kaskazini inatambua kiwango cha madhila yanayowakabili watu wa Kusini hasa linapokuja suala la afya kuhusu usawa wa usambazaji wa chanjo. 

Guterres alisema hata hivyo inawezekana na kwa kweli ni muhimu kwa nchi hizo mbili "Kuwa na ushirikiano wa maana juu ya mabadiliko ya tabianchi, biashara na teknolojia ili kuzuia kuvunjika kwa uchumi au hata uwezekano wa makabiliano ya siku zijazo." 

Jamii za milimani katika mkoa wa Hindu Kush Himalaya, pamoja na manispaa ya Mustang huko Nepal tayari zimeanza kuona athari za kupoteza viumbe hai, kuongezeka kwa kuyeyuka kwa glacial kutokana na upatikanaji mdogo wa maji unaotabirika.
UN Nepal
Jamii za milimani katika mkoa wa Hindu Kush Himalaya, pamoja na manispaa ya Mustang huko Nepal tayari zimeanza kuona athari za kupoteza viumbe hai, kuongezeka kwa kuyeyuka kwa glacial kutokana na upatikanaji mdogo wa maji unaotabirika.

Kinachohitajika kutatua changamoto hizi 

Katibu Mkuu amehitimisha hotuba yake kwa kutoa wito kwa serikali zote, sekta binafsi na wadau wote kuunda njia za ushirikiano zaidi, ikisisitiza haja ya kuziba pengo la migawanyiko yote kwa kurekebisha na kujenga usawa katika mfumo wa fedha wa kimataifa, Kuchukua hatua za maana dhidi ya mabadiliko ya tabianchi, Kurekebisha muundo wa biashara na mazoea ili kuendeleza malengo ya maendeleo endelevu, kuongoza njia ya kufikia fursa za kiuchumi kwa wanawake, na kufikia lengo la uhakika wa chakula duniani .  

Pia amesema "Mfumo wa kifedha uliofilisika kimaadili unakuza ukosefu wa usawa wa kimfumo.” 

Ametoa wito wa kuwepo kwa usanifu mpya wa madeni ambao utatoa ukwasi, msamaha wa madeni na mikopo ya muda mrefu ili kuwezesha nchi zinazoendelea kuwekeza katika maendeleo endelevu. 

"Nchi zinazoendelea zinahitaji upatikanaji wa fedha ili kupunguza umaskini na njaa na kuendeleza malengo ya maendeleo endelevu," amesema. 

Amehimiza nchi za G20 kukubaliana juu ya mpango wa kichocheo wa SDGs wa kimataifa ili kusaidia nchi za Kusini mwa Ulimwengu. 

Hivyo amesisitiza  kwamba “Sasakuliko wakati mwingine wowote, ni wakati wa kutengeneza njia za ushirikiano katika dunia yetu lililogawanyika kwani dunia haiwezi kusubiri."