Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ndoa za utotoni zashamiri Pembe ya Afrika - UNICEF

Watoto wa kike wanakuwa hatarini kuozeshwa mapema na wengi wao ni wale wanaotoka familia maskini na makundi ya pembezoni
©UNFPA-UNICEF Nepal/KPanday
Watoto wa kike wanakuwa hatarini kuozeshwa mapema na wengi wao ni wale wanaotoka familia maskini na makundi ya pembezoni

Ndoa za utotoni zashamiri Pembe ya Afrika - UNICEF

Sheria na Kuzuia Uhalifu

Watoto wa kike wenye umri mdogo hata miaka 12 huko Pembe ya Afrika wanalazimishwa kuolewa sambamba na kukeketwa au FGM, katika viwango vya kutisha wakati huu ambapo ukame mkali kuwahi kukumba eneo hilo katika kipindi cha miaka 40 ukisukuma familia katika mazingira magumu, limesema shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto duniani, UNICEF.

Katika taarifa iliyotolewa leo mjini Nairobi, Kenya, UNICEF imesema nchini Ethiopia ambako ukame umeathiri zaidi, ndoa za utotoni zimeongezeka maradufu katika kipindi cha mwaka mmoja.

UNICEF inasema hatari ya watoto kuwa watoro shuleni kutokana na janga la ukame imeongezeka mara tatu zaidi katika nchi za Ethiopia, Somalia na Kenya, na hivyo kuacha wasichana barubaru katika hatari kubwa kutokana na kukosa ulinzi ikiwemo hatari za kukeketwa na kulazimishwa kuolewa.

Watoto wa kike wenye umri wa miaka 12 waozeshwa kwa watu wazima

“Tunaona viwango vya juu vya ndoa za utotoni hapa Pembe ya Afrika sambamba na familia hohehahe zikiweka mipango ya kuoza watoto wao wa kike hata wenye umri wa miaka 12 kwa wanaume walio na umri wa mara tano zaidi kiumri,” amesema Andy Brooks, Mshauri wa UNICEF kuhusu ulinzi wa mtoto katika ukanda wa Mashariki na Kusini mwa Afrika.

Amesema “ndoa za utotoni na ukeketaji vinatowesha utoto na kuchochewa watoto wa kike kuacha shule na hivyo kuwaweka hatarini zaidi kukumbwa na ukatili wa majumbani na umaskini wa maisha.”

Mshauri huyo amesema hilo ni janga la watoto na wanahitaji fedha haraka ili kuongeza operesheni zao huko Ethiopia, Kenya na Somalia, “na siyo tu kuokoa maisha kwa muda mfupi, bali kuwapatia ulinzi wa muda mrefu.”

Taarifa hiyo ya UNICEF inasema “katika eneo lote la pembe ya Afrika, familia zinakabiliwa na uamuzi mgumu wa kuishi katikati ya janga la ukame lililochochewa na mabadiliko ya tabianchi. Vyanzo vya maji vimekauka, mifugo imekufa bila kusahau athari za vita ya Ukraine iliyochochea ongezeko la bei ya mafuta.”

Zaidi ya watoto milioni 1.8 wanahitaji matibabu ya utapiamlo uliokithiri  huku watu 213,000 wakielezwa kuwa wako hatarini kukumbwa na baa la njaa Somalia.