Kuokoa watu Kenya, Somalia, Djibouti na Ethiopia, FAO yaomba dola milioni 172

27 Juni 2022

Kutokana na kuongezeka kwa hatari ya njaa katika Pembe ya Afrika kunakosababishwa na hali mbaya ya ukame wa muda mrefu, shirika la Umoja wa ,Mataifa la Chakula na Kilimo FAO, limeonya kuwa msaada wa dharura wa kuokoa maisha unahitajika haraka ili kuepusha janga la kibinadamu. 

Wakati kilele cha janga kinakaribia kwa kasi, FAO imezindua Mpango wa haraka wa Kukabiliana na hali hiyo ambao unaangazia nchi nne pekee ambazo ziko katika hali mbaya zaidi yaani  Djibouti, Ethiopia, Kenya na Somalia.  

Taarifa ya FAO iliyotolewa hii leo Roma, Italia, imeeleza kuwa muda wa mpango huo mpya umeongezwa kutoka Juni hadi Desemba 2022 kwa lengo la kuzuia kuzorota kwa hali ya uhakika wa chakula katika kanda, kuokoa ustawi wa watu na hivyo maisha ya karibu watu milioni tano wa vijijini katika nchi zote nne. 

FAO inaomba jumla ya dola milioni 219 ili kutekeleza mipango yake katika eneo hilo la Pembe ya Afrika. Kufikia sasa, Shirika hilo la Umoja wa Mataifa limekusanya karibu dola milioni 47, na kuacha pengo la dola milioni 172. 

Kituo cha kusambaza maji maeneo yaliyo na ukame Somalia.
© IOM Somalia 2022/ Ismail Osma
Kituo cha kusambaza maji maeneo yaliyo na ukame Somalia.

“Ingawa fedha zilizopokelewa kufikia sasa zitatoa usaidizi wa kuokoa maisha kupitia fedha na vifurushi vya usaidizi wa maisha, ikiwa ni pamoja na afya ya wanyama na ukarabati wa miundombinu kwa takriban watu 700,000, mamilioni zaidi wanaweza kufikiwa ikiwa mpango huo utafadhiliwa kikamilifu.” Imesema taarifa ya FAO. 

Rein Paulsen, Mkurugenzi wa Ofisi ya Dharura na Mnepo wa FAO amesema, "ustawi wa kilimo haufadhiliwi kwa kiasi kikubwa katika hatua za usaidizi wa  kibinadamu, hata katika ukame, wakati kilimo kinabeba asilimia 80 ya athari. Kufanya mambo kwa mazoea sio chaguo tena. Ni wakati wa kuwekeza vizuri katika usaidizi wa ufanisi zaidi na wa kuangalia mbele. Hili lazima lihusishwe na usaidizi wa muda mrefu wa maendeleo”. 

Kuongezeka kwa uhaba wa chakula 

Kufikia mapema mwezi Mei mwaka huu, msimu wa mvua za kati ya Machi na Mei ulikuwa duni  katika Ethiopia, Kenya na Somalia kusababisha athari mbaya kwa uhakika wa chakula. Mpangilio wa mvua wa Djibouti unatofautiana na ule wa nchi zingine tatu ingawa mvua huko pia ilikuwa ya kusuasua mnamo mwaka 2021. 

Mpango uliorekebishwa 

Mpango wa kukabiliana na ukame uliorekebishwa unajumuisha vipengele vya FAO vya rufaa za kibinadamu katika nchi zinazolengwa. Mpango unatoa maelezo zaidi kuhusu kile ambacho kinahitaji kutokea kwa dharura ili kufikia kiwango cha kuanzia Januari 2022 na hatari zinazohusiana na hatua zisizotosha au zisizozingatia muda.  

Mpango huo pia unaeleza kuwa kukabiliana na ukame ni, kwanza kabisa, kuhusu kutekeleza seti sahihi ya hatua kwa wakati unaofaa wa mzunguko wa ukame. Washirika watalazimika kusawazisha rasilimali kati ya kila sekta ya kuokoa maisha, ambayo ni a) msaada wa chakula na mahitaji mengine ya maisha b) lishe; c) maji, usafi wa mazingira na usafi; na d) afya. Kukosa kujibu moja ya sekta nne zilizotajwa hapo juu kutadhoofisha juhudi za zingine. 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter