Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukame Pembe ya Afrika: UN katu haiwezi kusahau licha ya majanga mengine duniani

Bi. Joyce Msuya, Msaidizi wa Katibu Mkuu wa UN na Naibu Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya dharura, OCHA katika mahojiano na UN News Kiswahili Aprili 2022 New York, Marekani.
UN/ Anold Kayanda
Bi. Joyce Msuya, Msaidizi wa Katibu Mkuu wa UN na Naibu Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya dharura, OCHA katika mahojiano na UN News Kiswahili Aprili 2022 New York, Marekani.

Ukame Pembe ya Afrika: UN katu haiwezi kusahau licha ya majanga mengine duniani

Msaada wa Kibinadamu

Licha ya majanga mengine ya kibinadamu yanayoendelea duniani ikiwemo kule Ukraine, bado Umoja wa Mataifa unahangaika kila uchao kuhakikisha inasaidia wakazi wa Pembe ya Afrika ambako ukame umesababisha watu milioni 15 kukosa uhakika wa chakula, amesema Joyce Msuya Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na Naibu Mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa inayoratibu misaada ya dharura, OCHA.
 

 

Bi. Msuya ametoa kauli hiyo katika mahojiano maalum na Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani akisema nchi ambazo zimeathirika zaidi na ukame ni Kenya, Somalia na Ethiopia.

Soundcloud

 

Taswira ya Njaa

Bi. Msuya ametolea mfano familia moja nchini Kenya ambayo hivi sasa kiogozi wa kaya hiyo ana ajira na tegemeo lake lilikuwa ni kilimo ambacho kimeathiriwa na ukame.

“Kwa sasa hivi kwenye familia yake ana mke na watoto wanne, wanakula mlo moja tu. Na si mlo mmoj ambao wao wanapenda  na siyo tu mlo mmoja, kwa sababu kabila lao wanapenda sana ugali, sasa hivi anakunywa uji kwa sababu hawezi kununua unga wa kutosha ugali wa kulisha familia ya watu sita. Alikuwa ana shamba kijijini anaenda analima na kuleta mazao. Lakini mvua hazinyeshi, mazao yamekauka.”

Kwa kijana huyo hivi sasa analazimika kununua mboga kama vile maharage, halikadhalika mahindi. Unga wa  uji bei imepanda sokoni kutokana na vita vinavyoendelea. Kama alikuwa anweza kutumia shilingi 10 kununua unga, sasa hivi fedha hiyo haiwezi kununua kiasi cha unga alichokuwa ananunua miezi mitatu iliyopita.

Naibu Mkuu huyo wa OCHA anasema huo ni mfano mmoja unaowakilisha kaya nyingi katika Pembe ya Afrika, kuanzia Sudan Kusini na kwingineko,hali inayosababisha mifarakano kwenye familia ambazo zinalazimika kuhama kusaka chakula.

Familia za Turkana zinatumia kilimo cha umwagiliaji kulima mazao ya chakula wakati wa ukame wa muda mrefu nchini Kenya.
UNDP/Ngele Ali
Familia za Turkana zinatumia kilimo cha umwagiliaji kulima mazao ya chakula wakati wa ukame wa muda mrefu nchini Kenya.

Ukame Pembe ya Afrika unatishia mafanikio ya Ajenda 2030

Bi. Msuya amesema bila shaka ukame na njaa vinatishia mafanikio ya ajenda 2030 akitolea moja ya malengo hayo lile la elimu akisema, “watoto wanakumbwa na njaa na hivyo uwezo wao wa kwenda shuleni na kusoma unaathirika. Kwa hiyo tunachofanya OCHA mwisho wa mwezi huu wa Aprili tutakuwa na mkutano mkubwa wa kuwaleta pamoja wahisani kuweza kuchangia fedha ili kusaidia Pembe ya Afrika.

Hali ya Ufadhili

Kwa upande wa Somalia, OCHA inasema hadi tarehe 7 mwezi Aprili mwaka huu wa 2022 ombi la dola bilioni 1.5 za kusaidia watu milioni 5.5 walio hatarini Somalia lilikuwa limefadhiliwa kwa asilimia 4.4 pekee.

UN inafanya nini sasa

WFP ofisi ya kanda iko Nairobi, Kenya, sasa inaangalia jinsi gani ya kutumia fedha zilizopo kununua mahindi ya kusambaza kwa nchi zenye uhitaji. Pia tunaangalia jinsi gani mashirika ya kiraia yanaweza kupata fedha kutoka mfuko wa fedha za dharura kama vile za ukame, wachukue wanunue chakula na kupeleka. “Mashirika mengi ya kiraia yako mashinani, halikadhalika mashirika ya kidini yako karibuni zaidi na wananchi wanaweza kufikisha.”

OCHA itatumia nini kushawishi wahisani kuchangia hivi sasa?

Bi. Msuya anasema muhimu ni takwimu kwa sababu huu ni ukame wa tatu katika miaka mitano iliyopita. “Tatizo ambalo sasa hivi ni changamoto na tunafanyika kazi, ni tatizo hili la Ukraine, pesa nyingi pia zinaenda, kwa hiyo kuna mashindano katika dharura duniani. Kuna Ulaya, kuna Yemen, kuna Syria, kuna Afghanistan. Ni jinsi gani tunaweza kusema hapa tumepata kidogo, tuongeze kasi kwingine. Lingine tunafanya kazi na serikali, tunaweza kuwapa takwimu ili wawasilishe kwa wahisani kwenye mikutano ambayo Umoja wa Mataifa haiko kwenye mazungumzo.

Kidimbwi cha maji kikiwa kinachotumiwa kama chanzo cha maji ya kunywa kwa mifugo inayotembea umbali mrefu kuweza kupata maji njiani. Hapa ni Ethiopia
© UNICEF/Mulugeta Ayene
Kidimbwi cha maji kikiwa kinachotumiwa kama chanzo cha maji ya kunywa kwa mifugo inayotembea umbali mrefu kuweza kupata maji njiani. Hapa ni Ethiopia

Umoja wa Mataifa haiwezi kusahau Afrika

Suala la kusahauliwa Afrika, halipo kwa kuwa katika kila mikutano hoja ya Afrika inakuwepo na hata Katibu Mkuu Guterres anapaza sauti isisahaulike. Na tunajadili kuwa kati ya Mkuu wa OCHA au mimi ataenda Afrika Mashariki kuangalia hali  halisi.

Changamoto ipo na ni “kati ya sasa hivi na mwisho wa mwezi huu wa Aprili ni simu ngapi tupige, ngoma ngapi tupige ili wahisani wasisahau huo mkutano ambao tutafanya kuwaomba ili waongeze fedha,” amesema Bi. Msuya.

Ujumbe kwa wakazi wa Pembe ya Afrika

Kwanza Umoja wa MAtaifa haujasau na bado tunatazama na ndio maana kuanzia sasa hadi mwisho wa mwezi huu kuona mkutano unafanyika na wahisani wanashiriki.

Pili “naomba watumie sauti zao kukumbusha viongozi, wanajumuiyam makanisa, misikiti kuendelea kuhamasisha jumuiya na kuonesha kwamba hili ni tatizo. Sasa hivi kuna simu za mkononi, kuonesha hali halisi kuhamasisha kuna nchi ambazo zimeendelea wananchi tu wa kawaida wanapenda kutoa ili kusaidia watu wengine na la tatu, tuko pamoja.”