Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

FAO yapokea zaidi ya dola 227,500 kutoka Ujerumani kuepusha janga la njaa pembe ya Afrika

Mgao wa vyakula vya mifugo vyenye virutubisho kwa wafugaji wa Isiolo nchini Kenya kwa lengo la kuhakikisha wanaendelea kupata siyo tu lishe na maziwa bali pia kuuza bidhaa za mifugo na kupata kipato .
©FAO/Luis Tato
Mgao wa vyakula vya mifugo vyenye virutubisho kwa wafugaji wa Isiolo nchini Kenya kwa lengo la kuhakikisha wanaendelea kupata siyo tu lishe na maziwa bali pia kuuza bidhaa za mifugo na kupata kipato .

FAO yapokea zaidi ya dola 227,500 kutoka Ujerumani kuepusha janga la njaa pembe ya Afrika

Msaada wa Kibinadamu

Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo FAO hii leo limekaribisha mchango wa zaidi ya dola 227,5180 kutoka Ujerumani kwa ajili ya kuokoa maisha ya wakulima na wafugaji walioathiriwa zaidi na ukame katika Pembe ya Afrika.

Taarifa ya FAO kutoka Roma nchini Italia imeeleza huu ni mchango muhimu na umekuja wakati mahususi katika kukabiliana na dharura ya ukame inayowakabili wananchi wengi wa pembe ya Afrika.

Mkurugenzi Mkuu wa FAO QU Dongyu amenukuliwa katika taarifa hiyo akisema msaada wa Ujerumani unawakilisha mchango mkubwa katika mpango wa FAO wa kukabiliana na ukame wa Pembe ya Afrika ambako wanahitaji zaidi ya dola milioni 138 kusaidia jamii za vijijini kukabiliana na ukame unaowakabili, na katika fedha zinazoombwa,  dola milioni 130 zinahitajika haraka kwa shughuli malimbali kati ya mwezi huu wa Februari na Juni mwaka huu wa 2022.

“Tungependa kushukuru serikali ya Ujerumani kwa mchango wa ukarimu wao ambao utasaidia kutoa usaidizi unaohitajika kwa ufanisi katika jamii zilizo hatarini zaidi, zinazotegemea kilimo katika maeneo yaliyoathiriwa zaidi,” amesema Dongyu.

Mkurugenzi Mkuu huyo wa FAO ameongeza kuwa “kukuza shughuli za kilimo na kuendeleza maisha ya watu wa vijijini ni njia ambayo italeta manufaa makubwa ya kuepusha mzozo mkubwa wa kutokuwa na uhakika wa chakula. Pengo la sasa la ufadhili bado linatatiza kwa kiasi kikubwa juhudi zetu za kutoa msaada wa haraka na wa kutosha wa kuokoa maisha na kujikimu kwa wale wanaouhitaji zaidi. Bado hatujachelewa kuepusha janga la kibinadamu mwaka 2022, lakini rasilimali lazima zipatikane mara moja.”

Namna fedha zitakavyotumika

Kwa ufadhili huo mpya kutoka kwa Ujerumani, FAO itasaidia zaidi ya kaya 115,000 za vijijini zilizo katika mazingira magumu katika nchi tatu zilizoathiriwa zaidi na ukame ambazo ni Ethiopia, Kenya na Somalia.

Mtoto mvulana wa umri wa kwenda shule akiwasaidia wanaume kuwanywesha maji mifugo katika kijiji cha Bandarero kilichoathiriwa na ukame huko Kaunti ya Moyale, Kenya.
Rita Maingi/OCHA
Mtoto mvulana wa umri wa kwenda shule akiwasaidia wanaume kuwanywesha maji mifugo katika kijiji cha Bandarero kilichoathiriwa na ukame huko Kaunti ya Moyale, Kenya.

Lengo ni kuhakikisha upatikanaji wa chakula na bidhaa nyingine muhimu ikiwa ni pamoja na maji kwa ajili ya wanyama na umwagiliaji, huduma za mifugo na elimu, kulinda na kurejesha maisha ya uzalishaji na kurejesha uwezo wa kujitegemea katika jamii zilizoathirika na ukame.

Nchini Ethiopia, FAO itasaidia kaya 65,000 kupitia kutoa chanjo ya mifugo, ujenzi wa kliniki 30 za afya ya mifugo, ukarabati wa vituo vya maji, na kutekeleza uchinjaji wa mifugo.

Nchini Kenya, kaya 35,000 zitapata usaidizi wa huduma za kuendeleza mifugo yao na kutoa lishe ya kutosha kwa mifugo, ambayo itawezesha wanyama kuendelea kutoa maziwa, kama chanzo cha chakula na mapato kwa jamii. Aidha, FAO itatoa fedha taslimu kwa ajili ya kusaidia walio hatarini zaidi kupata vyakula na huduma za kimsingi.

Nchini Somalia, shirika hilo litasaidia zaidi ya kaya 16,500 kupitia utoaji wa fedha taslimu, na wengine kupata fedha kupitia programu za kufanya kazi. Fedha hizo zitatumika kusambaza vifurushi vya malisho ya wanyama, mbegu zinazostahimili ukame ambazo zitaenda sambamba na msaada wa umwagiliaji.