Vijana tumekutana kutoa mawazo bunifu yanayoweza kuokoa na kuilinda bahari:Nancy Iraba
Vijana tumekutana kutoa mawazo bunifu yanayoweza kuokoa na kuilinda bahari:Nancy Iraba
Tukiwa bado kwenye mkutano huo wa Umoja wa Mataifa kuhusu bahari, mbali ya kikao cha ngazi ya juu cha viongozi makundi mbalimbali yalianza kukutana mwishoni mwa wiki likiwemo kongamano la vijana.
Nancy Iraba mwanasayansi wa masuala ya bahari kutoka chou kikuu cha Dar es salaam nchini Tanzania ni miongoni mwa wanaohudhuria kongamano hilo la vijana na bahari akiwakilisha taifa lake na hapa anaeleza linajikita na nini? “Limejikita katika kuhakikisha kwamba tunaleta mawazo ya kibunifu katika maeneo mbalimbali ya bahari, ambapo maeneo hayo ni pamoja na katika kuangalia maeneo ya chakula katika bahari yetu, kuangalia uchafuzi katika bahari zetu unaendaje? Na vilevile tunaenda kuangalia matatizo kama ramani ya bahari yetu kwa sababu bahari yetu kama tunavyoijua ni asilimia 5% tu ndio ipo katika ramani nzuri lakini kuna kama asilimia 95% ambayo bado hatuifahamu. Lakini vilevile tunaenda kuangalia mambo ya kupunguza uchafuzi wa mazingira katika bahari zetu.”
Nancy ameenda mbali zaidi na kufafanua ni jinsi gani vijana hao wanaotoka kila pembe ya dunia watatoka na mawazo bunifu yanayohitajika “Tuko vijana zaidi ya 200, ambapo tumewekwa katika makundi mbalimbali na tunaangalia hizo changamoto katika bahari zetu na kuona kwa umoja wetu kwa jinsi ambavyo tumetoka katika mataifa mbalimbali, kwa kiasi gani tunaweza kuleta suluhu za pamoja ambapo zuluhu hizo zinaenda kuangalia pia katika Nyanja za ubunifu lakini pia katika nyanja ya kutunga sera, kwa sababu tunajua kwamba kuna ulazima wa sisi kama vijana kuweza kuungana pamoja na serikali yetu kuweza kuwa na masuluhisho ambayo bahari yetu kwa baadaye inaweza kuwa katika mikono salama zaidi.”
Mkutano huo wa bahari wa Umoja wa Mataifa uliofunguliwa rasmi leo unatarajiwa kufunga pazia Julai Mosi.