Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tuondoke Lisbon na mwelekeo sahihi wa kulinda baharí – Rais Kenyatta

Washiriki wa mkutano wa kimataifa kuhusu Bahari unaoendelea huko Lisbon Ureno, akiwepo muigizaji na mchechemuzi wa afya ya bahari, Jason Momoa (aliyevaa shati jeupe)
UN /Eskinder Debebe
Washiriki wa mkutano wa kimataifa kuhusu Bahari unaoendelea huko Lisbon Ureno, akiwepo muigizaji na mchechemuzi wa afya ya bahari, Jason Momoa (aliyevaa shati jeupe)

Tuondoke Lisbon na mwelekeo sahihi wa kulinda baharí – Rais Kenyatta

Tabianchi na mazingira

Mwenyekiti mwenza wa Mkutano wa Pili kuhusu Bahari unaofanyika huko Lisbon, Ureno Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya ametaka vijana kuwa kiti cha mbele katika mashauriano yoyote kuhusu mustakabali wa bahari.

Vijana wana majawabu ya kulinda baharí – Rais wa Kenya

Wanafunzi huko Watamu nchini Kenya wakisaidia uhifadhi wa bahari kwa kufanya usafi na kumrejesha kasa baharini
UNEP/Cyril Villemain
Wanafunzi huko Watamu nchini Kenya wakisaidia uhifadhi wa bahari kwa kufanya usafi na kumrejesha kasa baharini

Akihutubia wakati wa ufunguzi wa mkutano huo, Rais Kenyatta amesema kauli yake hiyo inazingatia kile alichoshuhudia vijana wakiwasilisha katika jukwaa tangulizi la vijana kuhusu bahari.

“Hatua za kuhamasisha dhidi ya baharí walizowasilisha jana, imeonesha kuwa vijana ni na wanaweza kuwa sehemu ya majawabu,” amesema kiongozi huyo wa Kenya.

Rais Kenyatta ameongeza kuwa “iwapo tutasimamia vizuri bahari tena kwa uendelevu zaidi, inaweza kuzalisha chakula kingi mara sita zaidi, kuchochea nishati endelevu mara 40 zaidi kuliko sasa na kusaidia kuondoa kutoka lindi la umaskini mamilioni ya watu duniani kote na pia kuinua uchumi sambamba na mnepo wa kimazingira.”

Ni kwa mantiki hiyo amewaambia washiriki matarajio ni kwamba kila mmoja ataondoka Lisbon akiwa na uelewa dhahiri juu ya mbinu mbalimbali za kuchangisha fedha na mwelekeo katika kulinda bahari.

Kitalu cha Matumbawe, Fiji.
Reef Explorer Fiji
Kitalu cha Matumbawe, Fiji.

Bahari imenusuru Ureno – Rais wa Ureno

Mwenyekiti mwenza na mwenyeji wa mkutano huo, Rais Marcelo Rebelo de Sousa, akawajulisha washirika kuwa, “Ureno iko hivi sasa kama ilivyo kutokana na bahari.”

Amesema kuwa Lisbon imekuwa pahala sahihi kabisa pa kufanyia mkutano kwa sababu bahari imekuwa muhimu katika marekebisho yaliyofanya Ureno kuwa kama ilivyo hivi sasa.

Uvuvi wa kukokota nyavu ni hatari – Rais wa Colombia

Akizungumza pia katika mkutano huo, Rais wa Colombia Iván Duque Márquez ametaja mbinu mpya ya uvuvi ya kukokota nyavu ya kuvulia samaki kwa kutumia boti moja au zaidi ili kusaka na kuvua samaki, akisema inaharibu sekta hiyo akifananisha na ukataji wa misitu baharini.

“Ukokotaji wa nyavu chini ya bahari kwa kutumia boti moja au zaidi ni sawa na kukata msitu wa baharini. Kwa sababu mbinu hiyo inaharibu matumbawe” amesema Rais Márquez akionya kuwa, “na kwa kufanya hivyo kunatoa kiwango kikubwa cha hewa ya ukaa sawa na ile inayozalishwa na sekta ya anga kila mwaka. Na zaidi yah apo, kuharibu matumbawe kunatishia makazi ya asilimia 45 ya viumbe vya bahari.”

Mikoko baharini
Maktaba
Mikoko baharini

Bwana Maji (Aquaman)

Wakati wa mkutano huo, nyota wa filamu ya Aquaman na mwanaharakati Jason Momoa ambaye yuko Ureno kushiriki mkutano huo, aliteuliwa na shirika la Umoja wa Mataifa la mazingira duniani, UNEP kuwa mchechemuzi wa Uhai chini ya Maji, ikimulika lengo namba 14 la malengo ya maendeleo endelevu, SDGs.
Bwana Momoa ameshukuru kupewa jukumu hilo la kuchechemua kuhusu afya ya bahari.
“Ingawa kila kitu ni muhimu, ni kama tusipochukua hatua sasa na kufanya mabadiliko na kuzuia watu kuzungumza tu bila kuchukua hatua, ukweli ni kwamba, ni mustakabli wa vizazi vijavyo, watoto wangu, watoto wako na wajukuu zetu,” amesema Bwana Momoa.

Amesema kinachofanywa hivi sasa ni kwa ajili ya vizazi vijavyo.