Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uchumi endelevu wa buluu ni muhimu kwa nchi ndogo na wakazi wa pwani

Samaki hukaushwa kwa jua kwenye eneo la mwaloni Kigoma, Tanzania.
© FAO/Luis Tato
Samaki hukaushwa kwa jua kwenye eneo la mwaloni Kigoma, Tanzania.

Uchumi endelevu wa buluu ni muhimu kwa nchi ndogo na wakazi wa pwani

Tabianchi na mazingira

Wakati takriban asilimia 40 ya watu duniani wanaishi karibu na bahari, siku ya pili ya mkutano wa Umoja wa Mataifa wa bahari unaeoendelea mjini Lisbon nchini Ureno imelenga kuimarisha uchumi endelevu unaotegemea bahari kwakusimamia mifmu ya ikolojia ya pwani.

Idadi kubwa ya wananchi waishio pwani wanachangia kwakiasi kikubwa katika uchumi wa dunia kwa takriban dola trilioni 1.5 kwa mwaka huku matarajio yakielekeza itaongezeka na kufikia takriban dola trilioni 3 ifikapo mwaka 2030.

Uhakikishaji wa mfumo wa ikolojia ya bahari wenye afya utasaidia maishaya wananchi na kukuza ukuaji wa uchumi lakini kunahitaji usaidizi unaolenga sekta muhimu, ikiwa ni pamoja na uvuvi na ufugaji wa samaki, utalii, nishati, shughuli za meli na bandari, na uchimbaji wa madini ya baharini, pamoja na maeneo ya ubunifu kama vile nishati mbadala na teknolojia ya baharini.

Rasilimali za baharini 'muhimu'

Hii ni muhimu hasa kwa mataifa ya visiwa vidogo vinavyoendelea (SIDS), ambavyo rasilimali za baharini ni rasilimali muhimu, zinazowapa uhakika wa chakula, lishe, ajira, fedha za kigeni na burudani.

Zaidi ya hayo, kupitia uingiliaji kati wa sera unaotegemea ushahidi, mali hizi zinaweza pia kutoa michango iliyoimarishwa na endelevu katika ukuaji wa uchumi, na ustawi wa SIDS na nchi zilizoendelea duniani (LDCs).

Akishiriki katika mdahalo mkuu wa siku ya pili ya Mkutano huo, Rais wa zamani wa Ushelisheli, Danny Faure, ameieleza Idhaa ya Umoja wa Mataifa kwamba ni “muhimu sana kwamba nchi ndogo ziwe na nafasi kwenye meza, ili kuhakikisha kwamba zinaweza kuweka mbele matarajio yao na kwenda katika mwelekeo sahihi.”

Akikubali kwamba mabadiliko ya tabianchi yanaendelea kuathiri nchi yake, na nchi nyingine kadhaa za visiwa vidogo, Faure pia alitoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuendelea kuunga mkono nchi kama vile Ushelisheli. “Uchumi wa buluu ni muhimu kwa maisha ya watu wetu na mataifa.

Ninaona [uwekezaji] unakuja polepole sana na ninaamini ni muhimu sana kwamba, kimataifa, tuendelee kuzingatia, ili tuweze kujenga ushirikiano kati ya mashirika ya kiraia na sekta binafsi," alisema.

Je, uchumi endelevu wa buluu unamaanisha nini?

Licha ya kukosekana kwa ufafanuzi unaokubalika na wote wa neno uchumi wa buluu, Benki ya Dunia inafafanua kama "matumizi endelevu ya rasilimali za bahari kwa ukuaji wa uchumi, kuboresha maisha, na kazi wakati wa kuhifadhi afya ya mfumo ikolojia wa bahari.

Uchumi wa buluu unatanguliza nguzo zote tatu za uendelevu: mazingira, kiuchumi na kijamii. Wakati wa kuzungumza juu ya maendeleo endelevu, ni muhimu kuelewa tofauti kati ya uchumi wa buluu na uchumi wa bahari.

Neno hili linamaanisha kuwa mpango huo ni endelevu wa mazingira, unajumuisha na unastahimili tabianchi. Pamoja na kutoa bidhaa na huduma zinazoweza kupimika kwa njia za fedha, miamba ya matumbawe, mikoko, nyasi bahari na ardhioevu, hutoa huduma muhimu za mfumo ikolojia kama vile ulinzi wa pwani na uondoaji kaboni.

Hatua sasa

Nchi za visiwa vidogo zinazoendelea zinadhibiti asilimia 30 ya bahari na bahari zote.

Lakini je, SIDS na sekta binafsi zinawezaje kujenga ubia sawa na unaowajibika kwa ajili ya bahari endelevu? Wakitoa wito wa utekelezaji wa ahadi zilizoainishwa katika Mfumo wa Utekelezaji wa haraka wa SIDS, unaojulikana kwa njia fupi ya SAMOA Pathway na matarajio ya Lengo namba 14 la Maendeleo Endelevu (SDG14), kuhusu uhifadhi na matumizi endelevu ya bahari, wataalam katika siku ya pili ya Mkutano walisisitiza umuhimu wa kutumia ushirikiano wa sekta binafsi ili kuweza kutumiza malengo yao.

Athari za mabadiliko ya tabianchi

Akizungumza na Idhaa ya Umoja wa Mataifa, Katibu wa Serikali ya Tuvalu, Tapugao Falefou, alisema kwamba nchi yake “haijaanza tu kuelewa mabadiliko ya tabianchi ni nini na jinsi yanavyoathiri [ulimwengu] bali pia kuelewa jinsi yanavyoathiri kimwili.”

Akielezea mmomonyoko mkubwa wa mwambao, ukame na ardhi iliyofunikwa na maji ya bahari, Falefou alisema “hilo halikutokea miaka 20 nyuma. Hizi ni athari za mabadiliko ya tabianchi ambazo ninaweza kuthibitisha, ambazo nchi kubwa zinaweza zisipate uzoefu.”

Njia ya mataifa kufanya kazi pamoja Kukiwa na mamilioni ya watu wameajiriwa duniani kote katika uvuvi na ufugaji wa samaki, wengi katika nchi zinazoendelea, mifumo ya ikolojia ya baharini na pwani yenye afya na uthabiti ni msingi kwa maendeleo endelevu.

Sekta nyingine ambazo ni muhimu kwa ustahimilivu wa nchi zinazoendelea ni pamoja na sekta ya utalii wa pwani, ambayo inachangia hadi asilimia 40 au zaidi ya pato la taifa katika baadhi ya SIDS, na sekta ya uvuvi wa baharini, ambayo hutoa takriban asilimia 20 ya wastani wa ulaji wa protini za wanyama zinazotumiwa na watu bilioni 3.2, na zaidi ya asilimia 50 ya ulaji wa wastani katika baadhi ya nchi zilizoendelea. Ngozi Okonjo-Iweala, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Biashara Duniani (WTO) aliongeza kuwa bila kuwepo kwa ushirikiano wa pande nyingi, hakuna anayeweza kutatua tatizo la Bahari.

"SIDS ina uwezo wa kuwa na uchumi mkubwa wa bahari (...) ikiwa tutafanya hivyo kwa uendelevu, tunaweza kufungua matarajio ya maendeleo", alisema hayo wakati anasisitiza kuhusu uchumi wa buluu .

Kwa kuzingatia muunganiko kati ya SDG14 na SDG 5 (usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake na wasichana) jopo la wataalam lilitetea kuongeza ushiriki wa wanawake na uongozi katika ngazi zote.

Huku wanawake wakiwa na uwakilishi mdogo sana katika sekta bahari, hasa katika majukumu ya kufanya maamuzi katika sayansi ya bahari, utungaji sera na uchumi wa buluu, jopo lilitoa wito wa kuchukua hatua zaidi na mabadiliko makubwa katika jamii.

“Tuna jukumu kubwa la kufanya chochote tunachoweza kuhakikisha uendelevu wa sayari yetu, na tukio kama hili [Kongamano] labda ni moja ya matukio muhimu zaidi katika suala la maisha ya baadaye," alisema Cleopatra Doumbia-Henry, Rais wa Chuo Kikuu cha World Maritine, kilichoko nchini Sweden.

Akirejea umuhimu wa kuangalia mazingira ya kazi ya wanawake na pengo la malipo katika uvuvi, Bi. Doumbia-Henry aliongeza kuwa “Tunatakiwa kuzingatia baadhi ya maswali haya, na ninachochoshwa nacho ni dharau kwenye huduma, tunahitaji kufanya mabadiliko, na kutekeleza, ili kuipeleka mbele.”

Ushiriki mkuu wa wanawake

Kwa Maria Damanaki, mwanzilishi wa Leading Women for the Ocean, mpango madhubuti wa utekelezaji unahitajika, pamoja na uwepo wa sheria.

“Tunahitaji kuona wanawake kama sehemu ya uchumi wa buluu, tunahitaji kuwaona kila mahali, ili kuingiza ushiriki wao, kwa sababu bila uongozi wao, ubinadamu kwa ujumla utapoteza mengi," Bi. Damanaki alisema.

Kwa ushiriki unaotarajiwa wa zaidi ya watetezi elfu 12 wa bahari, wakiwemo viongozi wa dunia, wafanyabiashara, vijana, washawishi, na wanasayansi, Mkutano utaendelea kuwasha msukumo mpya wa kuendeleza SDG14, katika lengo kuu la kutaka hatua ya kimataifa ya kulinda maisha chini ya maji.

Hatua madhubuti zitachukuliwa ili kujenga ustahimilivu wa bahari na jumuiya endelevu zaidi, zikiungwa mkono na wimbi jipya la ahadi za kurejesha afya ya bahari.

Wiki hii Idhaa ya Umoja wa Mataifa itaendelea kukuletea habari za kila siku kwenye Mkutano huo pamoja na mahojiano, podcast, na makala ambazo unaweza kuzisoma hapa.