Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vijana ni kizazi kitakachosaidia kuokoa bahari na mustakbali wetu:Guterres

Katibu Mkuu wa UN (Kulia) akizungumza na vijana katika mkutano wa bahari wa vijana na ubunifu Lisbon, Ureno
UN Photo/Eskinder Debebe
Katibu Mkuu wa UN (Kulia) akizungumza na vijana katika mkutano wa bahari wa vijana na ubunifu Lisbon, Ureno

Vijana ni kizazi kitakachosaidia kuokoa bahari na mustakbali wetu:Guterres

Tabianchi na mazingira

Dunia lazima ifanye jitihada zaidi ili kukomesha kuzorota kwa hali ya afya ya bahari, amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres leo Jumapili, akiwataka vijana waliokusanyika Carcavelos, Ureno, kwa ajili ya jukwaa la vijana na ubunifu la Umoja wa Mataifa kuongeza kasi kwa sababu viongozi wa kizazi chake wanasuasua.

Jukwaa hilo la siku mbili limewaleta pamoja mamia ya vijana kutoka nchi zipatazo 165 wakiwa na lengo la pamoja la “kulinda bahari.” Akizungumza mbele ya watetezi 100 wa vijana waliokusanyika ili kuhamasisha, kukuza, na kuharakisha hatua za vijana kwa ajili ya bahari yetu, Bw. Guterres amesisitiza haja ya kuokoa sayari duniua.

Katika ufukwe wa Carcavelos, ukingoni mwa bahari karibu na mkondo wa mji wa nyumbani kwake, Lisbon, Katibu Mkuu ameomba radhi kwa niaba ya kizazi chake, kwa hali ya sasa ya bahari, kwa hali ya bioanuwai na hali ya mabadiliko ya tabianchi.

Wajibu wa kila kizazi

"Kizazi changu, na wale ambao waliwajibika kisiasa ambayo inanihusu tulikuwa polepole au wakati mwingine hatukuwa tayari kutambua kwamba mambo yalikuwa yanazidi kuwa mbaya na mbaya zaidi katika nyanja hizi tatu, bahari, mabadiliko ya tabianchi na viumbe hai", Bwana Guterres ameueleza umati wa watu waliokusanyika .

Ameongeza kuwa duniani kote, ulimwengu bado unaendelea kusuasua sana na lazima uchukue hatua sasa ili kuanza kukarabati bahari, kuokoa viumbe hai, na kusimamisha mabadiliko ya tabianchi, kwani "ni jukumu la kila kizazi ambalo linaenda mbali zaidi ya viongozi wa kisiasa" .

Katibu Mkuu wa Un akizungumza katika mkutano wa bahari wa UN kongamano la vijana na ubunifu mjini Lisbon Ureno
UN Photo/Eskinder Debebe
Katibu Mkuu wa Un akizungumza katika mkutano wa bahari wa UN kongamano la vijana na ubunifu mjini Lisbon Ureno

Wakati wa mabadiliko 

Akiwatakia washiriki mafanikio katika miradi yao, mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amehitimisha wa kutoa wito kwa kizazi cha vijana kuchukua hatua. 

"Kizazi chenu kitakuwa muhimu sasa kuongoza kesho ili kuweza kudhibiti na kubadili mwelekeo huu na kuokoa sayari". 

Bahari kwa ajili na wanangu na vizazi vijavyo 

Kabla tu ya hotuba ya Katibu Mkuu, nyota wa filamu duniani na mwanaharakati wa masuala ya bahari, Jason Momoa alijitokeza kuzungumza kwa pamoja na mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu bahari Peter Thomson.  

Bwana. Momoa amesema kazi anayofanya ni "kwa ajili ya watoto wake na vizazi vijavyo". Akipokea kifimbo cha asili kutoka kwa mjumbe maalum Peter Thomson, Bwana. Momoa amesema kijiti hicho, ambacho kinaashiria ukweli kwamba changamoto zilizopo duniani za mabadiliko ya tabianchi na upotevu wa bayoanuwai zinahusishwa na hali ya afya ya bahari, imekuwa ikizunguka dunia na ingeendelea kufanya hivyo kama ishara ya kudumu kwa viongozi. 

“Wakati wa kuchukua hatua ni sasa. Bahari yetu iko taabani, tukichanganya nia, ari na matumaini, tunaweza kubadilisha matokeo haya,” amesema. 

Mwigizaji huyo ameongeza kuwa "Bahari, ambapo maji huanza na kumalizia safari yake, huwezesha mifumo kufanya kazi sawa kwa ustawi wa wanadamu na wasio wanadamu. Bila bahari yenye afya, maisha kama tunavyoyajua yasingekuwapo”. 

Bwana. Momoa ametoa wito wa "wimbi kubwa la mabadiliko ili kuhakikisha vizazi vya leo na vijavyo vinaweza kupokea zawadi yake ya bahari". 

Heshimu maliasili 

 Akiwa amezungukwa na vijana, mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu bahari Peter Thomson ameonya kwamba vijana watakuwa wakikabiliwa na hali ya ongezeko la joto duniani la nyuzi joto mbili hadi tatu katika maisha yao. "Hiyo ni kucheza na moto," amesema. 

Akielezea kuhusu kifimbo cha asil kuwa ni ishara ya kuunganisha watu amezungumzia juu ya umuhimu wa kuheshimu maliasili na kurudi kwenye uhusiano wa usawa na maliasili hiyo. 

 "Tunapaswa kujifunza kuishi kwa heshima na bahari, sio kutupa takataka ndani yake, na sio kuipasha moto sana," ameongeza Thomson. 

Mcheza filamu  Jason Momoa (Kushoto) akiwa na wakilishi wa vijana kwenye fukwe ya  Carcavelos Lisbon Ureno katika mkutano wa bahari
UN Photo/Eskinder Debebe
Mcheza filamu Jason Momoa (Kushoto) akiwa na wakilishi wa vijana kwenye fukwe ya Carcavelos Lisbon Ureno katika mkutano wa bahari

Kenya vijana wana mchango mkubwa 

Akizungumza kwa niaba ya Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya ambayo ni muandaaji mwenza wa mkutano huo wa Umoja wa Mataifa kuhusu bahari Waziri wa mafuta na nishati Dkt. Monica Juma amesema “Inatia matumaini kuona kizazi hiki cha walinda mazingira kinasiama kidete kukabiliana na changamoto za karne ya 21 na itakuwa makosa makubwa kutothamini umuhimu waw a kushirikisha vijana  katika jitihada za kusaka suluhu endelevu kuhusu bahari zetu.” 

Bi. Monica amesema nchini Kenya vijana wana mchango mkubwa na tayari wanaendesha juhudi za kuilinda bahari kwa miradi mbalimbali “Kenya vijana wanaendesha Mirani mbalimbali kama mikoko pamoja na Vanga Blu ambao ni mradi wa kuuza hewa ukaa. Vijana pia wanaongoza katika uvuvi endelevu kuanzia kwenye miradi midogomidogo hadi mikubwa kama mradi wa maendeleo ya uvuvi na vijana ndio wanaoendesha maendeleo endelevu Kenya na huu ni ushahidi katika kundi la maendeleo na uongozi imara ambao vijana ni lazima wautoe kwa dunia.”
Jukwaa na Mkutano wa Bahari wa Umoja wa Mataifa

Jukwaa hilo limekuwa fursa ya kipekee kwa vijana kuchangia katika utekelezaji wa lengo la maendeleo endelevu namba14 (SDG14), kabla tu ya kuanza kwa mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Bahari, unaofanyika kuanzia tarehe kesho 27 Juni hadi Julai 1, kutafuta masuluhu ya kisayansi na kibunifu ili kuboresha afya ya bahari yetu.

Mkutano wa bahari wa vijana na ubunifu mjini Lisbon Ureno
UN Photo/Eskinder Debebe
Mkutano wa bahari wa vijana na ubunifu mjini Lisbon Ureno


Wajasiriamali wachanga, wabunifu na wasuluhishi wameongeza juhudi zao, miradi na mawazo yao kwa mafunzo ya kitaaluma na ulinganifu na washauri, wawekezaji, sekta ya kibinafsi na maafisa wa serikali ili kuimarisha jitihada zao.
Mmoja wa washiriki katika Jukwaa hilo Gabriela Fernandes mwenye umri wa miaka 29, kutoka Ureno, alianzisha mradi unaolenga kusoma na kupiga picha pomboo na nyangumi. Anasema "Kuzisoma kutaturuhusu kuelewa mwingiliano kati ya wanyama walio juu ya mnyororo wa chakula na wanyama wengine wa baharini, ambayo itasaidia kugundua hali ya bioanuwai ya mahali fulani".
Serikali za Ureno na Kenya kwa pamoja zimeandaa jukwaa na mkutano huo wa bahari wa Umoja wa Kimataifa kwa ushirikiano na CEiiA, Manispaa ya Cascais, Shule ya biashara na uchumi ya Nova (NOVA SBE) na muungano wa bahari endelevu (SOA) unaoungwa mkono na Idara ya Umoja wa Mataifa ya masuala ya kiuchumi na kijamii (DESA).