Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN yashtushwa na athari za kibinadamu katika miji iliyozingirwa Ukraine

Wakati machafuko yakishika kasi Ukraine watu wamesongamana kwenye kituo cha tren Lviv wakisubiri kusafirishwa kwenda Poland
© UNICEF/Aleksey Filippov
Wakati machafuko yakishika kasi Ukraine watu wamesongamana kwenye kituo cha tren Lviv wakisubiri kusafirishwa kwenda Poland

UN yashtushwa na athari za kibinadamu katika miji iliyozingirwa Ukraine

Msaada wa Kibinadamu

Katika siku ya 24 ya mashambulizi ya Urusi nchini Ukraine, na wakati mapigano yakizidi, haswa katika miji ya Mariupol, Sumy, Kharkiv, Chernihiv, Sievierodonetsk na kaskazini mwa Kyiv, mashirika ya kibinadamu yameelezea wasiwasi wao mkubwa juu ya hatima ya raia walionaswa katika miji iliyozingirwa.

Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Wakimbizi (UNHCR), mashambulizi yanayolengwa dhidi ya raia na miundombinu ya kiraia na ukosefu wa njia salama za kuondoka yanaongeza hatari na kutishia maisha ya maelfu ya raia.

"Ripoti za kibinadamu zilizopokelewa kutoka maeneo haya ni za kutisha, na tunaendelea kutoa wito wa ulinzi wa raia na miundombinu ya kiraia, na kuheshimiwa kwa sheria za kimataifa za kibinadamu," amesema Matthew Saltmarsh, msemaji wa UNHCR mjini Geneva Uswis.

Ameongeza kuwa “Katika miji kama Mariupol na Sumy, hali ya kibinadamu ni mbaya sana. Wakazi wanakabiliwa na uhaba mkubwa na unaotishia maisha wa chakula, maji na dawa".

Mahitaji ya dharura zaidi mashariki mwa Ukraine:UNHCR

UNHCR inasema inafuatilia kwa karibu mazungumzo kwa ajili ya "njia salama" na tayari imeandaa mizigo ya misaada ya kibinadamu. "Tuko tayari kutuma vifaa muhimu kwenye mji wa Sumy mara tu hali zitakaporuhusu," amesema Saltmarsh.

Huko Odessa, UNHCR inabainisha kuwa mamlaka imezindua ombi la msaada wa chakula na dawa. Hili ni kwa ajili ya kugharamia mahitaji ya watu wapatao 450,000.

Maelfu ya Waukraine wakimbilia nchi jirani
© WFP/Marco Frattini
Maelfu ya Waukraine wakimbilia nchi jirani

Mashariki mwa Ukraine, mahitaji ya kibinadamu yanazidi kuwa ya dharura. Zaidi ya watu 200,000 hawana maji katika maeneo kadhaa ya Donetsk, wakati mashambulizi ya mara kwa mara katika eneo la Luhansk yameharibu asilimia 80% ya baadhi ya maeneo, na kuacha karibu familia 100,000 bila umeme.

Kwa upana zaidi, watu walio katika mazingira magumu kama vile wanawake na watoto wanazidi kukabiliwa na vikwazo vya kupata huduma muhimuna za msingi  kama vile usafiri, chakula, maji, dawa na huduma za afya za dharura katika maeneo yaliyoathirika.

 Waakimbizi wafikia milioni 3.2, wakiwemo milioni mbili nchini Poland

Msemaji wa UNHCR ameonya kuhusu "Kiwango na ukubwa wa wimbi la wakimbizi wa ndani na wanaotoka nje ya nchi, na kwamba mahitaji ya kibinadamu, yataendelea kuongezeka kutokana na hali kuzidi kuwa mbaya,"

Zaidi ya wiki tatu baada ya kuanza kwa vita nchini Ukraine, zaidi ya watu milioni 3.2 wameikimbia nchi hiyo, ikiwa ni pamoja na karibu milioni 2ambao wameingia Poland pekee, kulingana na UNHCR, ambayo pia inaripoti angalau kuna watu milioni mbili ambao ni wakimbizi wa ndani.

Kwa mienendo kama hii ya idadi ya watu, Shirika hilo la wakimbizi linaonya kwamba mahitaji ya kibinadamu yanaongezeka kwa kasi.

Mbali na wale ambao wamelazimika kukimbia, karibu watu milioni 13 ni wahanga katika maeneo yaliyoathiriwa zaidi na vita nchini Ukraine na wanahitaji msaada wa kibinadamu na ulinzi.

Wanawake kutoka Ukraine wakitembea mbele ya mahema yaliyosimikwa huko Medyka nchini Poland kusaidia wakimbizi.
© Daniele Aguzzoli
Wanawake kutoka Ukraine wakitembea mbele ya mahema yaliyosimikwa huko Medyka nchini Poland kusaidia wakimbizi.

Dharura ya msaada wa chakula kwa wakazi wa miji iliyozingirwa:WFP

Kwa upande wake, Shirika la mpango wa chakula duniani (WFP) limeeleza wasiwasi wake kuhusu hatma ya wakazi wanaoishi katika "miji iliyozingirwa" kama vile Mariupol, likionyesha kwamba bidhaa muhimu zinakwisha kwamba misafara yake ilikuwa bado haijaweza kuingia katika mji huo.

Kulingana na shirika hilo chakula na maji kwa wakazi wa Mariupol, jiji lililozingirwa kwa zaidi ya wiki mbili, vinaisha.

WFP imeonya kwamba msaada wa kibinadamu haukuruhusiwa kuingia katika eneo hilo.

"Njia pekee ya kusaidia Mariupol ni kuita misafara ya misaada ya kibinadamu, ambayo hadi sasa haijaweza kuingia," amesema Jakob Kern, mratibu wa dharura wa WFP nchini Ukraine, akizungumza kwa njia ya video kutoka alisema Krakow, Poland.

Miji mingine iliyozingirwa kwa kiasi, kama vile Kharkiv, Kyiv, Odessa na Sumy, inaweza kupokea msaada kutoka kwa mpango wa Umoja wa Mataifa, ambao umekusanya vifaa vya kulisha watu milioni tatu kwa muda wa mwezi mmoja.

Katika hatua nyingine, kwa sababu ya uharibifu wa sehemu ya miundombinu na kuongezeka kwa mapigano, maduka mengi ya mboga na maghala sasa yamesalia tupu.

Kulingana na WFP, minyororo ya ugavi wa chakula nchini Ukraine imeporomoka.

Baada ya kuvuka mpaka kuingia Ukraine mwanamke huyu anatafuta blanketi ya kumfunika mwanaye
WHO/Kasia Strek
Baada ya kuvuka mpaka kuingia Ukraine mwanamke huyu anatafuta blanketi ya kumfunika mwanaye

Janga la njaa

"Malori na treni zimeharibiwa, viwanja vya ndege vililipuliwa kwa mabomu, madaraja mengi yamebomoka, maduka makubwa yamesambaratishwa na maghala yameondolewa", amefafanua Bwana. Kern, akibainisha kuwa matokeo ya mzozo wa Ukraine yanahatarisha wimbi la njaa kubwa kote ulimwenguni .

WFP inahofia kwamba mzozo huo utazitumbukiza mamilioni ya familia za Ukraine kwenye njaa.

"Mgogoro unaoendelea sio tu umewalazimu mamilioni ya watu kukimbia makazi yao na kuwasogeza wengine wengi kwenye ukingo wa njaa, lakini pia unatishia uhakika wa chakula ulimwenguni kote, haswa katika maeneo yenye njaa," Jakob Kern ameuambia mkutano wa waandishi wa habari mjini Geneva. .

Ikikabiliwa na ongezeko la mahitaji, WFP ina chakula, unga wa ngano uliowekwa tayari kwa viwanda vya kuoka mikate na mgao wa chakula karibu na miji iliyozingirwa ili kusambazwa na washirika na utawala wa miji hiyo.

Katika maeneo ambayo chakula kinapatikana na maduka ya reja reja yanafanya kazi kama kawaida, WFP imeanza kujaribu matumizi ya fedha taslimu au vocha kama njia ya usaidizi.

Ndani ya Ukraine, kazi ni kutoa mbadala wa minyororo ya usambazaji wa chakula uliosambaratika.

Shirika hilo la Umoja wa Mataifa pia limeanzisha vituo vya uendeshaji huko Lviv na maeneo mengine ili kusambaza na kuandaa misafara ya kibinadamu katika maeneo yenye migogoro.

Maelfu ya raia wa Ukraine wasaka hifadhi katika nchi jirani ya Ukraine
© WFP/Marco Frattini
Maelfu ya raia wa Ukraine wasaka hifadhi katika nchi jirani ya Ukraine

Takriban mashambulizi 40 dhidi ya huduma za afya:WHO

Kwa upande wa afya, shirika la afya la Umoja wa Mataifa WHO, limeripoti mashambulizi 44 dhidi ya huduma za afya tangu Februari 24, ambayo yamesababisha watu 34 kujeruhiwa na wengine 12 kuuawa.

Kati ya waathiriwa hao, wanane miongoni mwa waliojeruhiwa na wawili kati ya waliokufa walikuwa wahudumu wa afya.

Upatikanaji wa huduma za afya unakabiliwa na vikwazo vingi, ikiwa ni pamoja na uhasama unaoendelea na ukosefu wa usafiri wa umma unaozuia harakati za kusafirisha wagonjwa.

 Kulingana na WHO, baadhi ya maeneo, kama vile mji wa kusini wa Mariupol, yamekumbwa na uhaba mkubwa wa vifaa vya matibabu.

Wakati idadi ya jumla ya vitanda vinavyopatikana kwa wagonjwa walio na Covid-19 imesalia kuwa thabiti na kushuka kwa karibu theluthi moja kutoka Februari 23 hadi Machi 13, tofauti zinazingatiwa kati ya mgawanyiko wa kiutawala.

Upungufu mkubwa zaidi umeripotiwa huko Luhansk ambao ni asilimia 77%.

Aidha, idadi ya vitanda vinavyokaliwa na wagonjwa wa Covid-19 imepungua kwa asilimia 80% nchi nzima, ikionyesha ugumu wa kupata hospitali, kwa mujibu wa WHO.

Nchi ina karibu kesi milioni 5 za COVID-19 ikijumuisha vifo 107,412, kulingana na hesabu iliyotolewa na WHO mnamo Machi 17, 2022.