Winchi za WFP zawasili Yemen

Meli iliobeba winchi nne zilizonunuliwa na shirika la mpango wa chakula duniani-WFP imetia nanga katika bandari ya Hodeidah nchini Yemen.
Lengo la winchi hizi ni kuchapuza juhudi za kupakua vifaa vya msaada kwa familia za raia wa Yemen kufuatia janga kubwa la njaa kuwahi kutokea duniani.
Kwa mujibu wa WFP watu Zaidi ya millioni 22 wanahitaji msaada wa kibinadamu mkiwemo watu zaidi ya millioni 11 walio katika hali mbaya. Idadi hii ni nyongeza ya watu zaidi ya millioni moja tangu mwezi Machi mwaka wa 2017.Vilevile idadi hii inawajumulisha karibu watu millioni nane unusu wanaokabiliwa na njaa wakitegemea msaada wa chakula kutoka nje.
Wengi wa watu hao wako katika maeneo ya kati na kaskazini mwa Yemen, maeneo ambayo hufikiwa kwa haraka kupitia bandari ya Hodeidah.
Mkurugenzi tendaji wa WFP David Beasley,amesema watafanya juu chini kuona kuwa misaada sio tu ya chakula lakini pia mingine inaendelea kuingia nchini humo na kuongeza kuwa bandari ya Hodeidah ni umuhimu sana kwa msaada unaowalenga mamilioni ya raia ambao wanakabiliwa na njaa.
Kila winchi moja inauwezo wa kushughulikia tani 60 jambo ambalo litasaidi kusambaza mizigo ya msaada wa kibinadamu pamoja na misaada mingine.
Winchi hizo zilinunuliwa na WFP kwa udhamini wa shirika la Marekani la maendeleo la USAID.