Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watu nusu milioni wakimbia nyumba zao Ukraine, 330,000 waingia nchi jirani:UN

Mama akiwa ame,mbeba binti yake katika nyumba yao iliyoko karibu kabisa na msitari wa makabiliano Ukraine (Toka Maktaba)
UNOCHA/Yevhen Maloletka
Mama akiwa ame,mbeba binti yake katika nyumba yao iliyoko karibu kabisa na msitari wa makabiliano Ukraine (Toka Maktaba)

Watu nusu milioni wakimbia nyumba zao Ukraine, 330,000 waingia nchi jirani:UN

Amani na Usalama

Huku mashambulizi ya Urusi yakiendelea katika miji ya Ukraine, takriban raia nusu milioni wamekimbia makazi yao, na theluthi mbili kati yao wamevuka mipaka ya kimataifa kutafuta hifadhi katika nchi jirani, Umoja wa Mataifa umesema leo Jumapili Februari 27 .

"Idadi ya wakimbizi nchini Ukraine imesasishwa hivi punde inategemea takwimu zilizotolewa na mamlaka ya kitaifa. Hadi sasa jumla ni watu 368,000 na idadi inaendelea kuongezeka,” kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi  UNHCR.

Shirika hilo kupitia ukurasa wake wa Twitter limeandika kuwa "Takwimu zinasahihishwa kila mara. Tunapanga kutoa masahihisho zaidi wakati wa mchana," kwenye tweet, likibainisha kuwa serikali inapanga idadi ya wakimbizi ambao wanaweza "kufikia milioni 5 katika hali mbaya zaidi. matukio”.

Kwa upande wake, ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu masuala ya kibinadamu na misaada ya dharura OCHA inaripoti kuwa idadi ya wakimbizi wa ndani sasa imefikia 160,000.

64 wapoteza maisha wengine wengi majeruhi

Kwa mujibu wa OCHA mzozo wa Ukraine unaendelea kuwa na gharama kubwa ya kibinadamu, na kusababisha kuongezeka kwa idadi ya vifo vya raia, kutatiza maisha na kuharibu miundombinu muhimu ya raia. 

Kulingana na Umoja wa Mataifa, mamia ya nyumba, mifumo ya maji na miundombinu ya vyoo, shule na vituo vya afya vimeathiriwa na vita.

"Wanajeshi wa Urusi wanaingia Ukraine huku mapigano makali yakiendelea katika miji mikubwa, ikiwa ni pamoja na mji mkuu Kyiv, Kharkiv, Kherson na Odessa, miongoni mwa mingine, na pia katika maeneo yaliyoathiriwa na migogoro ya Donetsk na Luhansk",limesema shirika la OCHA katika taarifa yake ya hivi punde ya kibinadamu, ikiongeza kwamba "serikali ya Ukraine inatangaza hali ya hatari na sheria ya kijeshi".

Wakati Moscow ikitangaza kupanua wigo wa mashambulizi ya kijeshi kote Ukraine, OCHA inaripoti takriban vifo vya raia na majeruhi 240 ambapo kati idadi hiyo 64 wamepoteza maisha nchini Ukraine, baada ya kuingia kwa wanajeshi wa Urusi nchini humo wiki hii.

Tathinini ya OCHA inasema "Kati ya Februari 24 na Februari 26 , ofisi ya Haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa (OHCHR) iliripoti angalau raia 240 kuathirika vibaya na vita hivyo ambapo angalau 64 waliouawa na 176 kujeruhiwa, kote Ukraine, kufuatia mashambulizi ya anga na ardhi. ,” 

Tarehe 6 Februari kijana huyu wa miaka 16 akichungulia kutoka kwenye nyumba ya chini ya ardhi au handaki ambako mara nyingi yeye na familia yake kujifisha kunapozuka machafuko Mashariki kwa Ukraine
© UNICEF/Aleksey Filippov
Tarehe 6 Februari kijana huyu wa miaka 16 akichungulia kutoka kwenye nyumba ya chini ya ardhi au handaki ambako mara nyingi yeye na familia yake kujifisha kunapozuka machafuko Mashariki kwa Ukraine

Mamia ya nyumba zimebomomolewa au kusambaratika 

OCHA pia imesemamiundombinu ikiwemo makazi pia imeharibiwa vibaya  na mashambulizi  na idadi huenda ikaongezeka.

Takriban asilimia 85% ya majeruhi wameripotiwa katika maeneo yanayodhibitiwa na serikali.

"Rais Zelenskyy ametangaza kwamba zaidi ya wanajeshi 130 wameuawa na wengine zaidi ya 310 kujeruhiwa baada ya siku ya kwanza ya operesheni za kijeshi za Urusi," OCHA imeripoti.

Imeongeza kuwa uharibifu wa miundombinu ya kiraia umewanyima mamia ya maelfu ya watu umeme na maji. 

Mamia ya nyumba zimeharibiwa au kusambaratishwa kabisa huku madaraja na barabara zilizokumbwa na makombora zikiacha baadhi ya jamii kufungiwa masoko ya chakula na mambo mengine ya msingi.

Maisha ya Watoto yako njiapanda:UNICEF

Kulingana na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF, mashambulizi hayo ya silaha nzito nzito tayari yameharibu miundombinu muhimu ya maji na shule. 

"Iwapo mapigano yataendelea, mamia ya maelfu ya familia zinaweza kulazimika kukimbia, na kusababisha ongezeko kubwa la mahitaji ya kibinadamu," amesema Afshan Khan, mkurugenzi wa UNICEF wa Kanda ya Ulaya na Marekani, akiandika kupitia mtandao wake wa Twitter.

Mahitaji ya dharura zaidi ya kibinadamu ni huduma za matibabu ya dharura, dawa muhimu, huduma za afya na vifaa, maji safi ya kunywa na usafi, makazi na ulinzi kwa watu waliolazimika kukimbia kutoka kwenye makazi yao. 

Kituo cha ukaguzi kinafusimamiwqa na serikalihuko Marinka, Mkoa wa Donetsk. (faili)
© WFP/Deborah Nguyen
Kituo cha ukaguzi kinafusimamiwqa na serikalihuko Marinka, Mkoa wa Donetsk. (faili)

Ongezeko la 555%  ya visa vya COVID-19 kati ya Januari 15 na Februari 25

Aidha, "mashirika ya Umoja wa Mataifa na washirika wengine wa kibinadamu wamelazimika kusimamisha shughuli zao kutokana na kuzorota kwa hali ya usalama," imesema OCHA.

 Hata hivyo, "Umoja wa Mataifa na washirika wake wanadumisha uwepo wao kote nchini Ukraine na kusalia mashinani kukabiliana na kuongezeka kwa mahitaji ya kibinadamu na hatari za ulinzi mara tu hali inavyoruhusu".

Kwa upande wa afya, ongezeko la hivi majuzi la mzozo linakuja wakati Ukraine inakabiliwa na kuongezeka kwa janga la COVID-19 kutokana na lahaja ya Omicron, ambayo imesababisha "Wagonjwa kuendelea kuongezeka kwa asilimia 555% kati ya Januari 15 na Februari 25."

Kulingana na OCHA, takwimu zinaweza kuwa ni kubwa zaidi ya hizi kutokana na  ukosefu wa kupima.

Takriban wagonjwa milioni 4.8 wa COVID-19 vikiwemo vifo 105,664 vimerekodiwa nchini Ukraine hadi sasa kwa mujibu wa takwimu za Februari 25 mwaka huu za Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO). 

Kufikia Februari 13, 2022, zaidi ya dozi milioni 31 za chanjo zimetolewa katika nchi hii ya Ulaya.