Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nilijifungua katikati ya mashambulizi nchini Ukraine: Mariia Shostak

Mariia Shostak na mwanaye Arthur wakiwa kwenye handaki la hospitali ya wazazi mjini Kyiv ambako yeye na akina mama wengine na familia zao wamepewa hifadhi
© Mariia Shostak via UNFPA
Mariia Shostak na mwanaye Arthur wakiwa kwenye handaki la hospitali ya wazazi mjini Kyiv ambako yeye na akina mama wengine na familia zao wamepewa hifadhi

Nilijifungua katikati ya mashambulizi nchini Ukraine: Mariia Shostak

Amani na Usalama

Mariia Shostak, mwanamke mwenye umri wa miaka 25 anayeishi katika mji mkuu wa Ukraine wa Kyiv, alianza kupatwa na uchungu tarehe 24 Februari, siku ambayo Shirikisho la Urusi lilianzisha mashambulizi ya kijeshi nchini Ukraine, na alijifungua mtoto huku kukiwa na sauti za ving'ora vikiashiria mashambulizi ya anga.

Anaelezea magumu na machungu aliyopitia na kuyavumilia, wakati akikileta maisha mapya katika ulimwengu huu ulioghubikwawa hatari ya ghafla na mbaya.

"Nilikuwa na ujauzito wenye changamoto, na nilienda hospitali ya masuala ya uzazi mapema ili mimi na mtoto tuwe chini ya uangalizi wa matibabu.”

Nilipoamka tarehe 24 Februari, skrini ya simu yangu ilikuwa imejaa ujumbe kutoka kwa ndugu na jamaa. Hata kabla ya kusoma, niligundua kuwa kuna kitu kilikuwa kimetokea.

Asubuhi hiyohiyo, nilipata uchungu ulioanza kidogokidogo na, alasiri, tulihamishwa kutoka owodini juu hadi kwenye mahandaki chini ya ardhi kwa mara ya kwanza. Ilikuwa inatisha. Usiku, sikulala.

Uchungu ulishika kasi, na Habari za mashambulizi hazikusaidia

Uchungu ulioengezeka kwa kasi na tarifa za machafuko zilizidisha adha. Mapema asubuhi ya tarehe 25 Februari, daktari alinichunguza na kuniambia kwamba ningejifungua siku hiyo. Nilimpigia simu mume wangu nyumbani aje.

Safari ambayo kwa kawaida huchukua dakika 20 ilichukua karibu saa nne kwa sababu ya foleni kwenye kituo cha mafuta, maduka ya chakula na maduka ya dawa.

Yuril ambaye ni mume wa Bi. Shostak akiwa amembeba mtoto wao mchanga hospitalini. Mpango wao ni kuendelea kuishi kwenye handaki nyumbani mwao.
© Mariia Shostak via UNFPA
Yuril ambaye ni mume wa Bi. Shostak akiwa amembeba mtoto wao mchanga hospitalini. Mpango wao ni kuendelea kuishi kwenye handaki nyumbani mwao.

Nilikuwa na bahati

Nilikuwa na bahati wakati wa kujifungu, haikutokea kwenye handaki ingawa baadhi ya wanawake walijifungua kwenye mahandaki katika chumba kilichopangwa kwa madhumuni haya.

Nilianza katika chumba cha kujifungulia lakini ilibidi nihamishiwe hadi kwenye chumba cha upasuaji kwa ajili ya kuupasuliwa.

Baadaye, ving’ora vya mashambulizi ya anga vilipolia, wafanyakazi wa hospital na wauguzi walitaka kunitoa na kunipeleka kwenye handaki lakini nilikataa.

Kwa sababu ya maumivu, sikuweza hata kuongea, achilia mbali kutembea popote. Wakati wote niliokuwa hapo nilitengwa na ulimwengu wa nje, ambapo labda ndio wakati pekee nilisahau kuhusu vita

Hofu, uchovu na maumivu

Baada ya upasuaji, nilikuwa katika chumba cha wagonjwa mahututi kwa saa kadhaa, sikuwa tena na ganzi. Nilikuwa na wasiwasi kwani sikujua mtoto na mume wangu walikuwa wapi.

Wakati huohuo, king'ora kingine cha mashambulizi ya anga kilisikika, na niliamua kushuka kwenye handaki. Nilikuwa nimevaa gauni la hospitali, bila viatu, kwenye kiti mwendo, nikiwa na katheta ya mkojo.

Nilifunikwa na blanketi na kupelekwa kwenye makazi ya dharura, ambapo nilimwona mwanangu kwa mara ya kwanza. Tulimwita Arthur.

Nilihisi hofu, uchovu, na maumivu. Siku moja baada ya upasuaji, nilipanda hadi kwenye wodi ya wajawazito na kurudi chini kwenye handaki mara kadhaa kwa siku. Tena na tena, king'ora cha mashambulizi ya anga kilisikika.

Uchovu ulipunguza hofu hadi kombora lilipogonga jengola jirani

Niliweza kulala kwa saa moja au mbili kwa siku. Muda mwingi tulikuwa kwenye handaki tukiwa tumekaa kwenye viti.

Mgongo wangu uliuma kwa kukaa, na miguu yangu bado ilikuwa imevimba kama wakati wa shida ya ujauzito.

Uchovu ulipunguza woga hadi kombora lilipogonga jengo la ghorofa karibu yetu tuliloweza kuliona kwenye dirisha.

“Mume wangu, Yurii, alisaidia, akinihudumia mimi na mtoto mchanga. Wafanyikazi wa matibabu waliandaa chakula kwenye chumba cha kulala na baadaye walitoa vitanda. Walisaidia kumweka mtoto kwenye matiti yangu aweze kunyonya, walikuwa wakiwapa dawa watoto, pia walinishika mkono nilipokuwa na shida ya kutembea.”

Ninahisi niko salama katika mji mkuu, kuna makazi ya kutosha na tunapata habari kwa wakati kutoka kwa mamlaka.

Mume wangu alitupangia kona maalum katika ghorofa ya chini ya nyumba yetu ili tukae.

“Nilizaliwa na kukulia hapa Kyiv, sina sehemu nyingine ninayoweza kuiita nyumbani. Hatutaondoka.”