Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Siku 100 za uvamizi wa Urusi kwa Ukraine, ustawi wa watu umeathirika sana

Mwanamke wa miaka 70 akisimama nje ya mlango wa nyumba iliyoteketezwa Chernihiv, Ukraine.
© UNICEF/Ashley Gilbertson
Mwanamke wa miaka 70 akisimama nje ya mlango wa nyumba iliyoteketezwa Chernihiv, Ukraine.

Siku 100 za uvamizi wa Urusi kwa Ukraine, ustawi wa watu umeathirika sana

Amani na Usalama

Leo ni siku 100 tangu kuanza kwa uvamizi wa Urusi nchini Ukraine ulioanza tarehe 24 Februari mwaka huu. Mashirika ya Umoja wa Mataifa na wadau wake wanasema katika hizi siku 100 tu, uvamizi huu ambao ni ukiukaji wa Katiba ya Umoja wa Mataifa, umewaweka watu wa Ukraine katika hali ya kutisha.

Ni siku 100 za mahangaiko, milio ya risasi, watoto kutenganishwa na wazazi wao, na hata kushambuliwa kwa miundombinu ya kutoa huduma za afya.   

Shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni, WHO linasema Siku 100 za vita zimeweka mfumo wa afya wa Ukraine chini ya shinikizo kubwa. Takwimu za shirika hilo zinasema kuwa kufikia jana yaani Juni 2, kumekuwa na mashambulio yaliyothibitishwa 269 yakilenga miundombinu ya afya, na kuua watu wasiopungua 76 na kujeruhi 59. 

Kwa upande wake shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR, linasema  baada ya siku 100 za uchungu, sasa linajielekeza katika kuwahakikishia watu wa Ukraine makazi kwani baridi linakuja na kwa kawaida hali ya baridi katika ukanda huo ni kali mno.  

Nalo shirika la Umoja wa Mataifa la idadi ya watu na afya ya uzazi, UNFPA limesema Siku 100 za vita ya Ukraine nchini Ukraine zimeathiri vibaya mamilioni ya wanawake na wasichana na kwamba kundi hilo liko katika hatari kubwa ya kuhatarisha maisha ya kuongezeka kwa unyanyasaji wa kingono na kimwili, usafirishaji haramu wa binadamu, unyonyaji na unyanyasaji, na kunyimwa ufikiaji wa huduma na bidhaa muhimu. 

UNFPA ilikadiria kuwa mwanzoni mwa vita kulikuwa na wanawake wajawazito 265,000 nchini Ukraine na kwamba  katika hizi siku 100 ripoti za unyanyasaji wa kijinsia, ikiwa ni pamoja na ubakaji katika maeneo yaliyoathiriwa na vita, zimekuwa za kutisha. 

Mratibu wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya mgogoro wa Ukraine, Amin Awad akihojiwa na UN News kuhusu kutimia kwa siku 100 za uvamizi wa Urusi kwa Ukraine, akirejelea kama alivyoweka wazi Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, amesema hii ni vita isiyo na maana na haipaswi kuendelea, "Sio vita ya ndani ya Ukraine tu. Ina athari za kidunia kati ya mashariki na magharibi. Kwa hivyo, inapaswa kukoma. Haina maslahi kwa mtu yeyote.” 

Wajumbe wa Tume Huru ya Kimataifa ya Uchunguzi wa Umoja wa Mataifa kuhusu Ukraine wanatarajiwa kufanya ziara yao ya kwanza nchini Ukraine kuanzia tarehe 7 hadi 16 Juni 2022. Makamishna hao wanakusudia kutembelea maeneo kadhaa nchini humo, ikiwa ni pamoja na Lviv, Kyiv, Kharkiv na Sumy, ili kupata taarifa za moja  kwa moja kuhusu madai ya ukiukwaji wa haki za binadamu, na ukiukaji wa sheria za kimataifa za kibinadamu, na kukutana na waathirika, mashahidi na watu waliokimbia makazi yao.